I.
Mdo. 10:25-26, 34-35, 44-48, II. IYoh 4:7-10, Inj. Yn 15:9-17
Tunapokwenda kusali misa leo
katika dominika ya sita ya pasaka
tujitahidi kadiri inavyowezekana kuruhusu Kristu mfufuka azidi kuijaza
mioyo yetu kwa furaha kuu ya kipasaka. Furaha ambayo inatokana na sisi kuwekwa
huru na dhambi na hivyo itupe hamu ya kuishi ufufuko huo kwa matendo ili tuzidi
kuipata zaidi na zaidi katika maisha yetu ya hapa duniani na baadae tukaipate
kwa ukamilifu huko Mbinguni.
Katika somo la injili tunaelezwa
kuwa Yesu ametupa upendeleo mkubwa sana wa kutufanya sisi kuwa rafiki zake. Ni desturi
ya mahali pengi duniani kwa baadhi ya watu wachache kupata bahati ya kuwa
marafiki wa viongozi katika ngazi mbambali ikiwemo ya ufalme au uraisi. Desturi
hii ilikuwepo pia katika dola ya Kirumi. Mfalme alikuwa na kikundi cha watu
kadhaa ambao aliwaita ni marafiki zake na kwa kweli walikuwa marafiki zake. Marafiki
hawa waliweza kumuona mfalme wakati wowote ule mara nyingine bila hata kupitia
kwa wasaidizi wake kwa kutoa taarifa mapema. Mfalme mara kadhaa aliongea kwanza
nao kabla ya kuongea na wasaidizi wake au raia kwa ujumla. Walifahamu siri
binafsi za mfalme na daima hawakuwa tayari kumuangusha mfalme wala kumuudhi,
mfalme anapotoa agizo fulani hawa ndio watakuwa wa kwanza kulitekeleza na
kulitetea mbele ya raia wengine. Kwa ujulma walikuwa na uhusiano wa ndani na wa
karibu na mflame kupita hata wasaidizi wa karibu wa mfalme.
Yesu aliye mfalme wetu anatuita
sisi rafiki ili tuwe na uhusiano wa karibu naye kama wa wale marafiki wa mfalme
wa Kirumi. Sisi si watumwa tena kwa sababu mtumwa hastahili kumsogelea bwana
wake bali sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu tuna ruhusa ya kumsogelea na
kumuendea Yesu wakati wote kupitia
sakramenti zake. Sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu Yesu ametushirikisha siri za
Mbinguni kama ambavyo marafiki wa mfalme wa Kirumi walivyojua siri binafsi za
mfalme wao. sisi ni marafiki wa Yesu kwa sababu mara kwa mara tunazungumza naye
iwe wakati wa raha na shida kupitia sala za jumuiya na sala binafsi. Sisi ni
marafiki wa Yesu kwa sababu hatutaki kumuangusha Yesu na ndio maana sisi kama
walivyo marafiki wa mfalme wa Kirumi, tutakuwa wa kwanza kutii amri ya mfalme
wetu.
Mfalme wetu Yesu anataka sisi
tuishi upendo unaodai kujitoa sadaka kwa ajili Mungu na jirani kwa sababu yeye amefanya hivyo kwa ajili yetu.
Marafiki wa mflame wako tayari kutii amri ya mfalme kwa matendo na kuitetea kwa
watu. Yesu anasema huu ndio upendo unaowatofautisha marafiki wa Yesu na wasio
marafiki wake. Upendo wa kujitoa nafsi hata ikitubidi kufa kwa ajili ya wenzetu. Ningependa hapa
tutafakari jambo ambalo ni changamoto sana katika jamii yetu sasa linalohusu
uhuru wa kuvaa. Uhuru ni jambo la thamani sana na linalompa hadhi mwanadamu na
kila mwanadamu anatamani autumie uhuru wake kikamilifu. Kila mtu anao uhuru wa
kuvaa nguo yeyote anayoipenda, lakini inapotokea nguo hiyo inasababisha wengine
watende dhambi ya uzinifu si busara sana kwa rafiki wa mfalme Yesu kusema hayo ni matatizo yao watajijua na Mungu
wao. Kujitoa sadaka uhuru wako kwa ajili ya kulinda dhamiri dhaifu za wengine
ni upendo unaomtofautisha rafiki wa Yesu
na asiye rafiki wa Yesu.
Mtume yohane anaendeleza wazo la
upendo katika somo la pili katika waraka wake. Hapa Yohane anaonesha ukubwa,
thamani na umuhimu wa fadhila hii ya Upendo. Ni fadhila ya Ki-Mungu, inatoka
kwa Mungu na Mungu ndio upendo wenyewe. Hivyo kama tunapenda ni kwasababu Mungu
ametuwezesha kupenda na ametuonesha mfano wa kupenda kwa kutupenda sisi kwanza.
Mtu anayependa anamjua Mungu kwa sababu yeye ndiye upendo wenyewe na anayemjua
Mungu anapenda kwa sababu ni katika kupenda tunamuona Mungu. Mtu anayependa
anakuwa karibu zaidi na Mungu.
Katika somo la kwanza Petro
akiongozwa na Roho wa Mungu anasema kuwa masharti ya kuwa mkrisu yaani kuwa rafiki wa Kristu ni kusadiki na kupokea
ubatizo. Kulikuwa na mgogoro katika kanisa la mwanzo kuhusu ikiwa ni lazima kwa
mpagani kutahiriwa kwanza kabla hajabatizwa na kuwa mkristu. Wayahudi waliokuwa
wakristu walishikilia msimamo kuwa ni lazima wapagani wasiokuwa wayahudi
wakatahiriwa kwanza kama sharti la kuwa myahudi kwanza kabla ya kubatizwa.
Petro anatatua mgogoro huyo kwa kuweka msimamo unaodhihirisha jinsi gani Mungu
asivyo na upendeleo. Mungu yuko tayari kumkubali yeyote yule kwa sharti moja tu
la uchaji na kutenda haki. Wazo la injili ya leo linaingia hapo kwamba sisi ni
rafiki wa Kristu ikiwa tutazishika amri zake. Lakini pia wazo la upendo wa
Kikristu ambao Kristu anataka sisi tulio rafiki zake tuuishi, upendo usio kuwa
na ubaguzi wala usiowawekea watu masharti magumu yasio na lazima katika
kumuendea Mungu wao. Yapo makanisa leo hii wachungaji na maaskofu wao wanatoa baraka
kulingana na kiasi cha pesa alichotoa mtu badala ya kuangalia moyo wa ukarimu
wa mtu. Si lazima kwamba aliyetoa pesa nyingi ndiye ana imani na ukarimu zaidi
ya yule aliyetoa kidogo.
Kuwa rafiki wa Yesu kunaleta
furaha sana, na yeyote anayemtembelea rafiki yake anataka kupata furaha. Hebu fikiri
rafiki yako amekuja kukutembela halafu muda wote sura imekunjamana haongei kitu
na wala hajibu kitu unapomsemesha, utajisikiaje? Ni wazi huwezi kujisikia
vizuri. Mara nyingi sisi tumekwenda kumtembela rafiki yetu Yesu tukiwa na sura
zimekunjamana hatuna furaha. Hatuongei chochote na hata Yesu akitusemesha
kupitia kinywa cha padri hatuitikii kabisa au tunaitikia kama tumelazimishwa. Unaweza
kufikiri tena unakuwa na rafiki ambaye anakufuata wakati wa shida tu, na hapo
utajisikiaje? Je sisi hatufanyi hivyo kwa
rafiki yetu Yesu? Je hatumdhalilishi rafiki yetu Yesu kwa kuwa wa kwanza
kuvunja au kutofuata maagizo yake na kwenda mbali zaidi kuwahamasisha wengine
wasitimize amri za Kristu?. Tusali na kujiibidiisha ili tuwe marafiki wema wa
Kristu
No comments:
Post a Comment