Kum
4:32-34, 39-40, Rum 8:14-17, Inj Mt 28:16-20
Leo ni sherehe ya Utatu
Mtakatifu. Kanisa linaadhimisha fumbo la Mungu mmoja katika nafsi tatu yaani
Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa kweli hili ni fumbo mama
kati ya mafumbo yote ya Kikristu kwasababu linamhusu Mungu mwenyewe. Kwa akili
ya kibinadamu tunaweza kwa kiasi fulani kufahamu juu ya uwepo wa Mungu, kwa
mfano, kila tunapotafakari juu ya maajabu ya uumbaji. Lakini ukweli kwamba Mungu huyu ana nafsi tatu tofauti zinazoshiriki
Umungu mmoja tunaweza kuufahamu tu ikiwa Mungu mwenyewe anaamua kutufunulia na
kwa fadhila ya imani. Neno la Mungu leo linatufunulia ukweli huu, tunahitaji
paji la imani ili kupokea na kuufahamu
ukweli huu.
Mungu wetu ni mmoja
mwenye nafsi tatu, hili ni fumbo kweli kwetu sisi wanadamu kwani kila
tunapojaribu kuelewa ni kwa namna gani hili linawezekana tunashindwa kwani
akili yetu ni finyu sana kumuelewa Mungu asiye na mipaka na wa milele. Tunapata
shida kuelewa kwasababu kwetu sisi nafsi ya mtu ni ya kipekee inafikiri na
kutenda katika upekee na hivyo kuwa na nafsi mbili na zaidi maana yake ni kuwa
na watu wawili na zaidi walio tofauti katika kufikiri na kutenda. Kila tunapojaribu
kuzitazama nafsi tatu za Mungu kwa namna yetu hii ya kibinadamu tunakwama kwani
ufunuo wa neno la Mungu unatueleza kuwa katika Mungu hakuna nafsi inayofikiri
na kutenda kipekee, Baba yu ndani ya Mwana na Mwana yu ndani ya Baba kadhalika
wote wako ndani ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu yu nadani ya Baba na Mwana.
Nafsi zote tatu za Mungu zinafikiri na kutenda katika umoja kamili wa Umungu.
Anachofikiri baba ndicho anachofikiri Roho Mtakatifu na Mwana pia. Hivyo nafsi tatu hazifanyi miungu watatu, bali
zote zi na asili ya Umungu ule ule, na hili ndilo fumbo lenyewe
Ufunuo wa ukweli huu wa
Utatu Mtakatifu watuonesha kuwa Mungu wetu yu hai, na zaidi ya hayo anatupenda sana. Mtume Paulo kwenye
somo la pili la leo anaonesha kuwa Mungu wetu anatupenda sana na hili
linaonekana pale anapoamua kutufanya sisi wana wake kupitia nafsi yake ya pili
yaani Kristu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ambaye Paulo anasema yeye ndiye
anayeshuhudia tukio hilo la sisi kufanyika wana. Roho Mtakatifu nafsi ya tatu anatuwezesha
sisi kumtambua nafsi ya kwanza ya Mungu kuwa ni Baba yetu. Anatufanya sisi kuwa
ndugu wa Kristu, warithi pamoja naye wa mateso na utukufu. Katika somo la
kwanza pia laonesha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kupitia matendo makuu ya
kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri.
Katika somo la injili,
mwinjili Matayo anaonesha umoja wa Umungu wa nafsi tatu. Kristu nafsi ya pili ya Mungu
ndiye aliyeweka sakramenti saba, na kwa namna ya pekee ubatizo, ambazo ni alama
wazi ya wokovu wetu kwa kifo chake msalabani.
Kristu anapowatuma wafuasi wake waende ulimwenguni kote na kuwafanya
mataifa yote kuwa wanafunzi wake anawaamuru wabatize kwa jina la Baba, Mwana na
Roho Mtakatifu. Hii maana yake ni kwamba katika kazi ya ukombozi ambayo Kristu,
nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeifanya, nafsi zote tatu zinashiriki katika
kazi hiyo kwa ukamilifu wake.
Sherehe hii ya Utatu
Mtakatifu inalenga kutukumbusha mambo makubwa mawili; moja ni kwamba kujua ukweli
huu kuhusu Mungu wetu anayeishi na kutupenda sana, kunatupa wajibu wa
kumrudishia sifa na shukrani kwa maneno na matendo yetu. Ingawaje sifa zetu
hazimzidishii Mungu chochote lakini
zatufaa kwa waokovu wetu. Tunamsifu Mungu kwa nafasi ya kwanza kwa sala na
ibada zetu. Wapo watu wanaodai kuwa hakuna ulazima wa kwenda kanisani kusali
dominika alimradi wanajitahidi kuepuka maovu na kutoa misaada. Hii si kweli
kabisa , kuna umuhimu na ulazima wa kumkiri Mungu kwa midomo yetu kupitia sala,
nyimbo na ibada, tendo hili linaelezea na kuimarisha imani na upendo wetu kwa Mungu na linatupa nguvu ya
kuishi vema amri ya mapendo. Katika ibada ya misa takatifu tunachota neema ya
kuishi kitakatifu.
Jambo la pili
tunalokumbushwa leo ni umoja. Katika Mungu kuna nafsi tatu tofauti lakini
zinatenda kwa umoja kamili wa Umungu. Tunapaswa kuwa na umoja kwanza wa sisi
wenyewe ndani yetu, umoja ambao unalenga kulinda hadhi yetu kama wakristu. Ikiwa
akili inayoelewa mambo, haina umoja na utashi unaoamua kulingana na mwangaza wa
akili daima nafsi ya mtu itakuwa katika fujo. Ikiwa dhamiri ya mtu haina umoja
na utashi wake pia mtu hukosa amani na daima atakuwa mtumwa. Kama hakuna umoja
kati ya utashi wa mtu na mwili wake matokeo yake pia ni vurugu ndani ya mtu. Kwa
mfano, ikiwa dhamiri ya mtu inamsukuma kuacha ulevi lakini utashi wake
unashindwa kuamua kadiri ya matakwa ya dhamiri yake njema, mtu huyu daima
atakosa amani kwani dhamiri yake itaendelea kumsuta kila mara kwa kuamua
kinyume na matakwa yake. Kama ndani ya
mtu kuna umoja daima kutakuwa na amani na matunda yake ni kwamba familia
zitakuwa na umoja, jumuiya, nchi na dunia kwa ujumla itakuwa na umoja.
Tusali daima kuomba
paji la Roho Mtakatifu la Ibada ili tuendelee kuusifu Utatu Mtakatifu daima na
zaidi ya hayo tuuishi umoja usiogawanyika unaopatikana katika Utatu Mtakatifu.
Blog imesinzia kidogo
ReplyDelete