Somo I. Mdo 10:34, 37-43, Somo II. IKor. 5:6-8, Injili. Mk 16:1-7
Leo kanisa
linaadhimisha fumbo la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu. Masomo ya leo yaeleza kuwa ufufuko wa Kristu
ni ushindi na ya kwamba sisi tunatumwa
kuwa mashahidi wa ushindi huo kwa maneno na matendo yetu. Ufufuko wa Kristu
unaleta maisha mapya, maisha katika Kristu, maisha ya milele ambayo mwanzo wake ni hapa duniani na
ukamilifu wake ni mbinguni. Wale wanawake watatu waliokwenda kaburini kadiri ya
injili ya leo walikuta kaburi li wazi na tupu, halina mwili. Lakini pale
ulipolazwa mwili waliona vitambaa alivyofungwa Yesu vimelala. Yesu amefufuka maana yake uzima wake wa
kibinadamu wa kimwili kupitia kifo chake umegeuzwa na kuwa uzima mpya wa
umilele, uzima usiokuwa na mipaka ya muda na mahali uzima usiokuwa na mahangaiko tena na ndio
maana sanda na vitambaa vingine alivyofungwa wakati wa kuzikwa vilibaki
kaburini Yesu alipofufuka. Hivyo ufufuko wa Yesu maana yake ni kupata maisha
mapya ya umilele katika mwili mpya wa utukufu. Sisi sote baada ya kumaliza
maisha ya hapa duniani tukiwa wenye imani tutafufuliwa na kuwa kama Yesu na
kuingia kwenye furaha ya milele na miili yetu ya utukufu.
Petro anahubiri juu ya
Kristu mfufuka katika somo la kwanza. Petro anatoa ushuhuda kuwa ufufuko ni
ushindi dhidi ya mateso na kifo cha mwili. Wayahudi walimwua lakini Mungu
alimfufua siku ya tatu. Si tu ushindi dhidi ya kifo cha mwili lakini Petro
anasema kuwa ufufuko huu ni ushindi dhidi ya kifo cha roho yaani dhambi na ndio
maana anamalizi kwa kusema kuwa kila amwaminiye atapokea ondoleo la dhambi,
maneno yale ambayo Kristu alimwambia Martha kuwa kila amwaminie ajapokufa
atakuwa anaishi(Yn 11:25). Petro anasema kuwa Kristu aliwaamuru wawe mashuhuda
wa habari hii njema ya ufufuko kwa maneno na maisha yao. Lazima kila mkristu
aushuhudie ufufuko wa Kristu kwa kuhubiri na kuishi vema. Unapozidi kushupaa
katika dhambi bila kutafuta nafasi ya kufufuliwa na Kristu wewe huamini kwamba Kristu alifufuka.
Katika somo la pili
mtume Paulo anatuasa kuwa maisha ya ufufuko yanadai kuachana na chachu ya kale
yaani dhambi na kuwa donge jipya yaani mioyo mipya. Sisi tuliofufuka pamoja na Kristu hatupaswi tena
kuridhika na dhambi. Paulo anaongea haya katika mazingira ambapo katika kanisa
la Korintho kulikuwa na maovu makubwa, uasherati ulizidi kiasi cha mtu kutembea
au kulala na mke wa baba yake yaani mama yake wa kambo. Kilichomkasirisha Paulo
ni kwamba kama jumuiya ya waamini walilifumbia macho jambo hili, wakaridhika na
maisha yaliendelea kama kawaida. Paulo anawaambia wasikubali kuwa karibu na
dhambi wakaridhika kwani dhambi ni kama chachu ambayo inasambaa taratibu mpaka
ngano yote inachachuka. Watu taratibu wataanza kuiga mfano baya wa mtu huyu
wakiona kuwa ni kawaida. Tunapaswa tushtuke, tusikitike tuone uchungu kila
tunapoona matendo maovu yakifanywa na watu wengine au na sisi na tuchukue
hatua. Tuna uhakika kwamba mapamabano yetu dhidi ya dambi yatafanikiwa
kwasababu tunaye Kristu aliyeshinda dhambi kwa ufufuko wake.
Katika somo la injili,
mwinjili Marko anatueleza habari ya ufufuko wa Kristu. Marko pekee kati ya
wainjili wote anasimulia kuwa yule mjumbe wa Mungu aliyewaambia wale wanawake
habari ya ufufuko alitamka kwao kuwa waende
wekawaambia wafuasi na Petro kwamba Kirstu mfufuka amewatangulia Galilaya.
Marko
anaweka msisitizo si tu kwamba wakawaambie wafuasi lakini na Petro. Kwa maneno
haya Marko anataka kuonesha kuwa ufufuko wa Yesu umeshinda dhambi ya Petro ya
kumkana Bwana wake mara tatu. Petro kwa sababu alimwamini na kumpenda Yesu hata
alipokufa katika dhambi ya kumkana Yesu anaendelea kuishi. Petro anaishi kwa
sababu hakuridhika na kumkana Yesu, tendo lile lilimpa uchungu, masikitiko na
mahangaiko ya moyo na hivyo akatafuta nafasi ya kuamka na kuanza tena na kwa
sababu hiyo Kristo alimfufua.
Ufufuko wa Kristu
unapaswa kutupatia mtazamo mpya wa maisha yetu ya hapa duniani. Tunapaswa sasa
kuyaona maisha ya hapa duniani kama maandalizi ya maisha ya milele. Tukiyatazama
mambo yote ya ulimwengu huu kama msaada wa kutufikisha kwa Mungu hatutakuwa na
hofu tena, hofu ya mambo ambayo dunia inayaona kuwa ndio kila kitu. Hatutakuwa na
hofu ya kifo tena kwasababu ni mlango wa maisha ya umilele. Tutakuwa watu wa
kutoa zaidi kuliko kupokea, watu wa kutumikia zaidi kuliko kutumikie. Hatuna hofu
ya kupoteza wala kuwa masikini kwa kutoa, hofu ya kudhalilishwa kwa kutumikia,
hofu ya kuchekwa kwa kutunza ubikira mpka siku ya ndoa takatifu.
No comments:
Post a Comment