Tuesday, 26 May 2015

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU, MAY 31, 2015

Kum 4:32-34, 39-40, Rum 8:14-17, Inj Mt 28:16-20

Leo ni sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kanisa linaadhimisha fumbo la Mungu mmoja katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa kweli hili ni fumbo mama kati ya mafumbo yote ya Kikristu kwasababu linamhusu Mungu mwenyewe. Kwa akili ya kibinadamu tunaweza kwa kiasi fulani kufahamu juu ya uwepo wa Mungu, kwa mfano, kila tunapotafakari juu ya maajabu ya uumbaji. Lakini ukweli  kwamba Mungu huyu ana nafsi tatu tofauti zinazoshiriki Umungu mmoja tunaweza kuufahamu tu ikiwa Mungu mwenyewe anaamua kutufunulia na kwa fadhila ya imani. Neno la Mungu leo linatufunulia ukweli huu, tunahitaji paji la imani ili kupokea na  kuufahamu ukweli huu.

Mungu wetu ni mmoja mwenye nafsi tatu, hili ni fumbo kweli kwetu sisi wanadamu kwani kila tunapojaribu kuelewa ni kwa namna gani hili linawezekana tunashindwa kwani akili yetu ni finyu sana kumuelewa Mungu asiye na mipaka na wa milele. Tunapata shida kuelewa kwasababu kwetu sisi nafsi ya mtu ni ya kipekee inafikiri na kutenda katika upekee na hivyo kuwa na nafsi mbili na zaidi maana yake ni kuwa na watu wawili na zaidi walio tofauti katika kufikiri na kutenda. Kila tunapojaribu kuzitazama nafsi tatu za Mungu kwa namna yetu hii ya kibinadamu tunakwama kwani ufunuo wa neno la Mungu unatueleza kuwa katika Mungu hakuna nafsi inayofikiri na kutenda kipekee, Baba yu ndani ya Mwana na Mwana yu ndani ya Baba kadhalika wote wako ndani ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu yu nadani ya Baba na Mwana. Nafsi zote tatu za Mungu zinafikiri na kutenda katika umoja kamili wa Umungu. Anachofikiri baba ndicho anachofikiri Roho Mtakatifu na Mwana pia.  Hivyo nafsi tatu hazifanyi miungu watatu, bali zote zi na asili ya Umungu ule ule, na hili ndilo fumbo lenyewe

Ufunuo wa ukweli huu wa Utatu Mtakatifu watuonesha kuwa Mungu wetu yu hai,  na zaidi ya hayo anatupenda sana. Mtume Paulo kwenye somo la pili la leo anaonesha kuwa Mungu wetu anatupenda sana na hili linaonekana pale anapoamua kutufanya sisi wana wake kupitia nafsi yake ya pili yaani Kristu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ambaye Paulo anasema yeye ndiye anayeshuhudia tukio hilo la sisi kufanyika wana. Roho Mtakatifu nafsi ya tatu anatuwezesha sisi kumtambua nafsi ya kwanza ya Mungu kuwa ni Baba yetu. Anatufanya sisi kuwa ndugu wa Kristu, warithi pamoja naye wa mateso na utukufu. Katika somo la kwanza pia laonesha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kupitia matendo makuu ya kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri.

Katika somo la injili, mwinjili Matayo anaonesha umoja wa Umungu  wa nafsi tatu. Kristu nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeweka sakramenti saba, na kwa namna ya pekee ubatizo, ambazo ni alama wazi ya wokovu wetu kwa kifo chake msalabani.  Kristu anapowatuma wafuasi wake waende ulimwenguni kote na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake anawaamuru wabatize kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii maana yake ni kwamba katika kazi ya ukombozi ambayo Kristu, nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeifanya, nafsi zote tatu zinashiriki katika kazi hiyo kwa ukamilifu wake.

Sherehe hii ya Utatu Mtakatifu inalenga kutukumbusha mambo makubwa mawili; moja ni kwamba kujua ukweli huu kuhusu Mungu wetu anayeishi na kutupenda sana, kunatupa wajibu wa kumrudishia sifa na shukrani kwa maneno na matendo yetu. Ingawaje sifa zetu hazimzidishii  Mungu chochote lakini zatufaa kwa waokovu wetu. Tunamsifu Mungu kwa nafasi ya kwanza kwa sala na ibada zetu. Wapo watu wanaodai kuwa hakuna ulazima wa kwenda kanisani kusali dominika alimradi wanajitahidi kuepuka maovu na kutoa misaada. Hii si kweli kabisa , kuna umuhimu na ulazima wa kumkiri Mungu kwa midomo yetu kupitia sala, nyimbo na ibada, tendo hili linaelezea na kuimarisha imani na  upendo wetu kwa Mungu na linatupa nguvu ya kuishi vema amri ya mapendo. Katika ibada ya misa takatifu tunachota neema ya kuishi kitakatifu.

Jambo la pili tunalokumbushwa leo ni umoja. Katika Mungu kuna nafsi tatu tofauti lakini zinatenda kwa umoja kamili wa Umungu. Tunapaswa kuwa na umoja kwanza wa sisi wenyewe ndani yetu, umoja ambao unalenga kulinda hadhi yetu kama wakristu. Ikiwa akili inayoelewa mambo, haina umoja na utashi unaoamua kulingana na mwangaza wa akili daima nafsi ya mtu itakuwa katika fujo. Ikiwa dhamiri ya mtu haina umoja na utashi wake pia mtu hukosa amani na daima atakuwa mtumwa. Kama hakuna umoja kati ya utashi wa mtu na mwili wake matokeo yake pia ni vurugu ndani ya mtu. Kwa mfano, ikiwa dhamiri ya mtu inamsukuma kuacha ulevi lakini utashi wake unashindwa kuamua kadiri ya matakwa ya dhamiri yake njema, mtu huyu daima atakosa amani kwani dhamiri yake itaendelea kumsuta kila mara kwa kuamua kinyume na  matakwa yake. Kama ndani ya mtu kuna umoja daima kutakuwa na amani na matunda yake ni kwamba familia zitakuwa na umoja, jumuiya, nchi na dunia kwa ujumla itakuwa na umoja.

Tusali daima kuomba paji la Roho Mtakatifu la Ibada ili tuendelee kuusifu Utatu Mtakatifu daima na zaidi ya hayo tuuishi umoja usiogawanyika unaopatikana katika Utatu Mtakatifu.



Friday, 22 May 2015

DOMINIKA YA PENTEKOSTE, MWAKA B. MAY 24, 2015

I.                    Mdo 2:1-11    II. 1 Kor 12:3b-7, 12-13  Inj. Yn 20:19-23
Siku ya hamsini ya kipindi kitakatifu cha Pasaka inahitimishwa na Dominika ya Pentekoste, kanisa linapokumbuka kazi ya Roho Mtakatifu kwa Mitume, mwanzo wa Kanisa na mwanzo wa utume wake kwa lugha, watu na mataifa yote. Roho mtakatifu analitakasa kanisa, analifariji katika mahangaiko yake ya hapa duniani na pia analiwezesha katika utume wake kupitia vipaji, karama na huduma mbalimbali anazozimimina kwa wanakanisa kadiri apendavyo

Katika injili leo Yohane anatupatia simulizi la Yesu mfufuka akiwatokea mitume katika chumba na anapowatokea anawaambia mambo kadhaa ambayo kwa kweli yanagusa pamoja na mambo mengine  utume wetu kama wana kanisa

Tunajifunza kuwa Kristu anahitaji Kanisa katika kuendeleza kazi yake ya ukombozi aliyoianzisha. Baada ya kupaa kwake mbinguni mitume wanapaswa kuwaongoza wanakanisa kwenda ulimwenguni pote na kwa kila kizazi kushuhudia ufufuko wa Kristu ili ulimwengu mzima upate wokovu. Twajua kuwa Kristu ndiye kichwa yaani Kiongozi wa Kanisa lakini anahitaji miguu, mdomo na mikono ya kupeleka ujumbe wake kwa watu wote akiwa ameketi kuume kwa Baba. Kanisa ndio miguu, mikono na mdomo wake. Kristu anategemea kanisa lenye wanadamu wasio wakamilifu wanaopambana kuufikia wokovu wao wenyewe kwanza halafu watu wengine. Kwa hiyo ni wazi kwamba kushuhudia wanakanisa wakianguka katika udhaifu  isiwe kigezo cha kukata tamaa na kulikimbia kanisa kwa sababu Kristu mwenyewe amechagua Kanisa dhaifu lifanye kazi yake.

Katika kufanya kazi ya utume Kanisa linamuhitaji sana Kristu. kwa sababu kanisa linafanya kazi ya utume hivyo lazima kuwepo na yule aliyelituma, ujumbe wa kupeleka, nguvu na mamlaka ya kupelekea ujumbe huo. Kristu ndiye anayelituma Kanisa, na analipa ujumbe wa wokovu kwa watu wote na zaidi ya hayo analipatia nguvu na mamlaka ya kupeleka ujumbe huo kupitia Roho Mtakatifu tunayempokea leo katika sherehe ya Pentekoste. Katika udhaifu wake kanisa linahitaji kujishikamanisha na Kristu daima ili liweze kufanikiwa maana Kristu mwenyewe anatuambia bila yeye hatuwezi chochote.

Kama Baba alivyomtuma Mwana ulimwenguni ndivyo Kristu anavyolituma Kanisa lake. Utume wa Kristu uliwezekana na ulifanikiwa kwa sababu tu Kristu alikuwa mtii kwa yule aliyemtuma na pia alimpenda sana. Kanisa linamwakilisha Kristu duniani hivyo daima linapaswa kuwa mtii kwake ili lisije kupeleka ujumbe wake badala ya ujumbe wa Kristu. Upendo ndio msingi wa utume wetu, yatupasa kuwa tayari kutolea maisha yetu kwa ajili ya yule aliyetutuma

 Kristu anatualika tupeleke ujumbe wa msamaha wake kwa wadhambi wanaotubu. Anapowaeleza mitume wake juu ya mamlaka ya kufunga na kufungua anawatuma waende ulimwenguni kote na kuwaeleza watu kuwa Kristu alikuja duniani kuwasamehe watu makosa yao. Atakayekuwa tayari kutubu na kuomba msamaha atasamehewa lakini yule anayekataa msamaha wake hatapokea msamaha huo.

Katika somo la pili mtume Paulo anatueleza kuwa utume wa kanisa unawezekana kwa sababu Roho Mtakatifu anagawa karama, vipaji na huduma mbalimbali kwa watu wake. Kupitia karama hizi wanakanisa wanapeleka ujumbe wa Kristu kwa watu. Karama mbalimbali zinatolewa kwa ajili ya manufaa ya Kanisa zima na wala si kwa ajili ya sifa na utukufu wa wale waliojaliwa karama hizo

Somo la kwanza ni simulizi la tukio la Pentekoste ambalo kwa kweli linaonesha kazi ya Roho Mtakatifu kwa mitume, mwanzo wa Kanisa, mwanzo wa utume wa kanisa kwa lugha, watu na mataifa yote. Ni muhimu kuelewa awali ya yote kwamba Roho Mtakatifu yupo na amekuwepo daima akifanya kazi kati ya watu hata kabla ya tukio hili ya Pentekoste. Ingawaje ni ukweli kwamba kuna kitu cha pekee kilitokea siku hiyo ya Pentekoste. Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu aliwavuvia mitume na kuwapa zawadi na karama ya ajabu ambayo hawakuwahi kuipata kabla. Uvuvio huu wa Roho Mtakatifu uliwafanya mitume walihubiri neno la Mungu kwa namna ambayo kwa mara ya kwanza iligusa mioyo ya watu na walielewa vizuri sana.

Wapo watu wanaosema kuwa mitume walipata uwezo wa kunena kwa lugha kama ishara ya kuvuviwa na Roho Mtakatifu. Kunena kwa lugha kunakozungumziwa na ule uwezo wa kutamka maneno ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuelewa, jambo ambalo lilikuwepo hata katika kanisa la mwanzo. Watu hawa wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa hiyo ndio ishara ya muhimu na ya pekee ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Mtume Paulo ameeleza kwa kirefu juu ya kipawa cha kunena kwa lugha katika (1Kor 14) lakini kwa ufupi anachoeleza ni kuwa kipaji chochote anachotoa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya manufaa ya jumuiya, la kama mtu amepewa kipaji na hakiwasaidiii wanajumuiya katika kuabudu kwao isipokuwa yule aliyepewa basi asikitumie katikati ya wanajamii hasa katika sala. Zaidi ya hayo hatuwezi kusema kuwa kiuongo kimoja katika mwili ndio chenye umuhimu kuliko vingine kwa sababu ili mwili uitwe mwili unahitaji kuwa na viunguo vyote kamili na ndio maana wasio na viungo fulani huitwa walemavu ingawaje hawajapoteza utu wao. Haiwezekani kipaji kimoja tu ndio kikawa muhimu kuliko kingine katika mwili wa fumbo wa Kristu yaani Kanisa.


Hivyo katika pentekoste si kwamba mitume walipata hiyo karama ya kunena kwa lugha kwa sababu kila walichokiongea watu walikielewa. Kipaji cha kunena kwa lugha kadiri ya Paulo ni kwa ajili ya yule tu mwenye kipaji hicho na watu wengine hawawezi kumuelewa. 

Thursday, 14 May 2015

DOMINIKA YA SABA YA PASAKA, MWAKA B. MAY 17, 2015

Mdo 1:15-17, 20a, 20c-26,  I Yoh 4:11-16, Inj. Yn 17:11b-19

Wakristu tunao uhakika kuwa  kiongozi wetu Yesu Kristu hata baada ya kupaa kwake mbinguni anaendelea kuwa pamoja nasi kutuongoza, kutuimarisha, kutubariki katika safari yetu ya kuelekea kule aliko yeye. Kwa mara nyingine leo tunakumbushwa kuwa ukristu wetu unatudai mambo makubwa sana yanayohitaji kujitoa mhanga kwa ajili ya Kristu kiongozi wetu. Peke yetu hatuwezi ni lazima tuombe msaada wake kwa njia ya sala yeye aliyetuahidi kuwa pamoja nasi mpaka mwisho wa safari.

Katika njili Yesu kuhani mkuu analiombea kundi lake kabla ya kuteswa, kufa, kufufuka na kupaa kwake mbinguni. Katika sala ya Yesu tunaweza pamoja na mambo mengi tukatafakri mambo makubwa manne kuhusu ukristu wetu.

Mkristu safi, hodari na shujaa si yule anayejitenga na ulimwengu bali yule anayeishi ndani ya ulimwengu lakini anaushinda ulimwengu. Yesu haombi kwamba tutoke ulimwenguni bali tulindwe na yule mwovu. Mara nyingi nimesikia watu mbalimbali walio katika ndoa wanawaambia mapadre na watawa kuwa afadhali wao wamechagua maisha ya kujitenga na ulimwengu kwa kuwa watawa  au  mapadre kwani wameepukana na maouvu ya ulimwengu. Ingawaje si kweli kwamba mapadre na watawa wametoka katika ulimwengu huu lakini hoja ya watu wanaofikiri hivyo kuhusu mapadre ni kwamba mtu atakuwa mkristu mzuri kama atatoka katikati ya ulimwengu uliojaa maovu jambo ambalo si la kweli. Wapendwa maisha ya ukristu maana yake ni kwenda kinyume na ulimwengu huo huo tunaoishi. Tunapaswa kuwa mashuhuda wa Kristu, kwa mfano, katika ulimwengu unaotumia mitandao ya kijamii kubomoa maaadili kwa sisi kutumia mitandao hiyo vizuri na si kuacha kutumia. Ukristu hautuweki huru dhidi ya matatizo bali unatupa mbinu za kupambana na matatizo

Wakristu tumewekwa wakfu yaani tumetengwa kwa ajili ya kazi maalumu. Sehemu ya mwisho ya sala ya kristu katika injili ya leo yaeleza ukweli huu Kristu anapoomba tutakaswe na hiyo kweli. Tumezoea kuwa mapadre na watawa tu ndio wamewakwa wakfu lakini ukweli ni kwamba kwa ubatizo wetu sisi sote tumetengwa kwaajili ya kazi maalumu ya kumshuhudia Kristu popote ulimwenguni kwa maneno na matendo yetu. Ni kweli kwamba mapadre na watawa wamewekwa wakfu kwa namna ya pekee lakini hili halifuti ukweli kuwa kila mbatizwa amewekwa wakfu kuwa shahidi wa Kristu. Kila mkristu popote alipo anapaswa kutambua kuwa yeye ni mteuliwa wa Kristu, ametengwa kwa ajili ya kumtambulisha Kristu kwa watu kwa utakatifu wake. Unapokuwa shuleni, sehemu ya kazi, nyumbani unapaswa kutambua kuwa wewe umechaguliwa na Kristu kuwa mfano wa maisha ya utakatifu, kinyume cha hapo unakufuru kwa kutenda uovu.

Silaha ya kumshinda mwovu hapa duniani ni kwa wakristu kuwa na umoja. Ni kwa bahati mbaya sana kati ya vitu ambavyo Kristu aliliombea kanisa lake umoja wa wakristu umepata misukosuko mingi. Wakristu wanapaswa kuwa na roho moja na moyo mmoja katika Kristu. Wapo watu katika ulimwengu huu ambao wanatumia silaha ya utengano kwa wakristu ili kujinufaisha katika mambo yao. Tumeona mara kadhaa wanasiasa wanavyovuruga kanisa ili likose msimamo mmoja katika kutetea maadili mema na hivyo wapate nafasi ya kukanyaga haki za watu kwa manufaa yao binafsi.

Wakristu tuna uhakika wa ulinzi wa Kristu dhidi ya mwovu tukiwa ulimwenguni. Yesu anatulinda kwa kweli ili tusiingie katika mtego wa shetani wa kutenda dhambi. Ulinzi huu tutaupata ikiwa tutakuwa tayari kuutafuta. Mara kadhaa kumekuwa na maswali inakuwaje watu wasio na hatia wanateseka na kufa kutokana na makosa ya watu wengine ikiwa Kristu anatuombea kwa Baba ili tulindwe na huyo mwovu. Si rahisi sana kusema kwa uhakika kwa nini haya yanatokea kwa sababu mateso bado ni fumbo kwetu. Lakini sisi wakristu daima tunaalikwa kumuangalia Kristu kiongozi wetu ambaye aliishi kila kitu sawa na sisi isipokuwa hakutenda dhambi, na bado akafa kifo cha aibu msalabani. Ufufuko wake umedhihirisha kuwa mateso ya mwili kwa mkristu si kitu ikiwa ameishi akiwa anamwamini Kristu. Hivyo pale inapotokea watu wasio na hatia wanateswa  na kufa na wakati mwingine kwa sababu ya imani yao, hatupaswi kumlaani Mungu kwa kudhani kuwa Mungu hayupo au hatupendi.

Somo la kwanza latutafakarisha juu ya wajibu wetu wa Kikristu. Katika kumchagua mtu atakayekuwa mbadala wa Yuda Iskariote wakristu wakwanza  waliongozwa na neno hili kuwa anapaswa awe shahidi wa ufufuko wa Kristu. katika somo hilo tunaelezwa jinsi ambavyo kanisa letu lenye watu zaidi ya bilioni leo hii lilikuwa na watu 120 tu wakati Matiya anachaguliwa kuwa mbadala wa Yuda. Inaonesha jinsi gani wakristu wa kwanza walifanya kazi kubwa ya kushuhudia ufufuko wa Kristu kiasi cha mimi na wewe leo kuitwa wakristu na huo ndio wajibu wetu mkuu kama wakristu.

Uhusiano wetu na Kristu umejengwa katika msingi wa upendo, hivyo ndivyo anavyotuambia Yohane katika somo la pili. Mungu ni upendo, kwa upendo wake ametuumba, ametukomboa, anaendelea kututegemeza na atatupa tuzo ya urithi wa mbingu milele. Kila tunapopendana tunakaa ndani ya Mungu, tunamualika Mungu kati yetu na Mungu anakaa ndani yetu. Upendo wa Mungu unajidhihirisha katika unyenyekevu. Ni rahisi sana mtu kuonesha unyenyekevu kwa mtu aliye mkubwa wake, kiumri ama kicheo au yule aliye na vipaji vingi kumzidi. Hebu fikiri ilivyo ngumu kwa mtu kujinyenyekesha kwa mdogo wake kiumri ama kicheo au kwa mtu aliyemzidi katika elimu ama vipaji na karama mbalimbali. Hivi ndivyo Mungu alivyotupenda, yeye aliyekuwa Mungu akatwaa hali ya utumwa ili atutumikie sisi viumbe vyake


Ikiwa kila mkristu ataona kuwa maisha ya hapa duniani ni maandalizi tu ya maisha mazuri na yenye raha mbinguni, itakuwa ni motisha tosha ya kupambana siku hadi siku  ili kufikia maisha hayo. Tuombe kwa Mungu ili daima tutafute kuwa mashuhuda wake kwa maneno na matendo yetu ili kufikia ukamilifu anaoutegemea kwetu.

Monday, 4 May 2015

DOMINIKA YA SITA YA PASAKA, MWAKA B. MAY 10, 2015

I.                    Mdo. 10:25-26, 34-35, 44-48, II. IYoh 4:7-10, Inj. Yn 15:9-17

Tunapokwenda kusali misa leo katika dominika ya sita ya pasaka  tujitahidi kadiri inavyowezekana kuruhusu Kristu mfufuka azidi kuijaza mioyo yetu kwa furaha kuu ya kipasaka. Furaha ambayo inatokana na sisi kuwekwa huru na dhambi na hivyo itupe hamu ya kuishi ufufuko huo kwa matendo ili tuzidi kuipata zaidi na zaidi katika maisha yetu ya hapa duniani na baadae tukaipate kwa ukamilifu huko Mbinguni.

Katika somo la injili tunaelezwa kuwa Yesu ametupa upendeleo mkubwa sana wa kutufanya sisi kuwa rafiki zake. Ni desturi ya mahali pengi duniani kwa baadhi ya watu wachache kupata bahati ya kuwa marafiki wa viongozi katika ngazi mbambali ikiwemo ya ufalme au uraisi. Desturi hii ilikuwepo pia katika dola ya Kirumi. Mfalme alikuwa na kikundi cha watu kadhaa ambao aliwaita ni marafiki zake na kwa kweli walikuwa marafiki zake. Marafiki hawa waliweza kumuona mfalme wakati wowote ule mara nyingine bila hata kupitia kwa wasaidizi wake kwa kutoa taarifa mapema. Mfalme mara kadhaa aliongea kwanza nao kabla ya kuongea na wasaidizi wake au raia kwa ujumla. Walifahamu siri binafsi za mfalme na daima hawakuwa tayari kumuangusha mfalme wala kumuudhi, mfalme anapotoa agizo fulani hawa ndio watakuwa wa kwanza kulitekeleza na kulitetea mbele ya raia wengine. Kwa ujulma walikuwa na uhusiano wa ndani na wa karibu na mflame kupita hata wasaidizi wa karibu wa mfalme.

Yesu aliye mfalme wetu anatuita sisi rafiki ili tuwe na uhusiano wa karibu naye kama wa wale marafiki wa mfalme wa Kirumi. Sisi si watumwa tena kwa sababu mtumwa hastahili kumsogelea bwana wake bali sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu tuna ruhusa ya kumsogelea na kumuendea  Yesu wakati wote kupitia sakramenti zake. Sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu Yesu ametushirikisha siri za Mbinguni kama ambavyo marafiki wa mfalme wa Kirumi walivyojua siri binafsi za mfalme wao. sisi ni marafiki wa Yesu kwa sababu mara kwa mara tunazungumza naye iwe wakati wa raha na shida kupitia sala za jumuiya na sala binafsi. Sisi ni marafiki wa Yesu kwa sababu hatutaki kumuangusha Yesu na ndio maana sisi kama walivyo marafiki wa mfalme wa Kirumi, tutakuwa wa kwanza kutii amri ya mfalme wetu.

Mfalme wetu Yesu anataka sisi tuishi upendo unaodai kujitoa sadaka kwa ajili Mungu na jirani  kwa sababu yeye amefanya hivyo kwa ajili yetu. Marafiki wa mflame wako tayari kutii amri ya mfalme kwa matendo na kuitetea kwa watu. Yesu anasema huu ndio upendo unaowatofautisha marafiki wa Yesu na wasio marafiki wake. Upendo wa kujitoa nafsi hata ikitubidi kufa  kwa ajili ya wenzetu. Ningependa hapa tutafakari jambo ambalo ni changamoto sana katika jamii yetu sasa linalohusu uhuru wa kuvaa. Uhuru ni jambo la thamani sana na linalompa hadhi mwanadamu na kila mwanadamu anatamani autumie uhuru wake kikamilifu. Kila mtu anao uhuru wa kuvaa nguo yeyote anayoipenda, lakini inapotokea nguo hiyo inasababisha wengine watende dhambi ya uzinifu si busara sana kwa rafiki wa mfalme Yesu  kusema hayo ni matatizo yao watajijua na Mungu wao. Kujitoa sadaka uhuru wako kwa ajili ya kulinda dhamiri dhaifu za wengine ni upendo unaomtofautisha rafiki wa  Yesu na asiye rafiki wa Yesu.

Mtume yohane anaendeleza wazo la upendo katika somo la pili katika waraka wake. Hapa Yohane anaonesha ukubwa, thamani na umuhimu wa fadhila hii ya Upendo. Ni fadhila ya Ki-Mungu, inatoka kwa Mungu na Mungu ndio upendo wenyewe. Hivyo kama tunapenda ni kwasababu Mungu ametuwezesha kupenda na ametuonesha mfano wa kupenda kwa kutupenda sisi kwanza. Mtu anayependa anamjua Mungu kwa sababu yeye ndiye upendo wenyewe na anayemjua Mungu anapenda kwa sababu ni katika kupenda tunamuona Mungu. Mtu anayependa anakuwa karibu zaidi na Mungu.

Katika somo la kwanza Petro akiongozwa na Roho wa Mungu anasema kuwa masharti ya kuwa mkrisu yaani  kuwa rafiki wa Kristu ni kusadiki na kupokea ubatizo. Kulikuwa na mgogoro katika kanisa la mwanzo kuhusu ikiwa ni lazima kwa mpagani kutahiriwa kwanza kabla hajabatizwa na kuwa mkristu. Wayahudi waliokuwa wakristu walishikilia msimamo kuwa ni lazima wapagani wasiokuwa wayahudi wakatahiriwa kwanza kama sharti la kuwa myahudi kwanza kabla ya kubatizwa. Petro anatatua mgogoro huyo kwa kuweka msimamo unaodhihirisha jinsi gani Mungu asivyo na upendeleo. Mungu yuko tayari kumkubali yeyote yule kwa sharti moja tu la uchaji na kutenda haki. Wazo la injili ya leo linaingia hapo kwamba sisi ni rafiki wa Kristu ikiwa tutazishika amri zake. Lakini pia wazo la upendo wa Kikristu ambao Kristu anataka sisi tulio rafiki zake tuuishi, upendo usio kuwa na ubaguzi wala usiowawekea watu masharti magumu yasio na lazima katika kumuendea Mungu wao. Yapo makanisa leo hii wachungaji na maaskofu wao wanatoa baraka kulingana na kiasi cha pesa alichotoa mtu badala ya kuangalia moyo wa ukarimu wa mtu. Si lazima kwamba aliyetoa pesa nyingi ndiye ana imani na ukarimu zaidi ya yule aliyetoa kidogo.


Kuwa rafiki wa Yesu kunaleta furaha sana, na yeyote anayemtembelea rafiki yake anataka kupata furaha. Hebu fikiri rafiki yako amekuja kukutembela halafu muda wote sura imekunjamana haongei kitu na wala hajibu kitu unapomsemesha, utajisikiaje? Ni wazi huwezi kujisikia vizuri. Mara nyingi sisi tumekwenda kumtembela rafiki yetu Yesu tukiwa na sura zimekunjamana hatuna furaha. Hatuongei chochote na hata Yesu akitusemesha kupitia kinywa cha padri hatuitikii kabisa au tunaitikia kama tumelazimishwa. Unaweza kufikiri tena unakuwa na rafiki ambaye anakufuata wakati wa shida tu, na hapo utajisikiaje?  Je sisi hatufanyi hivyo kwa rafiki yetu Yesu? Je hatumdhalilishi rafiki yetu Yesu kwa kuwa wa kwanza kuvunja au kutofuata maagizo yake na kwenda mbali zaidi kuwahamasisha wengine wasitimize amri za Kristu?. Tusali na kujiibidiisha ili tuwe marafiki wema wa Kristu