Somo I. Mdo 4:8-12, Somo II. 1Yn. 3:1-2, Injili Yn
10:11-18
Tunapoendelea kufurahia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu leo
tunaalikwa kujitahidi kadiri inavyowezekana kwa kutegemea msaada wake Mwenyezi
kubaki katika kundi la kondoo wa Kristu yaani kanisa lake. Yeye Kristu ni
mchungaji mwema, daima anatupigania na kutulinda dhidi ya mbwamwitu wakali. Iwapo
tutatoka katika kundi, na kutangatanga nje ya kundi, tutajiweka katika hatari ya
kushambuliwa na mbwa mwitu wakali, lakini pia tunaweza kujikuta tumeangukia
mikononi mwa wachungaji wanaofanya kazi kwa mshahara na hivyo kutojali sana
usalama wetu.
Katika injili Yesu anasema kuwa yeye ni mchungaji mwema na
kweli ndivyo alivyo. Ni mchumgaji mwema wa kondooo wake ambao ndio sisi
wakristu. Ni mchungaji mwema kwa sababu yuko tayari kutoa uhai wake ili
kutuokoa kutoka katika mikono ya mwbwa mwitu shetani anayetafuta kutumaliza. Anafanya
kazi yake si kwa sababu anatafuta faida yake binafsi bali kutokana na upendo
alionao. Anajua wazi kuwa kupoteza uhai wa kimwili kwa ajili ya kutulinda sisi
si kitu kwake kwani ni njia ya kufikia utukufu, atausalimisha uhai huo katika
ufufuko katika hali ya utukufu. Ni mchungaji mwema kwasababu anawajua kondoo
wake na yuko tayari kuwatafuta kondoo wote waliopotea na kuwarudisha kundini.
Wakristu tulio kondoo wa Kristu tunatumwa kufanya kazi kati
ya mbwa mwitu wakali, shetani na wafuasi wake wanaopinga kazi ya Kristu. Tuko katika
hatari kubwa ya kiroho na kimwili. Shetani daima anatafuta nafasi ya kuangamiza
uzima mpya tulioupokea katika ubatizo na katika sakramenti zingine hasa
ekaristi na kitubio. Uzima unaotusadia kuepuka dhambi na kuendelea kumtumikia
Mungu daima. Shetani pia anatafuta nafasi ya kuondoa uhai wetu wa kimwili ili
kutoa vitisho kwa kondoo wengine ili watawanyike na kumuacha nyuma mchungaji wao ha hivyo iwe
rahisi kwake kuwakamata na kuwaangamiza. Neno la Mungu leo linalenga
kutuondolea hofu dhidi ya Mbwa mwitu shetani. Tunaye mchungaji mwema ambaye yuko
tayari kutoa uhai wake ili kulinda na kutetea uhai wetu wa kiroho tulioupokea
kwa sakramenti. Lakini yupo tayari pia kutuondolea hofu dhidi ya kifo
tunapofanya kazi ya kumtangaza. Kifo cha mwili si kitu kwetu ikiwa tuna uzima
wa kiroho kwani ni mlango wa kufikia ukamilifu wa uzima huo wa kiroho mbinguni.
Katika somo la pili mtume Yohane anatueleza juu ya bahati
tuliyo nayo ya kuwa wana wa Mungu. Kwa Kristu mchungaji mwema kuutoa uhai wake
ametukumboa kutoka katika mikono ya shetani na kutufanya si watoto wa shetani
tena bali wana wa Mungu. Uhusiano wetu umekuwa si tu wa Muumba na viumbe vyake
bali Baba na wana wake. Ni uhusiano wa ndani uliojengwa katika misingi ya
upendo. Mungu aliye Baba yetu yuko tayari kutupigania na kututetea dhidi ya muovu
shetani ambaye kama alivyomuandama Kristu ataendelea kutuandama pia. Tunafanywa kuwa wana wa Mungu kwa neema yake
Baba kwetu lakini pia kwa jinsi tunavyopokea neema hiyo. Hakuna anayeweza kuwa
mwana wa Mungu kama hajapokea mwaliko wa kuwa mwana kwa kuishi maisha ya nuru. hawa
ndio kondoo ambabo Kristu asema kuwa walio wake anawajua nao wanamjua. Kufanyika
wana wa Mungu ni mwanzo wa safari ya kuelekea kufanana na Mungu pale
tutakapomuona uso kwa uso siku ya mwisho Kristu atakapokuja.
Katika somo la kwanza mitume wakiongozwa na Petro wanapata
ujasiri wa kuendelea kumhubiri Kristu mfufuka mbali ya kupokea vitisho vya
kuuawa kutoka kwa wakubwa wa watu na wazee wa Israeli. Ujasiri huu unatokana na
Imani yao kwa kristu aliyekwisha kuambia tayari kuwa yeye ni mchungaji mwema
yuko tayari kuwapigania kondoo wake dhidi ya mwovu shetani anayepambana
kuwanyima watu mbingu. Ufufuko wa kristu umewathibitishia ukweli huo sasa
hawana hofu tana na kifo ambacho shetani hutumia ili kuwakatisha tamaa wana wa
Mungu katika jitihada zao za kumhubiri Kristu.
Kristu mfufuka anatupigania daima katika maisha yetu. Pamoja na
kwamba Kristu anatulinda dhidi ya hatari za kimwili pia, lakini hasa yuko
tayari kutoa uhai wake ili tusipoteze uhai wa Ki-Mungu ndani ya roho zetu yaani neema ya utakaso tunayoipata kwa kupokea
sakramenti zake. Anapotulinda uhai wa kimwili anataka bado tuendelee kuishi
duniani ili tuufanyie kazi uhai wa Ki-Mungu
ndani ya roho zetu. Vinginevyo magonjwa, mateso, mahangaiko na hata vifo
vinavyotokea kwa wana wa Mungu havina madhara kwa uzima wa Ki-Mungu ndani ya
roho zetu ila badala yake vikipokelewa
kwa imani ni njia ya kupata uzima wa
milele Mbinguni.
No comments:
Post a Comment