Somo I. Mdo 3:13-15, 17-19a, Somo II.
1Yn 2:1-5a, Injili. Lk 24:35-48
Kristu mfufuka analeta habari njema ya ondoleo la dhambi. Neno
la Mungu laendelea kutusisitiza kuwa ufufuko wa Kristu ni ushindi dhidi ya
dhambi na hivi namna sahihi ya kuupokea na kuuishi ufufuko huo ni kutafuta
nafasi ya mara kwa mara ya kujipatanisha na Mungu wetu kila tunapoanguka
dhambini na hasa dhambi za mauti.
Katika injili leo Kristu anawatokea mitume katika chumba na
akiwa huko anakula chakula pamoja nao baada ya kuwaonesha makovu ya mikono yake
na miguu yake. Yesu anayafanya haya ili kuthibitisha kuwa katika ufufuko wake
yeye si roho tupu wala si mzuka bali ni
Mungu kweli na mtu kweli ambaye mwili wake wa kibinadamu haukuhairibiwa wala kupotea katika kifo bali
umegeuzwa na kuwa katika hali ya utukufu. Kwa kuonesha makovu ya miguu na
mikono yake Kristu analenga pia kuonesha kuwa ufufuko wake umekuja baada ya
kuvumilia mateso makali ya msalaba kwa ajili ya wokovu wetu. Hivi ndivyo
tutakavyokuwa siku ya mwisho atakakapokuja. Sisi sote tunatumwa kuwahubiria
watu kuwa sasa tumepata ondoleo la dhambi kwa ufufuko wa Kristu.
Petro katika somo la kwanza anawatangazia watu habari ya
toba. Anawaeleza Wayahudi kuwa, pamoja na kwamba walimkana Yesu mbele ya Pilato
aliyetaka kumfungulia Yesu lakini wao wakataka mhalifu ndiye afunguliwe yaani
Baraba lakini Yesu asiye na hatia ndiye auawe, Kristu mfufuka anawasamehe
dhambi yao kwa kuwa hawakujua watendalo. Anawaalika watubu warejee ili dhambi
yao ifutwe kwasababu sasa wamejua maana ya mambo yote yaliyotokea kama
yalivyoaguliwa na manabii tangu zamani. Wayahudi hawakujua watendalo lakini
sasa wamejua ni heri kwao lakini wanawajibika sasa kuishi toba vinginevyo adhabu
inawangoja. Yeyote anayeshupaa katika ouvu hata baada ya kuoneshwa uovu wake na
kuonywa ataangamia.
Katika somo la pili mtume Yohane kawenye barua yake anawaasa
wakristu wote juu ya kuepuka dhambi na
daima wawe wepesi wa kuungama pale wanapoanguka. Yohane amekwishatueleza kwenye
sura ya kwanza ya barua hii kwamba ni uongo kwa mtu kusema hana dhambi na kweli
haimo ndani yake. Mtume Yohane anaona hatari kubwa ya watu kubweteka kutokana
na maeno haya wasione haja tena wala wasipate
msukumo wa kujibidiisha katika kuepa dhambi. Yohane pia kwenye sura hiyo
ya kwanza anasisitiza kuwa tukiziungama dhambi zetu yeye (Kristu) ni mwaminifu
atatusamehe dhambi. Kuna hatari pia watu wakaitumia vibaya huruma hii na
wasione haja ya kuungama wakiamini kuwa huruma itakuja tu. Katika somo la leo
Yohane anaweka msisitizo juu ya kuepuka dhambi na umuhimu wa kuziungama dhambi
zetu. Kumjua Mungu maana yake ni kushika amri zake.
Kuepa dhambi ni vita kubwa sana kwani shetani hapendi kabisa
kuona kuwa tunaongoka. Vita hii inahitaji utayari wetu, ujasiri na jitihada
zetu tukipata nguvu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Lazima tutambue kuwa hakuna njia
nyingine zaidi ya kujipatanisha na Mungu wetu ikiwa tunataka kufurahia matunda
ya utukufu wa ufufuko.
No comments:
Post a Comment