I.
Mdo 2:1-11
II. 1 Kor 12:3b-7, 12-13 Inj. Yn
20:19-23
Siku ya hamsini ya kipindi
kitakatifu cha Pasaka inahitimishwa na Dominika ya Pentekoste, kanisa
linapokumbuka kazi ya Roho Mtakatifu kwa Mitume, mwanzo wa Kanisa na mwanzo wa
utume wake kwa lugha, watu na mataifa yote. Roho mtakatifu analitakasa kanisa,
analifariji katika mahangaiko yake ya hapa duniani na pia analiwezesha katika
utume wake kupitia vipaji, karama na huduma mbalimbali anazozimimina kwa
wanakanisa kadiri apendavyo
Katika injili leo Yohane
anatupatia simulizi la Yesu mfufuka akiwatokea mitume katika chumba na
anapowatokea anawaambia mambo kadhaa ambayo kwa kweli yanagusa pamoja na mambo
mengine utume wetu kama wana kanisa
Tunajifunza kuwa Kristu anahitaji
Kanisa katika kuendeleza kazi yake ya ukombozi aliyoianzisha. Baada ya kupaa
kwake mbinguni mitume wanapaswa kuwaongoza wanakanisa kwenda ulimwenguni pote
na kwa kila kizazi kushuhudia ufufuko wa Kristu ili ulimwengu mzima upate
wokovu. Twajua kuwa Kristu ndiye kichwa yaani Kiongozi wa Kanisa lakini
anahitaji miguu, mdomo na mikono ya kupeleka ujumbe wake kwa watu wote akiwa
ameketi kuume kwa Baba. Kanisa ndio miguu, mikono na mdomo wake. Kristu
anategemea kanisa lenye wanadamu wasio wakamilifu wanaopambana kuufikia wokovu
wao wenyewe kwanza halafu watu wengine. Kwa hiyo ni wazi kwamba kushuhudia
wanakanisa wakianguka katika udhaifu isiwe kigezo cha kukata tamaa na kulikimbia
kanisa kwa sababu Kristu mwenyewe amechagua Kanisa dhaifu lifanye kazi yake.
Katika kufanya kazi ya utume Kanisa
linamuhitaji sana Kristu. kwa sababu kanisa linafanya kazi ya utume hivyo
lazima kuwepo na yule aliyelituma, ujumbe wa kupeleka, nguvu na mamlaka ya
kupelekea ujumbe huo. Kristu ndiye anayelituma Kanisa, na analipa ujumbe wa
wokovu kwa watu wote na zaidi ya hayo analipatia nguvu na mamlaka ya kupeleka
ujumbe huo kupitia Roho Mtakatifu tunayempokea leo katika sherehe ya
Pentekoste. Katika udhaifu wake kanisa linahitaji kujishikamanisha na Kristu
daima ili liweze kufanikiwa maana Kristu mwenyewe anatuambia bila yeye hatuwezi
chochote.
Kama Baba alivyomtuma Mwana
ulimwenguni ndivyo Kristu anavyolituma Kanisa lake. Utume wa Kristu uliwezekana
na ulifanikiwa kwa sababu tu Kristu alikuwa mtii kwa yule aliyemtuma na pia
alimpenda sana. Kanisa linamwakilisha Kristu duniani hivyo daima linapaswa kuwa
mtii kwake ili lisije kupeleka ujumbe wake badala ya ujumbe wa Kristu. Upendo
ndio msingi wa utume wetu, yatupasa kuwa tayari kutolea maisha yetu kwa ajili
ya yule aliyetutuma
Kristu anatualika tupeleke ujumbe wa msamaha
wake kwa wadhambi wanaotubu. Anapowaeleza mitume wake juu ya mamlaka ya kufunga
na kufungua anawatuma waende ulimwenguni kote na kuwaeleza watu kuwa Kristu
alikuja duniani kuwasamehe watu makosa yao. Atakayekuwa tayari kutubu na kuomba
msamaha atasamehewa lakini yule anayekataa msamaha wake hatapokea msamaha huo.
Katika somo la pili mtume Paulo
anatueleza kuwa utume wa kanisa unawezekana kwa sababu Roho Mtakatifu anagawa
karama, vipaji na huduma mbalimbali kwa watu wake. Kupitia karama hizi
wanakanisa wanapeleka ujumbe wa Kristu kwa watu. Karama mbalimbali zinatolewa
kwa ajili ya manufaa ya Kanisa zima na wala si kwa ajili ya sifa na utukufu wa
wale waliojaliwa karama hizo
Somo la kwanza ni simulizi la
tukio la Pentekoste ambalo kwa kweli linaonesha kazi ya Roho Mtakatifu kwa
mitume, mwanzo wa Kanisa, mwanzo wa utume wa kanisa kwa lugha, watu na mataifa
yote. Ni muhimu kuelewa awali ya yote kwamba Roho Mtakatifu yupo na amekuwepo
daima akifanya kazi kati ya watu hata kabla ya tukio hili ya Pentekoste. Ingawaje
ni ukweli kwamba kuna kitu cha pekee kilitokea siku hiyo ya Pentekoste. Siku ya
Pentekoste Roho Mtakatifu aliwavuvia mitume na kuwapa zawadi na karama ya ajabu
ambayo hawakuwahi kuipata kabla. Uvuvio huu wa Roho Mtakatifu uliwafanya mitume
walihubiri neno la Mungu kwa namna ambayo kwa mara ya kwanza iligusa mioyo ya
watu na walielewa vizuri sana.
Wapo watu wanaosema kuwa mitume
walipata uwezo wa kunena kwa lugha kama ishara ya kuvuviwa na Roho Mtakatifu. Kunena
kwa lugha kunakozungumziwa na ule uwezo wa kutamka maneno ambayo hakuna mtu mwingine
anayeweza kuelewa, jambo ambalo lilikuwepo hata katika kanisa la mwanzo. Watu hawa
wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa hiyo ndio ishara ya muhimu na ya pekee ya
uwepo wa Roho Mtakatifu. Mtume Paulo ameeleza kwa kirefu juu ya kipawa cha kunena
kwa lugha katika (1Kor 14) lakini kwa ufupi anachoeleza ni kuwa kipaji chochote
anachotoa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya manufaa ya jumuiya, la kama mtu
amepewa kipaji na hakiwasaidiii wanajumuiya katika kuabudu kwao isipokuwa yule
aliyepewa basi asikitumie katikati ya wanajamii hasa katika sala. Zaidi ya hayo
hatuwezi kusema kuwa kiuongo kimoja katika mwili ndio chenye umuhimu kuliko
vingine kwa sababu ili mwili uitwe mwili unahitaji kuwa na viunguo vyote kamili
na ndio maana wasio na viungo fulani huitwa walemavu ingawaje hawajapoteza utu
wao. Haiwezekani kipaji kimoja tu ndio kikawa muhimu kuliko kingine katika
mwili wa fumbo wa Kristu yaani Kanisa.
Hivyo katika pentekoste si kwamba
mitume walipata hiyo karama ya kunena kwa lugha kwa sababu kila walichokiongea
watu walikielewa. Kipaji cha kunena kwa lugha kadiri ya Paulo ni kwa ajili ya
yule tu mwenye kipaji hicho na watu wengine hawawezi kumuelewa.
No comments:
Post a Comment