Tuesday, 26 May 2015

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU, MAY 31, 2015

Kum 4:32-34, 39-40, Rum 8:14-17, Inj Mt 28:16-20

Leo ni sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kanisa linaadhimisha fumbo la Mungu mmoja katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa kweli hili ni fumbo mama kati ya mafumbo yote ya Kikristu kwasababu linamhusu Mungu mwenyewe. Kwa akili ya kibinadamu tunaweza kwa kiasi fulani kufahamu juu ya uwepo wa Mungu, kwa mfano, kila tunapotafakari juu ya maajabu ya uumbaji. Lakini ukweli  kwamba Mungu huyu ana nafsi tatu tofauti zinazoshiriki Umungu mmoja tunaweza kuufahamu tu ikiwa Mungu mwenyewe anaamua kutufunulia na kwa fadhila ya imani. Neno la Mungu leo linatufunulia ukweli huu, tunahitaji paji la imani ili kupokea na  kuufahamu ukweli huu.

Mungu wetu ni mmoja mwenye nafsi tatu, hili ni fumbo kweli kwetu sisi wanadamu kwani kila tunapojaribu kuelewa ni kwa namna gani hili linawezekana tunashindwa kwani akili yetu ni finyu sana kumuelewa Mungu asiye na mipaka na wa milele. Tunapata shida kuelewa kwasababu kwetu sisi nafsi ya mtu ni ya kipekee inafikiri na kutenda katika upekee na hivyo kuwa na nafsi mbili na zaidi maana yake ni kuwa na watu wawili na zaidi walio tofauti katika kufikiri na kutenda. Kila tunapojaribu kuzitazama nafsi tatu za Mungu kwa namna yetu hii ya kibinadamu tunakwama kwani ufunuo wa neno la Mungu unatueleza kuwa katika Mungu hakuna nafsi inayofikiri na kutenda kipekee, Baba yu ndani ya Mwana na Mwana yu ndani ya Baba kadhalika wote wako ndani ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu yu nadani ya Baba na Mwana. Nafsi zote tatu za Mungu zinafikiri na kutenda katika umoja kamili wa Umungu. Anachofikiri baba ndicho anachofikiri Roho Mtakatifu na Mwana pia.  Hivyo nafsi tatu hazifanyi miungu watatu, bali zote zi na asili ya Umungu ule ule, na hili ndilo fumbo lenyewe

Ufunuo wa ukweli huu wa Utatu Mtakatifu watuonesha kuwa Mungu wetu yu hai,  na zaidi ya hayo anatupenda sana. Mtume Paulo kwenye somo la pili la leo anaonesha kuwa Mungu wetu anatupenda sana na hili linaonekana pale anapoamua kutufanya sisi wana wake kupitia nafsi yake ya pili yaani Kristu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ambaye Paulo anasema yeye ndiye anayeshuhudia tukio hilo la sisi kufanyika wana. Roho Mtakatifu nafsi ya tatu anatuwezesha sisi kumtambua nafsi ya kwanza ya Mungu kuwa ni Baba yetu. Anatufanya sisi kuwa ndugu wa Kristu, warithi pamoja naye wa mateso na utukufu. Katika somo la kwanza pia laonesha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kupitia matendo makuu ya kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri.

Katika somo la injili, mwinjili Matayo anaonesha umoja wa Umungu  wa nafsi tatu. Kristu nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeweka sakramenti saba, na kwa namna ya pekee ubatizo, ambazo ni alama wazi ya wokovu wetu kwa kifo chake msalabani.  Kristu anapowatuma wafuasi wake waende ulimwenguni kote na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake anawaamuru wabatize kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii maana yake ni kwamba katika kazi ya ukombozi ambayo Kristu, nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeifanya, nafsi zote tatu zinashiriki katika kazi hiyo kwa ukamilifu wake.

Sherehe hii ya Utatu Mtakatifu inalenga kutukumbusha mambo makubwa mawili; moja ni kwamba kujua ukweli huu kuhusu Mungu wetu anayeishi na kutupenda sana, kunatupa wajibu wa kumrudishia sifa na shukrani kwa maneno na matendo yetu. Ingawaje sifa zetu hazimzidishii  Mungu chochote lakini zatufaa kwa waokovu wetu. Tunamsifu Mungu kwa nafasi ya kwanza kwa sala na ibada zetu. Wapo watu wanaodai kuwa hakuna ulazima wa kwenda kanisani kusali dominika alimradi wanajitahidi kuepuka maovu na kutoa misaada. Hii si kweli kabisa , kuna umuhimu na ulazima wa kumkiri Mungu kwa midomo yetu kupitia sala, nyimbo na ibada, tendo hili linaelezea na kuimarisha imani na  upendo wetu kwa Mungu na linatupa nguvu ya kuishi vema amri ya mapendo. Katika ibada ya misa takatifu tunachota neema ya kuishi kitakatifu.

Jambo la pili tunalokumbushwa leo ni umoja. Katika Mungu kuna nafsi tatu tofauti lakini zinatenda kwa umoja kamili wa Umungu. Tunapaswa kuwa na umoja kwanza wa sisi wenyewe ndani yetu, umoja ambao unalenga kulinda hadhi yetu kama wakristu. Ikiwa akili inayoelewa mambo, haina umoja na utashi unaoamua kulingana na mwangaza wa akili daima nafsi ya mtu itakuwa katika fujo. Ikiwa dhamiri ya mtu haina umoja na utashi wake pia mtu hukosa amani na daima atakuwa mtumwa. Kama hakuna umoja kati ya utashi wa mtu na mwili wake matokeo yake pia ni vurugu ndani ya mtu. Kwa mfano, ikiwa dhamiri ya mtu inamsukuma kuacha ulevi lakini utashi wake unashindwa kuamua kadiri ya matakwa ya dhamiri yake njema, mtu huyu daima atakosa amani kwani dhamiri yake itaendelea kumsuta kila mara kwa kuamua kinyume na  matakwa yake. Kama ndani ya mtu kuna umoja daima kutakuwa na amani na matunda yake ni kwamba familia zitakuwa na umoja, jumuiya, nchi na dunia kwa ujumla itakuwa na umoja.

Tusali daima kuomba paji la Roho Mtakatifu la Ibada ili tuendelee kuusifu Utatu Mtakatifu daima na zaidi ya hayo tuuishi umoja usiogawanyika unaopatikana katika Utatu Mtakatifu.



1 comment: