Somo I: Yer. 31:31-34,
Somo II: Ebr. 5:7-9, Injili : Yn. 12:20-33
Tumebakiza wiki moja
kabla ya kuadhimisha mateso na kifo cha Kristu. Katika dominika ya leo kanisa
linaanza kutuingiza katika tafakari ya mateso ya Kristu. Neno la Mungu leo
linatufunulia ukweli kuhusu thamani ya mateso ya Kristu ambaye aliteseka kama wanadamu
wengine. Ili kuweza kuona thamani ya mateso katika maisha inategemea namna
tunavyoyapokea. Kristu aliyapokea mateso kwa imani na hivyo Baba yake wa
Mbinguni akamuonesha thamani hiyo na kumpa uhakika wa utukufu baada ya mateso. Baada
ya kuelewa thamani hiyo Kristo alitii sauti ya Mungu katika kuyakabili mateso
Katika somo la kwanza
nabii Jeremia anawapa Waisraeli habari njema ya Mungu kufanya agano jipya nao. Katika
agano hili jipya Mungu anasisitiza juu ya uhusiano wake na mwanadamu unaodai
kujitoa bila kujibakiza ndani ya moyo wa mtu. Anaposema kuwa ataiandika sheria
yake ndani ya moyo wa mtu anamanisha kuwa anataka watu wampende Mungu si kwa
matendo ya nje tu bali kwa moyo na akili zao zote. Watu wote watamjua Mungu
ndani ya mioyo yao kwa sababu watakuwa wameondolewa giza la dhambi ya asili kwa
agano hili jipya. Waisraeli walivunja agano la wanza kwasababu walisisitiza
zaidi juu ya uhusiano wao na Mungu kwa matendo ya nje kuliko kujitoa nafsi.
Kujitoa nafsi kwa ajili ya Mungu kunahitaji kutoa sadaka kubwa. Hakuna sadaka
kubwa isiyokuwa na maumivu au mateso. Tunapokosa ujasiri wa kuyakabili mateso
na maumivu hayo hautewezi kuwa waaminifu
kwa agano.
Katika somo la pili
mwandishi kwa Waebrania anamuonesha Kristu Kuhani mkuu aliyetesekea pamoja nasi
ili atufundishe namna ya kuyakabili mateso. Kwa sababu ya uchungu mkubwa
anaoupata Kristu kutokana na mateso sala yake kwa Mungu ni ya kilio cha sauti
na kumwaga machozi kama ilivyo kwa mwanadamu mwingine yeyote anapokuwa katika
mateso makali. Kristu anatufundisha kupokea mateso kwa imani ili tuweze
kujifunza mapenzi ya Mungu kwetu katika mateso yake. Kristu alijifunza kuwa
mateso yake ni kwa ajli ya ukombozi wetu na baada ya kutambua hilo anakubali
kutii mapezni ya Mungu. Kwa sababu ya
kupokea mateso kwa imani mateso yanamfanya Kristu awe mkamilifu katika kazi
yake , hivyo nafsi tukiyapokea mateso kwa imani
tunakuwa wakamilifu katika kumtumikia Mungu.
Katika somo la injili
Kristu anatufundisha kuwa kukubali na kupokea mateso yanayotokana na kujikana
nafsi zetu, kutolea sadaka yale tunayoyapenda sana, kujikatalia haki zetu
ikibidi haki ya kuishi kwa ajili ya kumtumikia Mungu na watu tutatoa mazao
mengi na tutazisalimisha nafsi zetu katika uzima wa milele. Tutatoa mazao kama
vile upendo, unyenyekevu , uvumilivu, msamaha na utu wema. Kuamua kutii mapenzi
ya Mungu katika mateso makali kuna ugumu mkubwa, kuna hofu nyingi na kunahitaji sadaka kubwa. Hivyo kutii kwa
kweli ni kuamuna kusonga mbele katika hofu nyingi na kushinda na hapa ndipo
penye fadhila. Kristu alikabiliana na ugumu na hofu nyingi katika kuamua kutiii
mapenzi ya Mungu katika mateso yake. Alifika mahali alimuomba Baba amuepushe na
saa ya mateso lakini alikabiliana na hofu na ugumu wote na akaweza kutii.
Tukiwa watu wa sala daima Mungu hatuachi
peke yetu katika kuyakabili mateso. Atakuwepo kwa ajili ya kututia moyo,
atatuonesha mapenzi yake na namna ya kutii sauti yake. Katika injili Yesu anapokuwa
na mahangaiko na hofu nyingi kuhusu mateso atakayoyapata sauti inatoka mbinguni
na kumhakikishia kuwa mwisho wa mateso hayo ni utukufu.
Mwanadamu anapitia
mateso mbalimbali katika maisha yake. Yapo mateso yanayotokana na dhambi zake
mwenyewe, mateso haya si ya kuyakimbilia tunapaswa kufanya juhudi ya kuyaepuka.
Kristu amekuja kutuondolea mateso haya kwa kifo chake msalabani na tukitaka
kuendelea kuyaepuka ametuachia sakramenti zake na hasa ya ekaristi na kitubio.
Yapo mateso ambayo hatuwezi kuyaepuka kwa sababu ya udhaifu wa miili yetu, kwa
mfano, mateso yatokanayo na magonjwa. Haya ni mateso ambayo hata Kristu
mwenyewe hakuyaondoa katika ulimwengu huu. Badala yake ametufundisha namna ya
kuyakabili kwa imani ili tuweze kutambua mapenzi yake kwetu. Mateso haya tukiyapokea
kwa imani na matumaini yanatusaidia katika malipizi ya dhambi zetu na za
ulimwengu. Yapo mateso mengine ambayo hayaepukiki ikiwa tunataka kuwa
wakimilifu kiroho na hata kimwili, mateso haya yanatokana na uamuzi wetu wa
kujikatalia nafsi zetu, mambo tunayoyapenda kwa ajili ya Mungu na jirani.
Unapojikatalia chakula katika kipindi hiki cha kwaresima unapata maumivu ya
njaa lakini lengo lako ni kujitawala katika chakula ili upate nafasi ya
kujibandua katika vitu vinavyopita na kukuza uhusiano wako na Kristu
Tunapoadhimisa dominika
hii ya tano tumuombe Mungu atujalie kupokea mateso kwa moyo wa imani na
matumaini ili tustahilishwe wokovu kwa mateso hayo.
No comments:
Post a Comment