MISA YA KARAMU YA BWANA
Somo I. Kut 12:1-8, 11-14, Somo la II. I Kor 11:23-26, Injili. Yn
13:1-15
Adhimisho la Karamu ya
Bwana ndio mwanzo wa siku tatu kuu za pasaka yaani Ijumaa kuu, Jumamosi Kuu na
Dominika ya Pasaka siku ambazo kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa
Bwana. Hivyo siku tatu kuu za pasaka zinaanza kwa adhimisho hili na kuishia na
masifu ya jioni ya pili ya Dominika ya pasaka. Leo kanisa kwa adhimisho hili la
karamu ya Bwana linakumbuka mambo matatu; Kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi
takatifu, Kuwekwa kwa Sakramenti ya Daraja na Amri kuu ya Upendo kwa Jirani.
Yesu alikuja duniani
ili tuwe na uzima na ameanza tayari kazi yake hiyo katika maisha yake ya hapa
duniani na kwa namna ya pekee kwa kifo chake pale msalabani. Baada ya ufufuko
Yesu anapaa mbinguni lakini anataka aendelee kutupatia uzima kama alivyokuwa
anafanya hapa duniani hadi ukamilifu wa dahari. Ili kufanikisha hilo anaweka ekaristi yaani mwili na damu yake. Katika ekaristi takatifu Yesu anaendelea
kubaki nasi ili kutupa uzima pamoja na kwamba
alisharudi kwa Baba. Kwa maneno haya “twaeni
mle wote huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu” na “twaeni mnywe wote hiki ni kikombe cha damu
yangu, damu ya agano jipya la milele, itakayomwagika kwa ajili yenu na kwa
ajili ya wengi kwa maondoleo ya dhambi, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, Yesu anaweka sakramenti ya ekaristi. Tuipokee sakramenti ya ekaristi kwa uchaji
ili tupate uzima wa milele
Yesu alikuja Duniani
ili kuanzisha safari ya ukombozi. Alifanya kazi hii kwa kufundisha, kuponya
magonjwa, kulisha watu chakula cha mwili na roho, kuwapa faraja watu na kilele
chake ni kifo cha msalaba. Baada ya ufufuko Yesu anarudi kwa Baba yake lakini
anataka habari hii njema ya ukombozi wake iwafikie vizazi vyote hadi ukamilifu
wa dahari. Anaweka sakramenti ya daraja ili kuwepo watu watakaomwakilisha na
kufanya kwa niaba yake hapa duniani. Mitume wanawekwa rasmi kwa kazi hiyo kwa maneno haya “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, nao
wanawarithisha vizazi vya mbele yao kazi hiyo kwa kuwawekea mikono.
Yesu katika karamu ya
mwisho anaweka amri mpya ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Mapendo yanayodai
kujinyenyekesha kwa hali ya juu kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Tunajifunza yafuatayo
kuhusu kuwekwa kwa amri ya mapendo kadiri ya injili ya leo;
Yesu hali akijua kuwa
amepewa mamlaka yote na Baba yake na kwamba saa yake ya kutukuzwa imefika, hadhi ii kubwa haikumpa kiburi na badala yake alijinyenyekesha
kiasi cha kuwaosha miguu mitume wake kazi iliyofanywa na watumwa. Unapogundua kuwa
una karama fulani au cheo fulani unapata kiburi na kujiona mtu wa kutumikiwa
zaidi au unajinyenyekesha na kutumikia?
Yesu alijua kuwa
ametoka kwa Mungu na ya kwamba anarudi kwake lakini hali hii haikumfanya
awadharau wanadamu na kuwa mbali nao kana kwamba sio wa aina yake badala yake
ndio wakati hasa alikuwa karibu nao kiasi cha kufanya kazi ya watumwa ya kuwaosha
wengine miguu. Kadiri unapokuwa karibu zaidi na Mungu kwa matendo yako mema unajiona
kuwa hupaswi kuongea na kuwakaribia wadhambi au unatafuta nafasi ya kuwaonesha
upendo wa Mungu ili wamuongokee?
Yesu pia alijua kuwa saa yake ya kusalitiwa na
kukanwa na Yuda na Petro, kwa namna ya pekee, imefika. Hili halikumfanya Yesu
awake hasira na chuki dhidi ya mitume wake na hasa Yuda na Petro. Badala yake
Yesu anawaka moto wa mapendo kwao kiasi cha kuwaosha miguu kama mtumwa
afanyavyo kwa bwana wake.
Adhimisho la Karamu ya
Bwana litusidie ili tumpokee Yesu wa ekaristi kwa imani na uchaji, tuwapokee
mapadre kama Kristu mwingine, na tujibidiishe katika kuishi upendo katika kweli.
Great homily padre keep up as days go on the blog will improve and become informative on pastoral issues even through photos
ReplyDeleteTumshukuru Mungu Bwana James
ReplyDelete