Somo I. Isa 52:13-53:12, Somo II. Ebr
4:14-16; 5:7-9, Injili. Yn 18:1-19:42
Kanisa zima linaadhimisha leo mateso na kifo cha Bwana wetu
Yesu Kristu msalabani. Ni siku ya kwanza katika siku kuu tatu za pasaka ambayo
tumeianza jana kwa adhimisho la karamu ya mwisho. Leo historia ya mateso ya Bwana
wetu Yesu Kristu inasomwa kadiri ya mwinjili Yohane. Tafakari yetu leo
itatazama ushiriki wa wahusika mbalimbali katika historia hiyo ili wahusika
hawa wawe kama kioo cha kujitazamia uhusiano wetu na Kristu pamoja na wenzetu
pia.
Mtume Petro ni mhusika anayemuendea Yesu katika ukweli na
wala hakuwa na unafiki. Petro alimpenda sana Yesu na daima aliishi kama alivyo,
alinena na kutenda kile alichoamini kuwa kinafaa machoni kwa Yesu, pale alipotenda mazuri Yesu
alimpongeza na pale alipotenda mabaya Yesu alimkemea ili ajirudi. Maisha ya
Petro yamekuwa ni ya kuanguka na kuinuka. Maaskari wanapokuja kumkamata Yesu, Petro
anamkata sikio mmojawapo wa wale waliokuja kumkamata kwa upanga. Yesu anamsihi
Petro arudishe upanga wake ili mpango wa Mungu utimie. Baada ya Yesu kukamatwa
wanafunzi wengine wanakimbia lakini Petro anamfuata Yesu mpaka ndani mbele ya
Kuhani mkuu. Baadae Petro aliyeonesha ushujaa mkubwa katika kumpigania Bwana
wake aliyempenda anaanguka kwa kumkana mara tatu. Ni kweli Petro ameanguka
lakini ameanguka katika mazingira ya kumfuata Yesu Kristu na ndio maana alipogundua
amekosa aliamka tena kwa kutubu. Yesu anamsamehe Petro na kumuweka kuwa
kiongozi wa kwanza wa kanisa lake kwa sababu moyo wa Petro daima ulimtafuta
Yesu, umeanguka katika safari ya kumtafuta Yesu, Petro ameamka ili aendelee
mbele.
Annas ni mhusika fisadi aliyedhamiria kumuangamiza Yesu hata
ikibidi kwa kukiuka misingi ya haki kwasababu alimpinga katika ufisadi wake. Annas
alikuwa ni mmiliki vibanda au maduka yaliyokuwa yanauza wanyama na vitu mbalimbali
kwa ajili ya kutolea sadaka hekaluni na
biashara hiii ilifanyika ndani ya hekalu. Wauzaji wa vitu hivi kwa ajili ya
kutolea sadaka waliwauzia watu kwa bei kubwa sana kuliko kama wangenunua nje ya
hekalu kiasi kwamba maskini walishindwa kumtolea Mungu wao sadaka. Watu walilazimika
kununua vitu hivi ndani ya hekalu kwa sababu vitu vilivyonunuliwa nje daima
vilichunguzwa ubora wake kama vinafaa na mara nyingi kama si mara zote
vilikataliwa. Hivyo Annas aliye wahi kuwa kuhani mkuu huko nyuma, kati ya mwaka
6 B.K n 15 B.K , alijipatia faida hekaluni kwa kuwanyonya maskini. Kadiri ya
mwinjili Yohane,( Yn 2:15-25), Yesu alikasirishwa sana na vitendo hivi
vilivyonajisi hekalu na kuamua kuwatimua wafanya biashara hekaluni. Annas, akiwa bado ana ushawishi katika ofisi ya
kuhani mkuu ambayo kwa wakati huu ilikuwa inakaliwa na shemeji yake Kayafa na
pia kwa watawala, anaamuru Yesu aletwe kwake kwanza kabla ya kwenda kwa Pilato.
Wayahudi walikuwa na sheria kuwa mtu hawezi kuhukumiwa kwa ushahidi wake
mwenyewe hivyo hapaswi kuulizwa maswali ili atoe ushuhuda wake mwenyewe, lakini
Annas anakiuka misingi hiyo kwa kumuuliza Yesu swali na Yesu anamkumbusha juu
ya utaratibu kwamba awaulize watu , wao ndio watatoa ushuhuda juu yake. Yesu akahukumiwa
kabla ya kesi kusikilizwa maana watu hawakuulizwa watoe ushuhuda.
Wayahudi ni wahusika wenye chuki kubwa sana dhidi ya Yesu
kiasi kwamba inawaziba, macho, akili na mioyo yao wasione, wasiwaze wala kuamua
sawaswa. Wayahudi tangu mwanzo walipinga vikali kulipa kodi kwa Kaisari na
sababu yao kubwa ilikuwa kaisari ni mpagani, Mungu pekee aliye mfalme wao ndiye
anastahili kupokea kodi yao. Mafasarisayo wanapomwendea Yesu na kumuuliza juuu
ya uhalali wa kulipa kodi kwa kaisari(Lk 20:22), wanataka kumtega kuona kama na
yeye anawaunga mkono ama la ili kupima Umasiya wake. Pia wayahudi tangu mwanzo
walijitambua kama taifa linalooongozwa na mfalme mmoja tu naye ni Mungu (1Sam
12:12), lakini leo Pilato anapowauliza nimsulibishe mfalme wenu wanajbu kwa
nguvu kabisa kuwa wao hawana mflame isipokuwa kaisari yule ambaye wanakataa kumpa
kodi kwa sababu ni mpagani, yule ambaye
hawamtambui. Hii yote ni kwa sababu ya chuki.
Pilato ni mhusika asiyekuwa jasiri katika kusimamia mambo ya
msingi na hasa haki. Pilato tayari alishaingia katika mgogoro na wayahudi, na
wayahudi walimshitaki kwa Kaisari. Linapotokea hili Pilato anaogopa asipofuata
matakwa yao watampeleka tena kwa kaisari na kibarua chake kitakua matatani
kwasababu tayaria ana onyo. Pilato anafanya kituko kingine anapoweka chapa juu
ya msalaba wa Yesu iliyokuwa inasema Yesu Mnazareti Mflame wa Wayahudi,
Wayahudi walipombishia asiandike hivyo alishupalia msimamo wake, akasema
niliyoandika nimeyaandika. Pale ambapo alitakiwa awe na msimamao katika
kuhakikisha jambo la msingi kama haki ya kuishi inalindwa ameshindwa kushupalia
msimamo wake hali aikijua fika kuwa Yesu hana kosa, lakini kwenye hili la chapa
ambalo halina madahara yeyote haogopi macho ya Wayahudi anasimamia msimamo
wake. Hata kwenye maisha yetu tunaweka msimamo kwenye mambo yasiyo na msingi
lakini kwenye mambo muhimu hatuwi na msimamo thabiti.
Maaaskari waliokuwa chini ya msalaba ni wahusika wasiojali
mahangaiko ya watu bali maslahi yao kwanza. Walikuwa wanahangaika kugawana vazi
la Yesu kwa kulipigia kura liwe la nani. Yesu anateseka sana msalabani lakini
wao si kitu kwao, lililo muhimu ni mali
zake wazigawane vipi . Ni mara ngapi tumewashuhudia watu wakikimbilia mifukoni
mwa majeruhi wa ajali kutafuta pesa, simu na vitu vingine vya thamani na kuwaacha
wakihangaika hadi kufa. Lori la mafuta limepata ajali watu wanakimbilia kuchota
mafuta badala ya kuokoa majeruhi. Ndugu katika familia wanaanza kugombania mali
za baba wa famiila anayekaribia kukata roho kitandani. Tumepoteza roho ya
huruma na kuwajali watu katika mahangaiko yao. Wakati mwingine si lazima
tuchukue mali zao, lakini tuko tunahangaika ili tupige picha tuzitume kwenye
mitandao ya kijamii. Hatuna moyo wa huruma na kuwasaidia watu katika mahangaiko
yao.
Kila mmoja akiingia ndani ya moyo wake leo anapomuona Yesu
anateseka anajivika uhusika upi kati ya hao wanaojitokeza katika simulizi la
mateso?. Tukumbuke basi siku ya leo ni ya kujiweka chini ya Yesu wa msalaba na
kumuomba msamaha pale tuliposhiriki katika kumsulibisha na pia kuzidi kumuomba
neema yake atuimarishe pale tuliposhiriki katika kumpigania na kumtetea ili
tuzidi kumpenda daima.
No comments:
Post a Comment