Monday, 27 April 2015

DOMINIKA YA TANO YA PASAKA, MWAKA B. MAY 3, 2015

I.                   Mdo 9:26-31, II. IYoh 3:18-24, Inj. Yn 15:1-8

Sisi tumefanywa kuwa watoto wa Mungu kwa ukombozi wa Kristu. Tumewekwa huru dhidi ya utumwa wa dhambi na hakika huu ndio uhuru wa kweli. Hatuwezi kuendelea kuwa wana wa Mungu, kuwa na uhuru huu wa kweli ikiwa tutatetereka katika imani, imani inayodai kujiunganisha maisha yetu na Kristu. Masomo ya leo yanatuelekeza katika kuishi fadhila zitakazoimarisha uhusiano wetu na Kristu

Yesu ni mzabibu wa kweli maana yake Yesu ndiye wokovu wetu wa kweli. Tawi lisilokaa ndani ya mzabibu haliwezi kuzaa na mkulima huliondoa, lakini lile likaalo ndani ya mzabibu huzaa na mkulima hulisafisha vizuri ili lizae sana. Sisi tu matawi ya Yesu aliye mzabibu wa kweli. Kama tukichagua kukaa ndani ya Yesu tutazaa matunda, la tusipokaa ndani yake tutanyauka, tutaondolewa na kutupwa motoni na kuteketea. Yeyote anayekaa ndani ya Yesu, Yesu hukaa ndani yake pia naye huzaa sana. Mkristu anayekataa kusikia sauti ya Yesu na kuenenda kadiri ya maelekezo ya ulimwengu atanyauka na kuteketea kiroho na kimwili jehanum. Pia yule mkristu anayemkiri Yesu kwa mdomo tu lakini kimatendo yuko mbali naye atanyauka na kuteketea jehanum. Wale ambao wanamfuata Yesu wakati wa raha tu lakini wanapopata misukosuko wanamkimbia watanyauka pia. Bila Kristu hatuwezi kitu. Mkristu atakuwa ndani ya Kristu daima kwa kusali mara kwa mara, kusoma na kutafakari neno la Mungu na kwa namna hii atamtukuza Mungu daima.

Mtume Yohane katika somo la pili anatufundisha kwamba kuwa mkristu maana yake ni kuwa na imani sahihi katika Kristu na kutenda  au kuishi kadiri ya imani hiyo sahihi. Imani yetu inapaswa kuwa katika jina la Yesu, yaani nafsi ya pili ya Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu, akaishi sawa nasi katika kila kitu lakini hakutenda dhambi. Alikufa kwa ajili yetu na akafufuka katika wafu li kutupa tumaini jipya na alikwenda kutuandalia makao ya milele mbinguni. Yesu huyu alitupa amri ya mapendo akatutaka tumuige yeye kama tunataka kufikia utukufu. Mtume Yohane anarudia wazo la Kristu katika injili kuwa yeyote anayezishika amri zake kwa maneno na matendo yake huyo anakaaa ndani yake na Kristu anakaa ndani ya mtu huyo. Mtume Yohane anasema tukiishi namna hii tutakuwa na amani ya roho kwani dhamiri zetu hazitatusuta. Yeyote anayeishi kwa ujanjaujanja, uwongo na unafiki moyo wake daima humsuta na kumhukumu na hawezi kuwa na uhuru na amani ya Mungu

Katika somo la kwanza Paulo baada ya kuongoka alianza kuhubiri habari ya Kristu mfufuko yule aliyekuwa anamtesa  kupitia wafuasi wake. Kwa sababu ya historia yake mbaya dhidi ya wakristu, waamini wa Yerusalem wanasita kumpokea anapojaribu kujiunga nao. Ni jambo la kawaida pengine kwa hicho walichokifanya wakristu hao, hata mimi na wewe leo hii tungeweza kuwa na wasiwsi kama wao. Wakati wakristu wengine wanahisi kuwa Paulo anakuja kuwapeleleza Barnaba anafanya kitu cha kijasiri cha kutanguliza mtazamo chanya kwa Paulo ili kumpa nafasi ya kuthibitisha uzuri wake.Barnaba pia anatufundisha kuwa tusiwahukumu watu kwa maisha yao ya zamani bali kwa jinsi wanavyoishi sasa. Walau tuamini kuwa kuna uwezekano wa wadhambi kuongoka kama ambavyo inaweza kututokea sisi katika maisha yetu. Wapo watu ambao wakishamchukulia mtu kuwa mbaya hiyo itadumu daima bila kuruhusu uwezekano wa kubadilika, hii ni mbaya kwa mkristu. Hivyo pamoja na tahadhari tunazochukua lakini tuweke uwezekano wa wema pia. Huu ndio upendo wa Kristu.


Si jambo rahisi kuishi fadhila hizo tulizoziona katika masomo ya leo. Utakatifu wa maisha unafikiwa kwa kufanya sadaka kubwa. Tunapaswa kupigana vita kubwa ya Kiroho na kuishinda. Ni  ajabu kuwa pamoja na kufahamu ukweli huu na  ya kwamba tunahitaji msaada wa Mungu katika jitihada zetu lakini tumekuwa wazito wa kutafuta msaada huo kwa njia ya sala na mafungo. Kijana yupo tayari kusali novena na kufunga chakula kwa siku kadhaa kwa ajili ya kuomba mchumba mwema, kufaulu mtihani au kupata kazi kitu ambacho ni kizuri, lakini hawezi kufanya hivyo kwa ajili kuomba neema ya kumsaidia asifanye tendo la ndoa kabla ya ndoa na mchumba wake. Daima atabaki na kusema tuu, aah ni udhaifu tu wa kibinadamu au ni shetani tu. Hakika tunahitaji kusali sana na kufunga ili tubaki tumeunganika Kristu daima.

Wednesday, 22 April 2015

DOMINIKA YA NNE YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 26, 2015

Somo I. Mdo 4:8-12, Somo II. 1Yn. 3:1-2, Injili Yn 10:11-18
Tunapoendelea kufurahia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu leo tunaalikwa kujitahidi kadiri inavyowezekana kwa kutegemea msaada wake Mwenyezi kubaki katika kundi la kondoo wa Kristu yaani kanisa lake. Yeye Kristu ni mchungaji mwema, daima anatupigania na kutulinda dhidi ya mbwamwitu wakali. Iwapo tutatoka katika kundi, na kutangatanga nje ya kundi, tutajiweka katika hatari ya kushambuliwa na mbwa mwitu wakali, lakini pia tunaweza kujikuta tumeangukia mikononi mwa wachungaji wanaofanya kazi kwa mshahara na hivyo kutojali sana usalama wetu.

Katika injili Yesu anasema kuwa yeye ni mchungaji mwema na kweli ndivyo alivyo. Ni mchumgaji mwema wa kondooo wake ambao ndio sisi wakristu. Ni mchungaji mwema kwa sababu yuko tayari kutoa uhai wake ili kutuokoa kutoka katika mikono ya mwbwa mwitu shetani anayetafuta kutumaliza. Anafanya kazi yake si kwa sababu anatafuta faida yake binafsi bali kutokana na upendo alionao. Anajua wazi kuwa kupoteza uhai wa kimwili kwa ajili ya kutulinda sisi si kitu kwake kwani ni njia ya kufikia utukufu, atausalimisha uhai huo katika ufufuko katika hali ya utukufu. Ni mchungaji mwema kwasababu anawajua kondoo wake na yuko tayari kuwatafuta kondoo wote waliopotea na kuwarudisha kundini.

Wakristu tulio kondoo wa Kristu tunatumwa kufanya kazi kati ya mbwa mwitu wakali, shetani na wafuasi wake wanaopinga kazi ya Kristu. Tuko katika hatari kubwa ya kiroho na kimwili. Shetani daima anatafuta nafasi ya kuangamiza uzima mpya tulioupokea katika ubatizo na katika sakramenti zingine hasa ekaristi na kitubio. Uzima unaotusadia kuepuka dhambi na kuendelea kumtumikia Mungu daima. Shetani pia anatafuta nafasi ya kuondoa uhai wetu wa kimwili ili kutoa vitisho kwa kondoo wengine ili watawanyike na  kumuacha nyuma mchungaji wao ha hivyo iwe rahisi kwake kuwakamata na kuwaangamiza. Neno la Mungu leo linalenga kutuondolea hofu dhidi ya Mbwa mwitu shetani. Tunaye mchungaji mwema ambaye yuko tayari kutoa uhai wake ili kulinda na kutetea uhai wetu wa kiroho tulioupokea kwa sakramenti. Lakini yupo tayari pia kutuondolea hofu dhidi ya kifo tunapofanya kazi ya kumtangaza. Kifo cha mwili si kitu kwetu ikiwa tuna uzima wa kiroho kwani ni mlango wa kufikia ukamilifu wa uzima huo wa kiroho mbinguni.

Katika somo la pili mtume Yohane anatueleza juu ya bahati tuliyo nayo ya kuwa wana wa Mungu. Kwa Kristu mchungaji mwema kuutoa uhai wake ametukumboa kutoka katika mikono ya shetani na kutufanya si watoto wa shetani tena bali wana wa Mungu. Uhusiano wetu umekuwa si tu wa Muumba na viumbe vyake bali Baba na wana wake. Ni uhusiano wa ndani uliojengwa katika misingi ya upendo. Mungu aliye Baba yetu yuko tayari kutupigania na kututetea dhidi ya muovu shetani ambaye kama alivyomuandama Kristu ataendelea kutuandama pia.  Tunafanywa kuwa wana wa Mungu kwa neema yake Baba kwetu lakini pia kwa jinsi tunavyopokea neema hiyo. Hakuna anayeweza kuwa mwana wa Mungu kama hajapokea mwaliko wa kuwa mwana kwa kuishi maisha ya nuru. hawa ndio kondoo ambabo Kristu asema kuwa walio wake anawajua nao wanamjua. Kufanyika wana wa Mungu ni mwanzo wa safari ya kuelekea kufanana na Mungu pale tutakapomuona uso kwa uso siku ya mwisho Kristu atakapokuja.

Katika somo la kwanza mitume wakiongozwa na Petro wanapata ujasiri wa kuendelea kumhubiri Kristu mfufuka mbali ya kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa wakubwa wa watu na wazee wa Israeli. Ujasiri huu unatokana na Imani yao kwa kristu aliyekwisha kuambia tayari kuwa yeye ni mchungaji mwema yuko tayari kuwapigania kondoo wake dhidi ya mwovu shetani anayepambana kuwanyima watu mbingu. Ufufuko wa kristu umewathibitishia ukweli huo sasa hawana hofu tana na kifo ambacho shetani hutumia ili kuwakatisha tamaa wana wa Mungu katika jitihada zao za kumhubiri Kristu.

Kristu mfufuka anatupigania daima katika maisha yetu. Pamoja na kwamba Kristu anatulinda dhidi ya hatari za kimwili pia, lakini hasa yuko tayari kutoa uhai wake ili tusipoteze uhai wa Ki-Mungu ndani ya roho zetu  yaani neema ya utakaso tunayoipata kwa kupokea sakramenti zake. Anapotulinda uhai wa kimwili anataka bado tuendelee kuishi duniani ili tuufanyie kazi uhai wa Ki-Mungu  ndani ya roho zetu. Vinginevyo magonjwa, mateso, mahangaiko na hata vifo vinavyotokea kwa wana wa Mungu havina madhara kwa uzima wa Ki-Mungu ndani ya roho zetu  ila badala yake vikipokelewa kwa imani ni njia ya kupata  uzima wa milele Mbinguni.


Monday, 13 April 2015

DOMINIKA YA TATU YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 19, 2015

Somo I. Mdo 3:13-15, 17-19a, Somo II. 1Yn 2:1-5a, Injili. Lk 24:35-48
      
Kristu mfufuka analeta habari njema ya ondoleo la dhambi. Neno la Mungu laendelea kutusisitiza kuwa ufufuko wa Kristu ni ushindi dhidi ya dhambi na hivi namna sahihi ya kuupokea na kuuishi ufufuko huo ni kutafuta nafasi ya mara kwa mara ya kujipatanisha na Mungu wetu kila tunapoanguka dhambini na hasa dhambi za mauti.

Katika injili leo Kristu anawatokea mitume katika chumba na akiwa huko anakula chakula pamoja nao baada ya kuwaonesha makovu ya mikono yake na miguu yake. Yesu anayafanya haya ili kuthibitisha kuwa katika ufufuko wake yeye si  roho tupu wala si mzuka bali ni Mungu kweli na mtu kweli ambaye mwili wake wa kibinadamu  haukuhairibiwa wala kupotea katika kifo bali umegeuzwa na kuwa katika hali ya utukufu. Kwa kuonesha makovu ya miguu na mikono yake Kristu analenga pia kuonesha kuwa ufufuko wake umekuja baada ya kuvumilia mateso makali ya msalaba kwa ajili ya wokovu wetu. Hivi ndivyo tutakavyokuwa siku ya mwisho atakakapokuja. Sisi sote tunatumwa kuwahubiria watu kuwa sasa tumepata ondoleo la dhambi kwa ufufuko wa Kristu.

Petro katika somo la kwanza anawatangazia watu habari ya toba. Anawaeleza Wayahudi kuwa, pamoja na kwamba walimkana Yesu mbele ya Pilato aliyetaka kumfungulia Yesu lakini wao wakataka mhalifu ndiye afunguliwe yaani Baraba lakini Yesu asiye na hatia ndiye auawe, Kristu mfufuka anawasamehe dhambi yao kwa kuwa hawakujua watendalo. Anawaalika watubu warejee ili dhambi yao ifutwe kwasababu sasa wamejua maana ya mambo yote yaliyotokea kama yalivyoaguliwa na manabii tangu zamani. Wayahudi hawakujua watendalo lakini sasa wamejua ni heri kwao lakini wanawajibika sasa kuishi toba vinginevyo adhabu inawangoja. Yeyote anayeshupaa katika ouvu hata baada ya kuoneshwa uovu wake na kuonywa ataangamia.

Katika somo la pili mtume Yohane kawenye barua yake anawaasa wakristu wote juu ya kuepuka dhambi  na daima wawe wepesi wa kuungama pale wanapoanguka. Yohane amekwishatueleza kwenye sura ya kwanza ya barua hii kwamba ni uongo kwa mtu kusema hana dhambi na kweli haimo ndani yake. Mtume Yohane anaona hatari kubwa ya watu kubweteka kutokana na maeno haya wasione haja tena wala wasipate  msukumo wa kujibidiisha katika kuepa dhambi. Yohane pia kwenye sura hiyo ya kwanza anasisitiza kuwa tukiziungama dhambi zetu yeye (Kristu) ni mwaminifu atatusamehe dhambi. Kuna hatari pia watu wakaitumia vibaya huruma hii na wasione haja ya kuungama wakiamini kuwa huruma itakuja tu. Katika somo la leo Yohane anaweka msisitizo juu ya kuepuka dhambi na umuhimu wa kuziungama dhambi zetu. Kumjua Mungu maana yake ni kushika amri zake.


Kuepa dhambi ni vita kubwa sana kwani shetani hapendi kabisa kuona kuwa tunaongoka. Vita hii inahitaji utayari wetu, ujasiri na jitihada zetu tukipata nguvu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Lazima tutambue kuwa hakuna njia nyingine zaidi ya kujipatanisha na Mungu wetu ikiwa tunataka kufurahia matunda ya utukufu wa ufufuko.

Friday, 10 April 2015

DOMINIKA YA PILI YA PASAKA MWAKA B. APRIL 12, 2015

Somo I. Mdo 4:32-35, Somo II. IYn 5:1-6, Injili Yn 20:19-31
Fadhila ya imani ni kushawishika kwa moyo na kweli za KiMungu bila kutegemea tu ushahidi wa  milango yetu ya fahamu. Ufufuko wa Yesu ni ushindi dhidi ya kifo cha mwili na cha roho. Ushindi huu unatuingiza katika maisha mapya ya furaha milele, maisha yasioyoonja taabu ya aina yeyote ile milele yote. Furaha hii ya milele tutaipata kikamilifu mara ya baada ya kumaliza maisha yetu ya hapa duniani. Furaha hii inapita furaha zote za ulimwengu huu. Pamoja na kwamba hatujawahi kuipata furaha hiyo lakini tuamimi kwamba ipo na tutaipata.

Imani ya Tomaso kwa Yesu Mfufuka  kadiri ya  injili ya leo inategemea tu ushahidi wa milango ya fahamu. Baada tu ya kumuona Tomaso anamkiri kuwa Bwana wake na Mungu wake na kuanzia hapo anapata tamanio la kuungannika na Kristu huyu mfufuka na anaishi kadiri ya tamanio hilo hadi kufa shahidi. Hatuoni kwamba Kristu amestaajabishwa sana na imani ya Tomaso baada ya ungamo lake. Badala yake Kristu anawabariki wale wote wanaotamani kuunganika na Kristu kwa kusikia tu habari zake kutoka kwa watu wengine na sauti ya dhamiri zao bila ya kumuona wala kugusa madonda yake. Kristu ni kama vile anamwambia Tomaso ikiwa kila mtu atakayefuata baada ya yeye kwenda mbinguni akahitaji kumuona na kugusa madonda yake  ili amwamini hata baada ya kuhubiriwa, hakutakuwa na waaamini kwani hawatapata nafasi ya kumuona na kumgusa Kristu.

Katika somo la kwanza, Wakristu wa kanisa la kwanza walishawishiwa juu ya  ufufuko wa Kristu kwa mahubiri ya mitume peke yake bila kuhitaji kumuona wala kumgusa Kristu. Ufufuo wa Kristu ulibadilisha mtazamo wao. Uliwafanya  waamini kuwa maisha ya Mbinguni yana raha zaidi kuliko raha za dunia hii zinazotokana na mali ingawaje hawajawahi kuishi mbinguni. Tamanio hili la maisha ya raha ya Mbinugni liliwafanya waone kuwa si tatizo kwao kufanya kila kitu shirika, kila mtu kutoa mali zake kwa ajili ya maihitaji ya jumuiya.

Neno la Mungu katika somo la pili linatueleza kuwa imani yetu kwa kristu, Mungu kweli na mtu kweli, inatufanya tuushinde ulimwnegu. Kristu aliyekubali kuwa mtu alionja upinzani mkali kutoka ulimwengu huu, nguvu kama vile mateso, uchungu, umasikini, ubinafsi, mali,  zinazotaka ufalme wa Mungu usienee duniani. Yesu mtu kweli alishinda vita dhidi ya nguvu zote hizi pinzani na daima alikuwa mtii kwa mapenzi ya Mungu. Yeyote anayemwamini Kristu Mungu kweli na mtu kweli, aliyeshinda upinzani wote huu katika ubinadamu wake daima atauushinda ulimwengu katika nguvu zake zote pinzani dhiidi ya mapenzi ya Mungu.


Binadamu kwa hulka yetu tunahitaji ishara ili tuamini jambo na ndio maana mara nyingi tuko tayari kusoma kwa bidii sana kwa sababu tunaamini kuwa mafanikio yetu kimaisha yanategemea elimu kubwa. Imani hii tumeipata kwa sababu tumemuona baba, mama, kaka dada au rafiki aliyefanikiwa katika masomo. Linapokuja swala la kufanya juhudi kubwa kuachana na vilema vyetu vya dhambi vinavyotusumbua ili tupate maisha ya raha mbinguni hadithi n itofauti na sababu kubwa ni kwamba kwa uhakika hatuna mfano tulioona wa mtu aliyefanya hivyo na sasa anapata raha mbinungi. Tumuombe Mungu atupe paji la imani tuweze kuamwamini Kristu pasipo kumgusa wala kumuona

Saturday, 4 April 2015

DOMINIKA YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 5, 2015

Somo I. Mdo 10:34, 37-43, Somo II.  IKor. 5:6-8, Injili. Mk 16:1-7

Leo kanisa linaadhimisha fumbo la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu.  Masomo ya leo yaeleza kuwa ufufuko wa Kristu ni ushindi na  ya kwamba sisi tunatumwa kuwa mashahidi wa ushindi huo kwa maneno na matendo yetu. Ufufuko wa Kristu unaleta maisha mapya, maisha katika Kristu, maisha ya milele  ambayo mwanzo wake ni hapa duniani na ukamilifu wake ni mbinguni. Wale wanawake watatu waliokwenda kaburini kadiri ya injili ya leo walikuta kaburi li wazi na tupu, halina mwili. Lakini pale ulipolazwa mwili waliona vitambaa alivyofungwa Yesu vimelala. Yesu amefufuka maana yake uzima wake wa kibinadamu wa kimwili kupitia kifo chake umegeuzwa na kuwa uzima mpya wa umilele, uzima usiokuwa na mipaka ya muda na mahali  uzima usiokuwa na mahangaiko tena na ndio maana sanda na vitambaa vingine  alivyofungwa wakati wa kuzikwa vilibaki kaburini Yesu alipofufuka. Hivyo ufufuko wa Yesu maana yake ni kupata maisha mapya ya umilele katika mwili mpya wa utukufu. Sisi sote baada ya kumaliza maisha ya hapa duniani tukiwa wenye imani tutafufuliwa na kuwa kama Yesu na kuingia kwenye furaha ya milele na miili yetu ya utukufu.

Petro anahubiri juu ya Kristu mfufuka katika somo la kwanza. Petro anatoa ushuhuda kuwa ufufuko ni ushindi dhidi ya mateso na kifo cha mwili. Wayahudi walimwua lakini Mungu alimfufua siku ya tatu. Si tu ushindi dhidi ya kifo cha mwili lakini Petro anasema kuwa ufufuko huu ni ushindi dhidi ya kifo cha roho yaani dhambi na ndio maana anamalizi kwa kusema kuwa kila amwaminiye atapokea ondoleo la dhambi, maneno yale ambayo Kristu alimwambia Martha kuwa kila amwaminie ajapokufa atakuwa anaishi(Yn 11:25). Petro anasema kuwa Kristu aliwaamuru wawe mashuhuda wa habari hii njema ya ufufuko kwa maneno na maisha yao. Lazima kila mkristu aushuhudie ufufuko wa Kristu kwa kuhubiri na kuishi vema. Unapozidi kushupaa katika dhambi bila kutafuta nafasi ya kufufuliwa na Kristu wewe huamini  kwamba Kristu alifufuka.

Katika somo la pili mtume Paulo anatuasa kuwa maisha ya ufufuko yanadai kuachana na chachu ya kale yaani dhambi na kuwa donge jipya yaani mioyo mipya. Sisi  tuliofufuka pamoja na Kristu hatupaswi tena kuridhika na dhambi. Paulo anaongea haya katika mazingira ambapo katika kanisa la Korintho kulikuwa na maovu makubwa, uasherati ulizidi kiasi cha mtu kutembea au kulala na mke wa baba yake yaani mama yake wa kambo. Kilichomkasirisha Paulo ni kwamba kama jumuiya ya waamini walilifumbia macho jambo hili, wakaridhika na maisha yaliendelea kama kawaida. Paulo anawaambia wasikubali kuwa karibu na dhambi wakaridhika kwani dhambi ni kama chachu ambayo inasambaa taratibu mpaka ngano yote inachachuka. Watu taratibu wataanza kuiga mfano baya wa mtu huyu wakiona kuwa ni kawaida. Tunapaswa tushtuke, tusikitike tuone uchungu kila tunapoona matendo maovu yakifanywa na watu wengine au na sisi na tuchukue hatua. Tuna uhakika kwamba mapamabano yetu dhidi ya dambi yatafanikiwa kwasababu tunaye Kristu aliyeshinda dhambi kwa ufufuko wake.

Katika somo la injili, mwinjili Marko anatueleza habari ya ufufuko wa Kristu. Marko pekee kati ya wainjili wote anasimulia kuwa yule mjumbe wa Mungu aliyewaambia wale wanawake habari ya ufufuko alitamka kwao kuwa waende  wekawaambia wafuasi na Petro kwamba Kirstu mfufuka amewatangulia Galilaya.   Marko anaweka msisitizo si tu kwamba wakawaambie wafuasi lakini na Petro. Kwa maneno haya Marko anataka kuonesha kuwa ufufuko wa Yesu umeshinda dhambi ya Petro ya kumkana Bwana wake mara tatu. Petro kwa sababu alimwamini na kumpenda Yesu hata alipokufa katika dhambi ya kumkana Yesu anaendelea kuishi. Petro anaishi kwa sababu hakuridhika na kumkana Yesu, tendo lile lilimpa uchungu, masikitiko na mahangaiko ya moyo na hivyo akatafuta nafasi ya kuamka na kuanza tena na kwa sababu hiyo Kristo alimfufua.

Ufufuko wa Kristu unapaswa kutupatia mtazamo mpya wa maisha yetu ya hapa duniani. Tunapaswa sasa kuyaona maisha ya hapa duniani kama maandalizi ya maisha ya milele. Tukiyatazama mambo yote ya ulimwengu huu kama msaada wa kutufikisha kwa Mungu hatutakuwa na hofu tena, hofu ya mambo ambayo dunia inayaona kuwa ndio kila kitu. Hatutakuwa na hofu ya kifo tena kwasababu ni mlango wa maisha ya umilele. Tutakuwa watu wa kutoa zaidi kuliko kupokea, watu wa kutumikia zaidi kuliko kutumikie. Hatuna hofu ya kupoteza wala kuwa masikini kwa kutoa, hofu ya kudhalilishwa kwa kutumikia, hofu ya kuchekwa kwa kutunza ubikira mpka siku ya ndoa takatifu.


Thursday, 2 April 2015

IJUMAA KUU YA MATESO YA BWANA. APRIL 3, 2015

Somo I. Isa 52:13-53:12, Somo II. Ebr 4:14-16; 5:7-9, Injili. Yn 18:1-19:42
Kanisa zima linaadhimisha leo mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristu msalabani. Ni siku ya kwanza katika siku kuu tatu za pasaka ambayo tumeianza jana kwa adhimisho la karamu ya mwisho. Leo historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu inasomwa kadiri ya mwinjili Yohane. Tafakari yetu leo itatazama ushiriki wa wahusika  mbalimbali katika historia hiyo ili wahusika hawa wawe kama kioo cha kujitazamia uhusiano wetu na Kristu pamoja na wenzetu pia.

Mtume Petro ni mhusika anayemuendea Yesu katika ukweli na wala hakuwa na unafiki. Petro alimpenda sana Yesu na daima aliishi kama alivyo, alinena na kutenda kile alichoamini kuwa kinafaa machoni  kwa Yesu, pale alipotenda mazuri Yesu alimpongeza na pale alipotenda mabaya Yesu alimkemea ili ajirudi. Maisha ya Petro yamekuwa ni ya kuanguka na kuinuka.  Maaskari wanapokuja kumkamata Yesu, Petro anamkata sikio mmojawapo wa wale waliokuja kumkamata kwa upanga. Yesu anamsihi Petro arudishe upanga wake ili mpango wa Mungu utimie. Baada ya Yesu kukamatwa wanafunzi wengine wanakimbia lakini Petro anamfuata Yesu mpaka ndani mbele ya Kuhani mkuu. Baadae Petro aliyeonesha ushujaa mkubwa katika kumpigania Bwana wake aliyempenda anaanguka kwa kumkana mara tatu. Ni kweli Petro ameanguka lakini ameanguka katika mazingira ya kumfuata Yesu Kristu na ndio maana alipogundua amekosa aliamka tena kwa kutubu. Yesu anamsamehe Petro na kumuweka kuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa lake kwa sababu moyo wa Petro daima ulimtafuta Yesu, umeanguka katika safari ya kumtafuta Yesu, Petro ameamka ili aendelee mbele.

Annas ni mhusika fisadi aliyedhamiria kumuangamiza Yesu hata ikibidi kwa kukiuka misingi ya haki kwasababu alimpinga katika ufisadi wake. Annas alikuwa ni mmiliki vibanda au maduka yaliyokuwa yanauza wanyama na vitu mbalimbali kwa ajili ya kutolea sadaka hekaluni  na biashara hiii ilifanyika ndani ya hekalu. Wauzaji wa vitu hivi kwa ajili ya kutolea sadaka waliwauzia watu kwa bei kubwa sana kuliko kama wangenunua nje ya hekalu kiasi kwamba maskini walishindwa kumtolea Mungu wao sadaka. Watu walilazimika kununua vitu hivi ndani ya hekalu kwa sababu vitu vilivyonunuliwa nje daima vilichunguzwa ubora wake kama vinafaa na mara nyingi kama si mara zote vilikataliwa. Hivyo Annas aliye wahi kuwa kuhani mkuu huko nyuma, kati ya mwaka 6 B.K n 15 B.K , alijipatia faida hekaluni kwa kuwanyonya maskini. Kadiri ya mwinjili Yohane,( Yn 2:15-25), Yesu alikasirishwa sana na vitendo hivi vilivyonajisi hekalu na kuamua kuwatimua wafanya biashara hekaluni. Annas,  akiwa bado ana ushawishi katika ofisi ya kuhani mkuu ambayo kwa wakati huu ilikuwa inakaliwa na shemeji yake Kayafa na pia kwa watawala, anaamuru Yesu aletwe kwake kwanza kabla ya kwenda kwa Pilato. Wayahudi walikuwa na sheria kuwa mtu hawezi kuhukumiwa kwa ushahidi wake mwenyewe hivyo hapaswi kuulizwa maswali ili atoe ushuhuda wake mwenyewe, lakini Annas anakiuka misingi hiyo kwa kumuuliza Yesu swali na Yesu anamkumbusha juu ya utaratibu kwamba awaulize watu , wao ndio watatoa ushuhuda juu yake. Yesu akahukumiwa kabla ya kesi kusikilizwa maana watu hawakuulizwa watoe ushuhuda.

Wayahudi ni wahusika wenye chuki kubwa sana dhidi ya Yesu kiasi kwamba inawaziba, macho, akili na mioyo yao wasione, wasiwaze wala kuamua sawaswa. Wayahudi tangu mwanzo walipinga vikali kulipa kodi kwa Kaisari na sababu yao kubwa ilikuwa kaisari ni mpagani, Mungu pekee aliye mfalme wao ndiye anastahili kupokea kodi yao. Mafasarisayo wanapomwendea Yesu na kumuuliza juuu ya uhalali wa kulipa kodi kwa kaisari(Lk 20:22), wanataka kumtega kuona kama na yeye anawaunga mkono ama la ili kupima Umasiya wake. Pia wayahudi tangu mwanzo walijitambua kama taifa linalooongozwa na mfalme mmoja tu naye ni Mungu (1Sam 12:12), lakini leo Pilato anapowauliza nimsulibishe mfalme wenu wanajbu kwa nguvu kabisa kuwa wao hawana mflame isipokuwa kaisari yule ambaye wanakataa kumpa kodi kwa sababu ni mpagani,  yule ambaye hawamtambui. Hii yote ni kwa sababu ya chuki.

Pilato ni mhusika asiyekuwa jasiri katika kusimamia mambo ya msingi na hasa haki. Pilato tayari alishaingia katika mgogoro na wayahudi, na wayahudi walimshitaki kwa Kaisari. Linapotokea hili Pilato anaogopa asipofuata matakwa yao watampeleka tena kwa kaisari na kibarua chake kitakua matatani kwasababu tayaria ana onyo. Pilato anafanya kituko kingine anapoweka chapa juu ya msalaba wa Yesu iliyokuwa inasema Yesu Mnazareti Mflame wa Wayahudi, Wayahudi walipombishia asiandike hivyo alishupalia msimamo wake, akasema niliyoandika nimeyaandika. Pale ambapo alitakiwa awe na msimamao katika kuhakikisha jambo la msingi kama haki ya kuishi inalindwa ameshindwa kushupalia msimamo wake hali aikijua fika kuwa Yesu hana kosa, lakini kwenye hili la chapa ambalo halina madahara yeyote haogopi macho ya Wayahudi anasimamia msimamo wake. Hata kwenye maisha yetu tunaweka msimamo kwenye mambo yasiyo na msingi lakini kwenye mambo muhimu hatuwi na msimamo thabiti.

Maaaskari waliokuwa chini ya msalaba ni wahusika wasiojali mahangaiko ya watu bali maslahi yao kwanza. Walikuwa wanahangaika kugawana vazi la Yesu kwa kulipigia kura liwe la nani. Yesu anateseka sana msalabani lakini wao si kitu kwao, lililo  muhimu ni mali zake wazigawane vipi . Ni mara ngapi tumewashuhudia watu wakikimbilia mifukoni mwa majeruhi wa ajali kutafuta pesa, simu na vitu vingine vya thamani na kuwaacha wakihangaika hadi kufa. Lori la mafuta limepata ajali watu wanakimbilia kuchota mafuta badala ya kuokoa majeruhi. Ndugu katika familia wanaanza kugombania mali za baba wa famiila anayekaribia kukata roho kitandani. Tumepoteza roho ya huruma na kuwajali watu katika mahangaiko yao. Wakati mwingine si lazima tuchukue mali zao, lakini tuko tunahangaika ili tupige picha tuzitume kwenye mitandao ya kijamii. Hatuna moyo wa huruma na kuwasaidia watu katika mahangaiko yao.

Kila mmoja akiingia ndani ya moyo wake leo anapomuona Yesu anateseka anajivika uhusika upi kati ya hao wanaojitokeza katika simulizi la mateso?. Tukumbuke basi siku ya leo ni ya kujiweka chini ya Yesu wa msalaba na kumuomba msamaha pale tuliposhiriki katika kumsulibisha na pia kuzidi kumuomba neema yake atuimarishe pale tuliposhiriki katika kumpigania na kumtetea ili tuzidi kumpenda daima.


Wednesday, 1 April 2015

ALHAMISI KUU. April 2, 2015

MISA YA KARAMU YA BWANA
Somo I. Kut 12:1-8, 11-14,  Somo la II. I Kor 11:23-26, Injili. Yn 13:1-15

Adhimisho la Karamu ya Bwana ndio mwanzo wa siku tatu kuu za pasaka yaani Ijumaa kuu, Jumamosi Kuu na Dominika ya Pasaka siku ambazo kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana. Hivyo siku tatu kuu za pasaka zinaanza kwa adhimisho hili na kuishia na masifu ya jioni ya pili ya Dominika ya pasaka. Leo kanisa kwa adhimisho hili la karamu ya Bwana linakumbuka mambo matatu; Kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu, Kuwekwa kwa Sakramenti ya Daraja na Amri kuu ya Upendo kwa Jirani.

Yesu alikuja duniani ili tuwe na uzima na ameanza tayari kazi yake hiyo katika maisha yake ya hapa duniani na kwa namna ya pekee kwa kifo chake pale msalabani. Baada ya ufufuko Yesu anapaa mbinguni lakini anataka aendelee kutupatia uzima kama alivyokuwa anafanya hapa duniani hadi ukamilifu wa dahari. Ili kufanikisha hilo anaweka ekaristi yaani mwili na damu yake. Katika ekaristi takatifu Yesu anaendelea kubaki nasi ili  kutupa uzima pamoja na kwamba alisharudi kwa Baba. Kwa maneno haya “twaeni mle wote huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu” na “twaeni mnywe wote hiki ni kikombe cha damu yangu, damu ya agano jipya la milele, itakayomwagika kwa ajili yenu na kwa ajili ya wengi kwa maondoleo ya dhambi, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, Yesu anaweka sakramenti ya ekaristi. Tuipokee sakramenti ya ekaristi kwa uchaji ili tupate uzima wa milele

Yesu alikuja Duniani ili kuanzisha safari ya ukombozi. Alifanya kazi hii kwa kufundisha, kuponya magonjwa, kulisha watu chakula cha mwili na roho, kuwapa faraja watu na kilele chake ni kifo cha msalaba. Baada ya ufufuko Yesu anarudi kwa Baba yake lakini anataka habari hii njema ya ukombozi wake iwafikie vizazi vyote hadi ukamilifu wa dahari. Anaweka sakramenti ya daraja ili kuwepo watu watakaomwakilisha na kufanya kwa niaba yake hapa duniani. Mitume wanawekwa rasmi kwa kazi hiyo kwa maneno haya “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, nao wanawarithisha vizazi vya mbele yao kazi hiyo kwa kuwawekea mikono.

Yesu katika karamu ya mwisho anaweka amri mpya ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Mapendo yanayodai kujinyenyekesha kwa hali ya juu kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Tunajifunza yafuatayo kuhusu kuwekwa kwa amri ya mapendo kadiri ya injili ya leo;

Yesu hali akijua kuwa amepewa mamlaka yote na Baba yake na kwamba saa yake ya kutukuzwa imefika,  hadhi ii kubwa haikumpa kiburi na badala yake alijinyenyekesha kiasi cha kuwaosha miguu mitume wake kazi iliyofanywa na watumwa. Unapogundua kuwa una karama fulani au cheo fulani unapata kiburi na kujiona mtu wa kutumikiwa zaidi au unajinyenyekesha na kutumikia?

Yesu alijua kuwa ametoka kwa Mungu na ya kwamba anarudi kwake lakini hali hii haikumfanya awadharau wanadamu na kuwa mbali nao kana kwamba sio wa aina yake badala yake ndio wakati hasa  alikuwa karibu nao  kiasi cha kufanya kazi ya watumwa ya kuwaosha wengine miguu. Kadiri unapokuwa karibu zaidi na Mungu kwa matendo yako mema unajiona kuwa hupaswi kuongea na kuwakaribia wadhambi au unatafuta nafasi ya kuwaonesha upendo wa Mungu ili wamuongokee?

Yesu  pia alijua kuwa saa yake ya kusalitiwa na kukanwa na Yuda na Petro, kwa namna ya pekee, imefika. Hili halikumfanya Yesu awake hasira na chuki dhidi ya mitume wake na hasa Yuda na Petro. Badala yake Yesu anawaka moto wa mapendo kwao kiasi cha kuwaosha miguu kama mtumwa afanyavyo kwa bwana wake.


Adhimisho la Karamu ya Bwana litusidie ili tumpokee Yesu wa ekaristi kwa imani na uchaji, tuwapokee mapadre kama Kristu mwingine, na tujibidiishe katika kuishi upendo katika kweli.