Tuesday, 26 May 2015

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU, MAY 31, 2015

Kum 4:32-34, 39-40, Rum 8:14-17, Inj Mt 28:16-20

Leo ni sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kanisa linaadhimisha fumbo la Mungu mmoja katika nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa kweli hili ni fumbo mama kati ya mafumbo yote ya Kikristu kwasababu linamhusu Mungu mwenyewe. Kwa akili ya kibinadamu tunaweza kwa kiasi fulani kufahamu juu ya uwepo wa Mungu, kwa mfano, kila tunapotafakari juu ya maajabu ya uumbaji. Lakini ukweli  kwamba Mungu huyu ana nafsi tatu tofauti zinazoshiriki Umungu mmoja tunaweza kuufahamu tu ikiwa Mungu mwenyewe anaamua kutufunulia na kwa fadhila ya imani. Neno la Mungu leo linatufunulia ukweli huu, tunahitaji paji la imani ili kupokea na  kuufahamu ukweli huu.

Mungu wetu ni mmoja mwenye nafsi tatu, hili ni fumbo kweli kwetu sisi wanadamu kwani kila tunapojaribu kuelewa ni kwa namna gani hili linawezekana tunashindwa kwani akili yetu ni finyu sana kumuelewa Mungu asiye na mipaka na wa milele. Tunapata shida kuelewa kwasababu kwetu sisi nafsi ya mtu ni ya kipekee inafikiri na kutenda katika upekee na hivyo kuwa na nafsi mbili na zaidi maana yake ni kuwa na watu wawili na zaidi walio tofauti katika kufikiri na kutenda. Kila tunapojaribu kuzitazama nafsi tatu za Mungu kwa namna yetu hii ya kibinadamu tunakwama kwani ufunuo wa neno la Mungu unatueleza kuwa katika Mungu hakuna nafsi inayofikiri na kutenda kipekee, Baba yu ndani ya Mwana na Mwana yu ndani ya Baba kadhalika wote wako ndani ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu yu nadani ya Baba na Mwana. Nafsi zote tatu za Mungu zinafikiri na kutenda katika umoja kamili wa Umungu. Anachofikiri baba ndicho anachofikiri Roho Mtakatifu na Mwana pia.  Hivyo nafsi tatu hazifanyi miungu watatu, bali zote zi na asili ya Umungu ule ule, na hili ndilo fumbo lenyewe

Ufunuo wa ukweli huu wa Utatu Mtakatifu watuonesha kuwa Mungu wetu yu hai,  na zaidi ya hayo anatupenda sana. Mtume Paulo kwenye somo la pili la leo anaonesha kuwa Mungu wetu anatupenda sana na hili linaonekana pale anapoamua kutufanya sisi wana wake kupitia nafsi yake ya pili yaani Kristu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ambaye Paulo anasema yeye ndiye anayeshuhudia tukio hilo la sisi kufanyika wana. Roho Mtakatifu nafsi ya tatu anatuwezesha sisi kumtambua nafsi ya kwanza ya Mungu kuwa ni Baba yetu. Anatufanya sisi kuwa ndugu wa Kristu, warithi pamoja naye wa mateso na utukufu. Katika somo la kwanza pia laonesha upendo wa Mungu kwa mwanadamu kupitia matendo makuu ya kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri.

Katika somo la injili, mwinjili Matayo anaonesha umoja wa Umungu  wa nafsi tatu. Kristu nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeweka sakramenti saba, na kwa namna ya pekee ubatizo, ambazo ni alama wazi ya wokovu wetu kwa kifo chake msalabani.  Kristu anapowatuma wafuasi wake waende ulimwenguni kote na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake anawaamuru wabatize kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hii maana yake ni kwamba katika kazi ya ukombozi ambayo Kristu, nafsi ya pili ya Mungu ndiye aliyeifanya, nafsi zote tatu zinashiriki katika kazi hiyo kwa ukamilifu wake.

Sherehe hii ya Utatu Mtakatifu inalenga kutukumbusha mambo makubwa mawili; moja ni kwamba kujua ukweli huu kuhusu Mungu wetu anayeishi na kutupenda sana, kunatupa wajibu wa kumrudishia sifa na shukrani kwa maneno na matendo yetu. Ingawaje sifa zetu hazimzidishii  Mungu chochote lakini zatufaa kwa waokovu wetu. Tunamsifu Mungu kwa nafasi ya kwanza kwa sala na ibada zetu. Wapo watu wanaodai kuwa hakuna ulazima wa kwenda kanisani kusali dominika alimradi wanajitahidi kuepuka maovu na kutoa misaada. Hii si kweli kabisa , kuna umuhimu na ulazima wa kumkiri Mungu kwa midomo yetu kupitia sala, nyimbo na ibada, tendo hili linaelezea na kuimarisha imani na  upendo wetu kwa Mungu na linatupa nguvu ya kuishi vema amri ya mapendo. Katika ibada ya misa takatifu tunachota neema ya kuishi kitakatifu.

Jambo la pili tunalokumbushwa leo ni umoja. Katika Mungu kuna nafsi tatu tofauti lakini zinatenda kwa umoja kamili wa Umungu. Tunapaswa kuwa na umoja kwanza wa sisi wenyewe ndani yetu, umoja ambao unalenga kulinda hadhi yetu kama wakristu. Ikiwa akili inayoelewa mambo, haina umoja na utashi unaoamua kulingana na mwangaza wa akili daima nafsi ya mtu itakuwa katika fujo. Ikiwa dhamiri ya mtu haina umoja na utashi wake pia mtu hukosa amani na daima atakuwa mtumwa. Kama hakuna umoja kati ya utashi wa mtu na mwili wake matokeo yake pia ni vurugu ndani ya mtu. Kwa mfano, ikiwa dhamiri ya mtu inamsukuma kuacha ulevi lakini utashi wake unashindwa kuamua kadiri ya matakwa ya dhamiri yake njema, mtu huyu daima atakosa amani kwani dhamiri yake itaendelea kumsuta kila mara kwa kuamua kinyume na  matakwa yake. Kama ndani ya mtu kuna umoja daima kutakuwa na amani na matunda yake ni kwamba familia zitakuwa na umoja, jumuiya, nchi na dunia kwa ujumla itakuwa na umoja.

Tusali daima kuomba paji la Roho Mtakatifu la Ibada ili tuendelee kuusifu Utatu Mtakatifu daima na zaidi ya hayo tuuishi umoja usiogawanyika unaopatikana katika Utatu Mtakatifu.



Friday, 22 May 2015

DOMINIKA YA PENTEKOSTE, MWAKA B. MAY 24, 2015

I.                    Mdo 2:1-11    II. 1 Kor 12:3b-7, 12-13  Inj. Yn 20:19-23
Siku ya hamsini ya kipindi kitakatifu cha Pasaka inahitimishwa na Dominika ya Pentekoste, kanisa linapokumbuka kazi ya Roho Mtakatifu kwa Mitume, mwanzo wa Kanisa na mwanzo wa utume wake kwa lugha, watu na mataifa yote. Roho mtakatifu analitakasa kanisa, analifariji katika mahangaiko yake ya hapa duniani na pia analiwezesha katika utume wake kupitia vipaji, karama na huduma mbalimbali anazozimimina kwa wanakanisa kadiri apendavyo

Katika injili leo Yohane anatupatia simulizi la Yesu mfufuka akiwatokea mitume katika chumba na anapowatokea anawaambia mambo kadhaa ambayo kwa kweli yanagusa pamoja na mambo mengine  utume wetu kama wana kanisa

Tunajifunza kuwa Kristu anahitaji Kanisa katika kuendeleza kazi yake ya ukombozi aliyoianzisha. Baada ya kupaa kwake mbinguni mitume wanapaswa kuwaongoza wanakanisa kwenda ulimwenguni pote na kwa kila kizazi kushuhudia ufufuko wa Kristu ili ulimwengu mzima upate wokovu. Twajua kuwa Kristu ndiye kichwa yaani Kiongozi wa Kanisa lakini anahitaji miguu, mdomo na mikono ya kupeleka ujumbe wake kwa watu wote akiwa ameketi kuume kwa Baba. Kanisa ndio miguu, mikono na mdomo wake. Kristu anategemea kanisa lenye wanadamu wasio wakamilifu wanaopambana kuufikia wokovu wao wenyewe kwanza halafu watu wengine. Kwa hiyo ni wazi kwamba kushuhudia wanakanisa wakianguka katika udhaifu  isiwe kigezo cha kukata tamaa na kulikimbia kanisa kwa sababu Kristu mwenyewe amechagua Kanisa dhaifu lifanye kazi yake.

Katika kufanya kazi ya utume Kanisa linamuhitaji sana Kristu. kwa sababu kanisa linafanya kazi ya utume hivyo lazima kuwepo na yule aliyelituma, ujumbe wa kupeleka, nguvu na mamlaka ya kupelekea ujumbe huo. Kristu ndiye anayelituma Kanisa, na analipa ujumbe wa wokovu kwa watu wote na zaidi ya hayo analipatia nguvu na mamlaka ya kupeleka ujumbe huo kupitia Roho Mtakatifu tunayempokea leo katika sherehe ya Pentekoste. Katika udhaifu wake kanisa linahitaji kujishikamanisha na Kristu daima ili liweze kufanikiwa maana Kristu mwenyewe anatuambia bila yeye hatuwezi chochote.

Kama Baba alivyomtuma Mwana ulimwenguni ndivyo Kristu anavyolituma Kanisa lake. Utume wa Kristu uliwezekana na ulifanikiwa kwa sababu tu Kristu alikuwa mtii kwa yule aliyemtuma na pia alimpenda sana. Kanisa linamwakilisha Kristu duniani hivyo daima linapaswa kuwa mtii kwake ili lisije kupeleka ujumbe wake badala ya ujumbe wa Kristu. Upendo ndio msingi wa utume wetu, yatupasa kuwa tayari kutolea maisha yetu kwa ajili ya yule aliyetutuma

 Kristu anatualika tupeleke ujumbe wa msamaha wake kwa wadhambi wanaotubu. Anapowaeleza mitume wake juu ya mamlaka ya kufunga na kufungua anawatuma waende ulimwenguni kote na kuwaeleza watu kuwa Kristu alikuja duniani kuwasamehe watu makosa yao. Atakayekuwa tayari kutubu na kuomba msamaha atasamehewa lakini yule anayekataa msamaha wake hatapokea msamaha huo.

Katika somo la pili mtume Paulo anatueleza kuwa utume wa kanisa unawezekana kwa sababu Roho Mtakatifu anagawa karama, vipaji na huduma mbalimbali kwa watu wake. Kupitia karama hizi wanakanisa wanapeleka ujumbe wa Kristu kwa watu. Karama mbalimbali zinatolewa kwa ajili ya manufaa ya Kanisa zima na wala si kwa ajili ya sifa na utukufu wa wale waliojaliwa karama hizo

Somo la kwanza ni simulizi la tukio la Pentekoste ambalo kwa kweli linaonesha kazi ya Roho Mtakatifu kwa mitume, mwanzo wa Kanisa, mwanzo wa utume wa kanisa kwa lugha, watu na mataifa yote. Ni muhimu kuelewa awali ya yote kwamba Roho Mtakatifu yupo na amekuwepo daima akifanya kazi kati ya watu hata kabla ya tukio hili ya Pentekoste. Ingawaje ni ukweli kwamba kuna kitu cha pekee kilitokea siku hiyo ya Pentekoste. Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu aliwavuvia mitume na kuwapa zawadi na karama ya ajabu ambayo hawakuwahi kuipata kabla. Uvuvio huu wa Roho Mtakatifu uliwafanya mitume walihubiri neno la Mungu kwa namna ambayo kwa mara ya kwanza iligusa mioyo ya watu na walielewa vizuri sana.

Wapo watu wanaosema kuwa mitume walipata uwezo wa kunena kwa lugha kama ishara ya kuvuviwa na Roho Mtakatifu. Kunena kwa lugha kunakozungumziwa na ule uwezo wa kutamka maneno ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuelewa, jambo ambalo lilikuwepo hata katika kanisa la mwanzo. Watu hawa wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa hiyo ndio ishara ya muhimu na ya pekee ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Mtume Paulo ameeleza kwa kirefu juu ya kipawa cha kunena kwa lugha katika (1Kor 14) lakini kwa ufupi anachoeleza ni kuwa kipaji chochote anachotoa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya manufaa ya jumuiya, la kama mtu amepewa kipaji na hakiwasaidiii wanajumuiya katika kuabudu kwao isipokuwa yule aliyepewa basi asikitumie katikati ya wanajamii hasa katika sala. Zaidi ya hayo hatuwezi kusema kuwa kiuongo kimoja katika mwili ndio chenye umuhimu kuliko vingine kwa sababu ili mwili uitwe mwili unahitaji kuwa na viunguo vyote kamili na ndio maana wasio na viungo fulani huitwa walemavu ingawaje hawajapoteza utu wao. Haiwezekani kipaji kimoja tu ndio kikawa muhimu kuliko kingine katika mwili wa fumbo wa Kristu yaani Kanisa.


Hivyo katika pentekoste si kwamba mitume walipata hiyo karama ya kunena kwa lugha kwa sababu kila walichokiongea watu walikielewa. Kipaji cha kunena kwa lugha kadiri ya Paulo ni kwa ajili ya yule tu mwenye kipaji hicho na watu wengine hawawezi kumuelewa. 

Thursday, 14 May 2015

DOMINIKA YA SABA YA PASAKA, MWAKA B. MAY 17, 2015

Mdo 1:15-17, 20a, 20c-26,  I Yoh 4:11-16, Inj. Yn 17:11b-19

Wakristu tunao uhakika kuwa  kiongozi wetu Yesu Kristu hata baada ya kupaa kwake mbinguni anaendelea kuwa pamoja nasi kutuongoza, kutuimarisha, kutubariki katika safari yetu ya kuelekea kule aliko yeye. Kwa mara nyingine leo tunakumbushwa kuwa ukristu wetu unatudai mambo makubwa sana yanayohitaji kujitoa mhanga kwa ajili ya Kristu kiongozi wetu. Peke yetu hatuwezi ni lazima tuombe msaada wake kwa njia ya sala yeye aliyetuahidi kuwa pamoja nasi mpaka mwisho wa safari.

Katika njili Yesu kuhani mkuu analiombea kundi lake kabla ya kuteswa, kufa, kufufuka na kupaa kwake mbinguni. Katika sala ya Yesu tunaweza pamoja na mambo mengi tukatafakri mambo makubwa manne kuhusu ukristu wetu.

Mkristu safi, hodari na shujaa si yule anayejitenga na ulimwengu bali yule anayeishi ndani ya ulimwengu lakini anaushinda ulimwengu. Yesu haombi kwamba tutoke ulimwenguni bali tulindwe na yule mwovu. Mara nyingi nimesikia watu mbalimbali walio katika ndoa wanawaambia mapadre na watawa kuwa afadhali wao wamechagua maisha ya kujitenga na ulimwengu kwa kuwa watawa  au  mapadre kwani wameepukana na maouvu ya ulimwengu. Ingawaje si kweli kwamba mapadre na watawa wametoka katika ulimwengu huu lakini hoja ya watu wanaofikiri hivyo kuhusu mapadre ni kwamba mtu atakuwa mkristu mzuri kama atatoka katikati ya ulimwengu uliojaa maovu jambo ambalo si la kweli. Wapendwa maisha ya ukristu maana yake ni kwenda kinyume na ulimwengu huo huo tunaoishi. Tunapaswa kuwa mashuhuda wa Kristu, kwa mfano, katika ulimwengu unaotumia mitandao ya kijamii kubomoa maaadili kwa sisi kutumia mitandao hiyo vizuri na si kuacha kutumia. Ukristu hautuweki huru dhidi ya matatizo bali unatupa mbinu za kupambana na matatizo

Wakristu tumewekwa wakfu yaani tumetengwa kwa ajili ya kazi maalumu. Sehemu ya mwisho ya sala ya kristu katika injili ya leo yaeleza ukweli huu Kristu anapoomba tutakaswe na hiyo kweli. Tumezoea kuwa mapadre na watawa tu ndio wamewakwa wakfu lakini ukweli ni kwamba kwa ubatizo wetu sisi sote tumetengwa kwaajili ya kazi maalumu ya kumshuhudia Kristu popote ulimwenguni kwa maneno na matendo yetu. Ni kweli kwamba mapadre na watawa wamewekwa wakfu kwa namna ya pekee lakini hili halifuti ukweli kuwa kila mbatizwa amewekwa wakfu kuwa shahidi wa Kristu. Kila mkristu popote alipo anapaswa kutambua kuwa yeye ni mteuliwa wa Kristu, ametengwa kwa ajili ya kumtambulisha Kristu kwa watu kwa utakatifu wake. Unapokuwa shuleni, sehemu ya kazi, nyumbani unapaswa kutambua kuwa wewe umechaguliwa na Kristu kuwa mfano wa maisha ya utakatifu, kinyume cha hapo unakufuru kwa kutenda uovu.

Silaha ya kumshinda mwovu hapa duniani ni kwa wakristu kuwa na umoja. Ni kwa bahati mbaya sana kati ya vitu ambavyo Kristu aliliombea kanisa lake umoja wa wakristu umepata misukosuko mingi. Wakristu wanapaswa kuwa na roho moja na moyo mmoja katika Kristu. Wapo watu katika ulimwengu huu ambao wanatumia silaha ya utengano kwa wakristu ili kujinufaisha katika mambo yao. Tumeona mara kadhaa wanasiasa wanavyovuruga kanisa ili likose msimamo mmoja katika kutetea maadili mema na hivyo wapate nafasi ya kukanyaga haki za watu kwa manufaa yao binafsi.

Wakristu tuna uhakika wa ulinzi wa Kristu dhidi ya mwovu tukiwa ulimwenguni. Yesu anatulinda kwa kweli ili tusiingie katika mtego wa shetani wa kutenda dhambi. Ulinzi huu tutaupata ikiwa tutakuwa tayari kuutafuta. Mara kadhaa kumekuwa na maswali inakuwaje watu wasio na hatia wanateseka na kufa kutokana na makosa ya watu wengine ikiwa Kristu anatuombea kwa Baba ili tulindwe na huyo mwovu. Si rahisi sana kusema kwa uhakika kwa nini haya yanatokea kwa sababu mateso bado ni fumbo kwetu. Lakini sisi wakristu daima tunaalikwa kumuangalia Kristu kiongozi wetu ambaye aliishi kila kitu sawa na sisi isipokuwa hakutenda dhambi, na bado akafa kifo cha aibu msalabani. Ufufuko wake umedhihirisha kuwa mateso ya mwili kwa mkristu si kitu ikiwa ameishi akiwa anamwamini Kristu. Hivyo pale inapotokea watu wasio na hatia wanateswa  na kufa na wakati mwingine kwa sababu ya imani yao, hatupaswi kumlaani Mungu kwa kudhani kuwa Mungu hayupo au hatupendi.

Somo la kwanza latutafakarisha juu ya wajibu wetu wa Kikristu. Katika kumchagua mtu atakayekuwa mbadala wa Yuda Iskariote wakristu wakwanza  waliongozwa na neno hili kuwa anapaswa awe shahidi wa ufufuko wa Kristu. katika somo hilo tunaelezwa jinsi ambavyo kanisa letu lenye watu zaidi ya bilioni leo hii lilikuwa na watu 120 tu wakati Matiya anachaguliwa kuwa mbadala wa Yuda. Inaonesha jinsi gani wakristu wa kwanza walifanya kazi kubwa ya kushuhudia ufufuko wa Kristu kiasi cha mimi na wewe leo kuitwa wakristu na huo ndio wajibu wetu mkuu kama wakristu.

Uhusiano wetu na Kristu umejengwa katika msingi wa upendo, hivyo ndivyo anavyotuambia Yohane katika somo la pili. Mungu ni upendo, kwa upendo wake ametuumba, ametukomboa, anaendelea kututegemeza na atatupa tuzo ya urithi wa mbingu milele. Kila tunapopendana tunakaa ndani ya Mungu, tunamualika Mungu kati yetu na Mungu anakaa ndani yetu. Upendo wa Mungu unajidhihirisha katika unyenyekevu. Ni rahisi sana mtu kuonesha unyenyekevu kwa mtu aliye mkubwa wake, kiumri ama kicheo au yule aliye na vipaji vingi kumzidi. Hebu fikiri ilivyo ngumu kwa mtu kujinyenyekesha kwa mdogo wake kiumri ama kicheo au kwa mtu aliyemzidi katika elimu ama vipaji na karama mbalimbali. Hivi ndivyo Mungu alivyotupenda, yeye aliyekuwa Mungu akatwaa hali ya utumwa ili atutumikie sisi viumbe vyake


Ikiwa kila mkristu ataona kuwa maisha ya hapa duniani ni maandalizi tu ya maisha mazuri na yenye raha mbinguni, itakuwa ni motisha tosha ya kupambana siku hadi siku  ili kufikia maisha hayo. Tuombe kwa Mungu ili daima tutafute kuwa mashuhuda wake kwa maneno na matendo yetu ili kufikia ukamilifu anaoutegemea kwetu.

Monday, 4 May 2015

DOMINIKA YA SITA YA PASAKA, MWAKA B. MAY 10, 2015

I.                    Mdo. 10:25-26, 34-35, 44-48, II. IYoh 4:7-10, Inj. Yn 15:9-17

Tunapokwenda kusali misa leo katika dominika ya sita ya pasaka  tujitahidi kadiri inavyowezekana kuruhusu Kristu mfufuka azidi kuijaza mioyo yetu kwa furaha kuu ya kipasaka. Furaha ambayo inatokana na sisi kuwekwa huru na dhambi na hivyo itupe hamu ya kuishi ufufuko huo kwa matendo ili tuzidi kuipata zaidi na zaidi katika maisha yetu ya hapa duniani na baadae tukaipate kwa ukamilifu huko Mbinguni.

Katika somo la injili tunaelezwa kuwa Yesu ametupa upendeleo mkubwa sana wa kutufanya sisi kuwa rafiki zake. Ni desturi ya mahali pengi duniani kwa baadhi ya watu wachache kupata bahati ya kuwa marafiki wa viongozi katika ngazi mbambali ikiwemo ya ufalme au uraisi. Desturi hii ilikuwepo pia katika dola ya Kirumi. Mfalme alikuwa na kikundi cha watu kadhaa ambao aliwaita ni marafiki zake na kwa kweli walikuwa marafiki zake. Marafiki hawa waliweza kumuona mfalme wakati wowote ule mara nyingine bila hata kupitia kwa wasaidizi wake kwa kutoa taarifa mapema. Mfalme mara kadhaa aliongea kwanza nao kabla ya kuongea na wasaidizi wake au raia kwa ujumla. Walifahamu siri binafsi za mfalme na daima hawakuwa tayari kumuangusha mfalme wala kumuudhi, mfalme anapotoa agizo fulani hawa ndio watakuwa wa kwanza kulitekeleza na kulitetea mbele ya raia wengine. Kwa ujulma walikuwa na uhusiano wa ndani na wa karibu na mflame kupita hata wasaidizi wa karibu wa mfalme.

Yesu aliye mfalme wetu anatuita sisi rafiki ili tuwe na uhusiano wa karibu naye kama wa wale marafiki wa mfalme wa Kirumi. Sisi si watumwa tena kwa sababu mtumwa hastahili kumsogelea bwana wake bali sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu tuna ruhusa ya kumsogelea na kumuendea  Yesu wakati wote kupitia sakramenti zake. Sisi ni rafiki wa Yesu kwa sababu Yesu ametushirikisha siri za Mbinguni kama ambavyo marafiki wa mfalme wa Kirumi walivyojua siri binafsi za mfalme wao. sisi ni marafiki wa Yesu kwa sababu mara kwa mara tunazungumza naye iwe wakati wa raha na shida kupitia sala za jumuiya na sala binafsi. Sisi ni marafiki wa Yesu kwa sababu hatutaki kumuangusha Yesu na ndio maana sisi kama walivyo marafiki wa mfalme wa Kirumi, tutakuwa wa kwanza kutii amri ya mfalme wetu.

Mfalme wetu Yesu anataka sisi tuishi upendo unaodai kujitoa sadaka kwa ajili Mungu na jirani  kwa sababu yeye amefanya hivyo kwa ajili yetu. Marafiki wa mflame wako tayari kutii amri ya mfalme kwa matendo na kuitetea kwa watu. Yesu anasema huu ndio upendo unaowatofautisha marafiki wa Yesu na wasio marafiki wake. Upendo wa kujitoa nafsi hata ikitubidi kufa  kwa ajili ya wenzetu. Ningependa hapa tutafakari jambo ambalo ni changamoto sana katika jamii yetu sasa linalohusu uhuru wa kuvaa. Uhuru ni jambo la thamani sana na linalompa hadhi mwanadamu na kila mwanadamu anatamani autumie uhuru wake kikamilifu. Kila mtu anao uhuru wa kuvaa nguo yeyote anayoipenda, lakini inapotokea nguo hiyo inasababisha wengine watende dhambi ya uzinifu si busara sana kwa rafiki wa mfalme Yesu  kusema hayo ni matatizo yao watajijua na Mungu wao. Kujitoa sadaka uhuru wako kwa ajili ya kulinda dhamiri dhaifu za wengine ni upendo unaomtofautisha rafiki wa  Yesu na asiye rafiki wa Yesu.

Mtume yohane anaendeleza wazo la upendo katika somo la pili katika waraka wake. Hapa Yohane anaonesha ukubwa, thamani na umuhimu wa fadhila hii ya Upendo. Ni fadhila ya Ki-Mungu, inatoka kwa Mungu na Mungu ndio upendo wenyewe. Hivyo kama tunapenda ni kwasababu Mungu ametuwezesha kupenda na ametuonesha mfano wa kupenda kwa kutupenda sisi kwanza. Mtu anayependa anamjua Mungu kwa sababu yeye ndiye upendo wenyewe na anayemjua Mungu anapenda kwa sababu ni katika kupenda tunamuona Mungu. Mtu anayependa anakuwa karibu zaidi na Mungu.

Katika somo la kwanza Petro akiongozwa na Roho wa Mungu anasema kuwa masharti ya kuwa mkrisu yaani  kuwa rafiki wa Kristu ni kusadiki na kupokea ubatizo. Kulikuwa na mgogoro katika kanisa la mwanzo kuhusu ikiwa ni lazima kwa mpagani kutahiriwa kwanza kabla hajabatizwa na kuwa mkristu. Wayahudi waliokuwa wakristu walishikilia msimamo kuwa ni lazima wapagani wasiokuwa wayahudi wakatahiriwa kwanza kama sharti la kuwa myahudi kwanza kabla ya kubatizwa. Petro anatatua mgogoro huyo kwa kuweka msimamo unaodhihirisha jinsi gani Mungu asivyo na upendeleo. Mungu yuko tayari kumkubali yeyote yule kwa sharti moja tu la uchaji na kutenda haki. Wazo la injili ya leo linaingia hapo kwamba sisi ni rafiki wa Kristu ikiwa tutazishika amri zake. Lakini pia wazo la upendo wa Kikristu ambao Kristu anataka sisi tulio rafiki zake tuuishi, upendo usio kuwa na ubaguzi wala usiowawekea watu masharti magumu yasio na lazima katika kumuendea Mungu wao. Yapo makanisa leo hii wachungaji na maaskofu wao wanatoa baraka kulingana na kiasi cha pesa alichotoa mtu badala ya kuangalia moyo wa ukarimu wa mtu. Si lazima kwamba aliyetoa pesa nyingi ndiye ana imani na ukarimu zaidi ya yule aliyetoa kidogo.


Kuwa rafiki wa Yesu kunaleta furaha sana, na yeyote anayemtembelea rafiki yake anataka kupata furaha. Hebu fikiri rafiki yako amekuja kukutembela halafu muda wote sura imekunjamana haongei kitu na wala hajibu kitu unapomsemesha, utajisikiaje? Ni wazi huwezi kujisikia vizuri. Mara nyingi sisi tumekwenda kumtembela rafiki yetu Yesu tukiwa na sura zimekunjamana hatuna furaha. Hatuongei chochote na hata Yesu akitusemesha kupitia kinywa cha padri hatuitikii kabisa au tunaitikia kama tumelazimishwa. Unaweza kufikiri tena unakuwa na rafiki ambaye anakufuata wakati wa shida tu, na hapo utajisikiaje?  Je sisi hatufanyi hivyo kwa rafiki yetu Yesu? Je hatumdhalilishi rafiki yetu Yesu kwa kuwa wa kwanza kuvunja au kutofuata maagizo yake na kwenda mbali zaidi kuwahamasisha wengine wasitimize amri za Kristu?. Tusali na kujiibidiisha ili tuwe marafiki wema wa Kristu 

Monday, 27 April 2015

DOMINIKA YA TANO YA PASAKA, MWAKA B. MAY 3, 2015

I.                   Mdo 9:26-31, II. IYoh 3:18-24, Inj. Yn 15:1-8

Sisi tumefanywa kuwa watoto wa Mungu kwa ukombozi wa Kristu. Tumewekwa huru dhidi ya utumwa wa dhambi na hakika huu ndio uhuru wa kweli. Hatuwezi kuendelea kuwa wana wa Mungu, kuwa na uhuru huu wa kweli ikiwa tutatetereka katika imani, imani inayodai kujiunganisha maisha yetu na Kristu. Masomo ya leo yanatuelekeza katika kuishi fadhila zitakazoimarisha uhusiano wetu na Kristu

Yesu ni mzabibu wa kweli maana yake Yesu ndiye wokovu wetu wa kweli. Tawi lisilokaa ndani ya mzabibu haliwezi kuzaa na mkulima huliondoa, lakini lile likaalo ndani ya mzabibu huzaa na mkulima hulisafisha vizuri ili lizae sana. Sisi tu matawi ya Yesu aliye mzabibu wa kweli. Kama tukichagua kukaa ndani ya Yesu tutazaa matunda, la tusipokaa ndani yake tutanyauka, tutaondolewa na kutupwa motoni na kuteketea. Yeyote anayekaa ndani ya Yesu, Yesu hukaa ndani yake pia naye huzaa sana. Mkristu anayekataa kusikia sauti ya Yesu na kuenenda kadiri ya maelekezo ya ulimwengu atanyauka na kuteketea kiroho na kimwili jehanum. Pia yule mkristu anayemkiri Yesu kwa mdomo tu lakini kimatendo yuko mbali naye atanyauka na kuteketea jehanum. Wale ambao wanamfuata Yesu wakati wa raha tu lakini wanapopata misukosuko wanamkimbia watanyauka pia. Bila Kristu hatuwezi kitu. Mkristu atakuwa ndani ya Kristu daima kwa kusali mara kwa mara, kusoma na kutafakari neno la Mungu na kwa namna hii atamtukuza Mungu daima.

Mtume Yohane katika somo la pili anatufundisha kwamba kuwa mkristu maana yake ni kuwa na imani sahihi katika Kristu na kutenda  au kuishi kadiri ya imani hiyo sahihi. Imani yetu inapaswa kuwa katika jina la Yesu, yaani nafsi ya pili ya Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu, akaishi sawa nasi katika kila kitu lakini hakutenda dhambi. Alikufa kwa ajili yetu na akafufuka katika wafu li kutupa tumaini jipya na alikwenda kutuandalia makao ya milele mbinguni. Yesu huyu alitupa amri ya mapendo akatutaka tumuige yeye kama tunataka kufikia utukufu. Mtume Yohane anarudia wazo la Kristu katika injili kuwa yeyote anayezishika amri zake kwa maneno na matendo yake huyo anakaaa ndani yake na Kristu anakaa ndani ya mtu huyo. Mtume Yohane anasema tukiishi namna hii tutakuwa na amani ya roho kwani dhamiri zetu hazitatusuta. Yeyote anayeishi kwa ujanjaujanja, uwongo na unafiki moyo wake daima humsuta na kumhukumu na hawezi kuwa na uhuru na amani ya Mungu

Katika somo la kwanza Paulo baada ya kuongoka alianza kuhubiri habari ya Kristu mfufuko yule aliyekuwa anamtesa  kupitia wafuasi wake. Kwa sababu ya historia yake mbaya dhidi ya wakristu, waamini wa Yerusalem wanasita kumpokea anapojaribu kujiunga nao. Ni jambo la kawaida pengine kwa hicho walichokifanya wakristu hao, hata mimi na wewe leo hii tungeweza kuwa na wasiwsi kama wao. Wakati wakristu wengine wanahisi kuwa Paulo anakuja kuwapeleleza Barnaba anafanya kitu cha kijasiri cha kutanguliza mtazamo chanya kwa Paulo ili kumpa nafasi ya kuthibitisha uzuri wake.Barnaba pia anatufundisha kuwa tusiwahukumu watu kwa maisha yao ya zamani bali kwa jinsi wanavyoishi sasa. Walau tuamini kuwa kuna uwezekano wa wadhambi kuongoka kama ambavyo inaweza kututokea sisi katika maisha yetu. Wapo watu ambao wakishamchukulia mtu kuwa mbaya hiyo itadumu daima bila kuruhusu uwezekano wa kubadilika, hii ni mbaya kwa mkristu. Hivyo pamoja na tahadhari tunazochukua lakini tuweke uwezekano wa wema pia. Huu ndio upendo wa Kristu.


Si jambo rahisi kuishi fadhila hizo tulizoziona katika masomo ya leo. Utakatifu wa maisha unafikiwa kwa kufanya sadaka kubwa. Tunapaswa kupigana vita kubwa ya Kiroho na kuishinda. Ni  ajabu kuwa pamoja na kufahamu ukweli huu na  ya kwamba tunahitaji msaada wa Mungu katika jitihada zetu lakini tumekuwa wazito wa kutafuta msaada huo kwa njia ya sala na mafungo. Kijana yupo tayari kusali novena na kufunga chakula kwa siku kadhaa kwa ajili ya kuomba mchumba mwema, kufaulu mtihani au kupata kazi kitu ambacho ni kizuri, lakini hawezi kufanya hivyo kwa ajili kuomba neema ya kumsaidia asifanye tendo la ndoa kabla ya ndoa na mchumba wake. Daima atabaki na kusema tuu, aah ni udhaifu tu wa kibinadamu au ni shetani tu. Hakika tunahitaji kusali sana na kufunga ili tubaki tumeunganika Kristu daima.

Wednesday, 22 April 2015

DOMINIKA YA NNE YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 26, 2015

Somo I. Mdo 4:8-12, Somo II. 1Yn. 3:1-2, Injili Yn 10:11-18
Tunapoendelea kufurahia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu leo tunaalikwa kujitahidi kadiri inavyowezekana kwa kutegemea msaada wake Mwenyezi kubaki katika kundi la kondoo wa Kristu yaani kanisa lake. Yeye Kristu ni mchungaji mwema, daima anatupigania na kutulinda dhidi ya mbwamwitu wakali. Iwapo tutatoka katika kundi, na kutangatanga nje ya kundi, tutajiweka katika hatari ya kushambuliwa na mbwa mwitu wakali, lakini pia tunaweza kujikuta tumeangukia mikononi mwa wachungaji wanaofanya kazi kwa mshahara na hivyo kutojali sana usalama wetu.

Katika injili Yesu anasema kuwa yeye ni mchungaji mwema na kweli ndivyo alivyo. Ni mchumgaji mwema wa kondooo wake ambao ndio sisi wakristu. Ni mchungaji mwema kwa sababu yuko tayari kutoa uhai wake ili kutuokoa kutoka katika mikono ya mwbwa mwitu shetani anayetafuta kutumaliza. Anafanya kazi yake si kwa sababu anatafuta faida yake binafsi bali kutokana na upendo alionao. Anajua wazi kuwa kupoteza uhai wa kimwili kwa ajili ya kutulinda sisi si kitu kwake kwani ni njia ya kufikia utukufu, atausalimisha uhai huo katika ufufuko katika hali ya utukufu. Ni mchungaji mwema kwasababu anawajua kondoo wake na yuko tayari kuwatafuta kondoo wote waliopotea na kuwarudisha kundini.

Wakristu tulio kondoo wa Kristu tunatumwa kufanya kazi kati ya mbwa mwitu wakali, shetani na wafuasi wake wanaopinga kazi ya Kristu. Tuko katika hatari kubwa ya kiroho na kimwili. Shetani daima anatafuta nafasi ya kuangamiza uzima mpya tulioupokea katika ubatizo na katika sakramenti zingine hasa ekaristi na kitubio. Uzima unaotusadia kuepuka dhambi na kuendelea kumtumikia Mungu daima. Shetani pia anatafuta nafasi ya kuondoa uhai wetu wa kimwili ili kutoa vitisho kwa kondoo wengine ili watawanyike na  kumuacha nyuma mchungaji wao ha hivyo iwe rahisi kwake kuwakamata na kuwaangamiza. Neno la Mungu leo linalenga kutuondolea hofu dhidi ya Mbwa mwitu shetani. Tunaye mchungaji mwema ambaye yuko tayari kutoa uhai wake ili kulinda na kutetea uhai wetu wa kiroho tulioupokea kwa sakramenti. Lakini yupo tayari pia kutuondolea hofu dhidi ya kifo tunapofanya kazi ya kumtangaza. Kifo cha mwili si kitu kwetu ikiwa tuna uzima wa kiroho kwani ni mlango wa kufikia ukamilifu wa uzima huo wa kiroho mbinguni.

Katika somo la pili mtume Yohane anatueleza juu ya bahati tuliyo nayo ya kuwa wana wa Mungu. Kwa Kristu mchungaji mwema kuutoa uhai wake ametukumboa kutoka katika mikono ya shetani na kutufanya si watoto wa shetani tena bali wana wa Mungu. Uhusiano wetu umekuwa si tu wa Muumba na viumbe vyake bali Baba na wana wake. Ni uhusiano wa ndani uliojengwa katika misingi ya upendo. Mungu aliye Baba yetu yuko tayari kutupigania na kututetea dhidi ya muovu shetani ambaye kama alivyomuandama Kristu ataendelea kutuandama pia.  Tunafanywa kuwa wana wa Mungu kwa neema yake Baba kwetu lakini pia kwa jinsi tunavyopokea neema hiyo. Hakuna anayeweza kuwa mwana wa Mungu kama hajapokea mwaliko wa kuwa mwana kwa kuishi maisha ya nuru. hawa ndio kondoo ambabo Kristu asema kuwa walio wake anawajua nao wanamjua. Kufanyika wana wa Mungu ni mwanzo wa safari ya kuelekea kufanana na Mungu pale tutakapomuona uso kwa uso siku ya mwisho Kristu atakapokuja.

Katika somo la kwanza mitume wakiongozwa na Petro wanapata ujasiri wa kuendelea kumhubiri Kristu mfufuka mbali ya kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa wakubwa wa watu na wazee wa Israeli. Ujasiri huu unatokana na Imani yao kwa kristu aliyekwisha kuambia tayari kuwa yeye ni mchungaji mwema yuko tayari kuwapigania kondoo wake dhidi ya mwovu shetani anayepambana kuwanyima watu mbingu. Ufufuko wa kristu umewathibitishia ukweli huo sasa hawana hofu tana na kifo ambacho shetani hutumia ili kuwakatisha tamaa wana wa Mungu katika jitihada zao za kumhubiri Kristu.

Kristu mfufuka anatupigania daima katika maisha yetu. Pamoja na kwamba Kristu anatulinda dhidi ya hatari za kimwili pia, lakini hasa yuko tayari kutoa uhai wake ili tusipoteze uhai wa Ki-Mungu ndani ya roho zetu  yaani neema ya utakaso tunayoipata kwa kupokea sakramenti zake. Anapotulinda uhai wa kimwili anataka bado tuendelee kuishi duniani ili tuufanyie kazi uhai wa Ki-Mungu  ndani ya roho zetu. Vinginevyo magonjwa, mateso, mahangaiko na hata vifo vinavyotokea kwa wana wa Mungu havina madhara kwa uzima wa Ki-Mungu ndani ya roho zetu  ila badala yake vikipokelewa kwa imani ni njia ya kupata  uzima wa milele Mbinguni.


Monday, 13 April 2015

DOMINIKA YA TATU YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 19, 2015

Somo I. Mdo 3:13-15, 17-19a, Somo II. 1Yn 2:1-5a, Injili. Lk 24:35-48
      
Kristu mfufuka analeta habari njema ya ondoleo la dhambi. Neno la Mungu laendelea kutusisitiza kuwa ufufuko wa Kristu ni ushindi dhidi ya dhambi na hivi namna sahihi ya kuupokea na kuuishi ufufuko huo ni kutafuta nafasi ya mara kwa mara ya kujipatanisha na Mungu wetu kila tunapoanguka dhambini na hasa dhambi za mauti.

Katika injili leo Kristu anawatokea mitume katika chumba na akiwa huko anakula chakula pamoja nao baada ya kuwaonesha makovu ya mikono yake na miguu yake. Yesu anayafanya haya ili kuthibitisha kuwa katika ufufuko wake yeye si  roho tupu wala si mzuka bali ni Mungu kweli na mtu kweli ambaye mwili wake wa kibinadamu  haukuhairibiwa wala kupotea katika kifo bali umegeuzwa na kuwa katika hali ya utukufu. Kwa kuonesha makovu ya miguu na mikono yake Kristu analenga pia kuonesha kuwa ufufuko wake umekuja baada ya kuvumilia mateso makali ya msalaba kwa ajili ya wokovu wetu. Hivi ndivyo tutakavyokuwa siku ya mwisho atakakapokuja. Sisi sote tunatumwa kuwahubiria watu kuwa sasa tumepata ondoleo la dhambi kwa ufufuko wa Kristu.

Petro katika somo la kwanza anawatangazia watu habari ya toba. Anawaeleza Wayahudi kuwa, pamoja na kwamba walimkana Yesu mbele ya Pilato aliyetaka kumfungulia Yesu lakini wao wakataka mhalifu ndiye afunguliwe yaani Baraba lakini Yesu asiye na hatia ndiye auawe, Kristu mfufuka anawasamehe dhambi yao kwa kuwa hawakujua watendalo. Anawaalika watubu warejee ili dhambi yao ifutwe kwasababu sasa wamejua maana ya mambo yote yaliyotokea kama yalivyoaguliwa na manabii tangu zamani. Wayahudi hawakujua watendalo lakini sasa wamejua ni heri kwao lakini wanawajibika sasa kuishi toba vinginevyo adhabu inawangoja. Yeyote anayeshupaa katika ouvu hata baada ya kuoneshwa uovu wake na kuonywa ataangamia.

Katika somo la pili mtume Yohane kawenye barua yake anawaasa wakristu wote juu ya kuepuka dhambi  na daima wawe wepesi wa kuungama pale wanapoanguka. Yohane amekwishatueleza kwenye sura ya kwanza ya barua hii kwamba ni uongo kwa mtu kusema hana dhambi na kweli haimo ndani yake. Mtume Yohane anaona hatari kubwa ya watu kubweteka kutokana na maeno haya wasione haja tena wala wasipate  msukumo wa kujibidiisha katika kuepa dhambi. Yohane pia kwenye sura hiyo ya kwanza anasisitiza kuwa tukiziungama dhambi zetu yeye (Kristu) ni mwaminifu atatusamehe dhambi. Kuna hatari pia watu wakaitumia vibaya huruma hii na wasione haja ya kuungama wakiamini kuwa huruma itakuja tu. Katika somo la leo Yohane anaweka msisitizo juu ya kuepuka dhambi na umuhimu wa kuziungama dhambi zetu. Kumjua Mungu maana yake ni kushika amri zake.


Kuepa dhambi ni vita kubwa sana kwani shetani hapendi kabisa kuona kuwa tunaongoka. Vita hii inahitaji utayari wetu, ujasiri na jitihada zetu tukipata nguvu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Lazima tutambue kuwa hakuna njia nyingine zaidi ya kujipatanisha na Mungu wetu ikiwa tunataka kufurahia matunda ya utukufu wa ufufuko.

Friday, 10 April 2015

DOMINIKA YA PILI YA PASAKA MWAKA B. APRIL 12, 2015

Somo I. Mdo 4:32-35, Somo II. IYn 5:1-6, Injili Yn 20:19-31
Fadhila ya imani ni kushawishika kwa moyo na kweli za KiMungu bila kutegemea tu ushahidi wa  milango yetu ya fahamu. Ufufuko wa Yesu ni ushindi dhidi ya kifo cha mwili na cha roho. Ushindi huu unatuingiza katika maisha mapya ya furaha milele, maisha yasioyoonja taabu ya aina yeyote ile milele yote. Furaha hii ya milele tutaipata kikamilifu mara ya baada ya kumaliza maisha yetu ya hapa duniani. Furaha hii inapita furaha zote za ulimwengu huu. Pamoja na kwamba hatujawahi kuipata furaha hiyo lakini tuamimi kwamba ipo na tutaipata.

Imani ya Tomaso kwa Yesu Mfufuka  kadiri ya  injili ya leo inategemea tu ushahidi wa milango ya fahamu. Baada tu ya kumuona Tomaso anamkiri kuwa Bwana wake na Mungu wake na kuanzia hapo anapata tamanio la kuungannika na Kristu huyu mfufuka na anaishi kadiri ya tamanio hilo hadi kufa shahidi. Hatuoni kwamba Kristu amestaajabishwa sana na imani ya Tomaso baada ya ungamo lake. Badala yake Kristu anawabariki wale wote wanaotamani kuunganika na Kristu kwa kusikia tu habari zake kutoka kwa watu wengine na sauti ya dhamiri zao bila ya kumuona wala kugusa madonda yake. Kristu ni kama vile anamwambia Tomaso ikiwa kila mtu atakayefuata baada ya yeye kwenda mbinguni akahitaji kumuona na kugusa madonda yake  ili amwamini hata baada ya kuhubiriwa, hakutakuwa na waaamini kwani hawatapata nafasi ya kumuona na kumgusa Kristu.

Katika somo la kwanza, Wakristu wa kanisa la kwanza walishawishiwa juu ya  ufufuko wa Kristu kwa mahubiri ya mitume peke yake bila kuhitaji kumuona wala kumgusa Kristu. Ufufuo wa Kristu ulibadilisha mtazamo wao. Uliwafanya  waamini kuwa maisha ya Mbinguni yana raha zaidi kuliko raha za dunia hii zinazotokana na mali ingawaje hawajawahi kuishi mbinguni. Tamanio hili la maisha ya raha ya Mbinugni liliwafanya waone kuwa si tatizo kwao kufanya kila kitu shirika, kila mtu kutoa mali zake kwa ajili ya maihitaji ya jumuiya.

Neno la Mungu katika somo la pili linatueleza kuwa imani yetu kwa kristu, Mungu kweli na mtu kweli, inatufanya tuushinde ulimwnegu. Kristu aliyekubali kuwa mtu alionja upinzani mkali kutoka ulimwengu huu, nguvu kama vile mateso, uchungu, umasikini, ubinafsi, mali,  zinazotaka ufalme wa Mungu usienee duniani. Yesu mtu kweli alishinda vita dhidi ya nguvu zote hizi pinzani na daima alikuwa mtii kwa mapenzi ya Mungu. Yeyote anayemwamini Kristu Mungu kweli na mtu kweli, aliyeshinda upinzani wote huu katika ubinadamu wake daima atauushinda ulimwengu katika nguvu zake zote pinzani dhiidi ya mapenzi ya Mungu.


Binadamu kwa hulka yetu tunahitaji ishara ili tuamini jambo na ndio maana mara nyingi tuko tayari kusoma kwa bidii sana kwa sababu tunaamini kuwa mafanikio yetu kimaisha yanategemea elimu kubwa. Imani hii tumeipata kwa sababu tumemuona baba, mama, kaka dada au rafiki aliyefanikiwa katika masomo. Linapokuja swala la kufanya juhudi kubwa kuachana na vilema vyetu vya dhambi vinavyotusumbua ili tupate maisha ya raha mbinguni hadithi n itofauti na sababu kubwa ni kwamba kwa uhakika hatuna mfano tulioona wa mtu aliyefanya hivyo na sasa anapata raha mbinungi. Tumuombe Mungu atupe paji la imani tuweze kuamwamini Kristu pasipo kumgusa wala kumuona

Saturday, 4 April 2015

DOMINIKA YA PASAKA, MWAKA B. APRIL 5, 2015

Somo I. Mdo 10:34, 37-43, Somo II.  IKor. 5:6-8, Injili. Mk 16:1-7

Leo kanisa linaadhimisha fumbo la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu.  Masomo ya leo yaeleza kuwa ufufuko wa Kristu ni ushindi na  ya kwamba sisi tunatumwa kuwa mashahidi wa ushindi huo kwa maneno na matendo yetu. Ufufuko wa Kristu unaleta maisha mapya, maisha katika Kristu, maisha ya milele  ambayo mwanzo wake ni hapa duniani na ukamilifu wake ni mbinguni. Wale wanawake watatu waliokwenda kaburini kadiri ya injili ya leo walikuta kaburi li wazi na tupu, halina mwili. Lakini pale ulipolazwa mwili waliona vitambaa alivyofungwa Yesu vimelala. Yesu amefufuka maana yake uzima wake wa kibinadamu wa kimwili kupitia kifo chake umegeuzwa na kuwa uzima mpya wa umilele, uzima usiokuwa na mipaka ya muda na mahali  uzima usiokuwa na mahangaiko tena na ndio maana sanda na vitambaa vingine  alivyofungwa wakati wa kuzikwa vilibaki kaburini Yesu alipofufuka. Hivyo ufufuko wa Yesu maana yake ni kupata maisha mapya ya umilele katika mwili mpya wa utukufu. Sisi sote baada ya kumaliza maisha ya hapa duniani tukiwa wenye imani tutafufuliwa na kuwa kama Yesu na kuingia kwenye furaha ya milele na miili yetu ya utukufu.

Petro anahubiri juu ya Kristu mfufuka katika somo la kwanza. Petro anatoa ushuhuda kuwa ufufuko ni ushindi dhidi ya mateso na kifo cha mwili. Wayahudi walimwua lakini Mungu alimfufua siku ya tatu. Si tu ushindi dhidi ya kifo cha mwili lakini Petro anasema kuwa ufufuko huu ni ushindi dhidi ya kifo cha roho yaani dhambi na ndio maana anamalizi kwa kusema kuwa kila amwaminiye atapokea ondoleo la dhambi, maneno yale ambayo Kristu alimwambia Martha kuwa kila amwaminie ajapokufa atakuwa anaishi(Yn 11:25). Petro anasema kuwa Kristu aliwaamuru wawe mashuhuda wa habari hii njema ya ufufuko kwa maneno na maisha yao. Lazima kila mkristu aushuhudie ufufuko wa Kristu kwa kuhubiri na kuishi vema. Unapozidi kushupaa katika dhambi bila kutafuta nafasi ya kufufuliwa na Kristu wewe huamini  kwamba Kristu alifufuka.

Katika somo la pili mtume Paulo anatuasa kuwa maisha ya ufufuko yanadai kuachana na chachu ya kale yaani dhambi na kuwa donge jipya yaani mioyo mipya. Sisi  tuliofufuka pamoja na Kristu hatupaswi tena kuridhika na dhambi. Paulo anaongea haya katika mazingira ambapo katika kanisa la Korintho kulikuwa na maovu makubwa, uasherati ulizidi kiasi cha mtu kutembea au kulala na mke wa baba yake yaani mama yake wa kambo. Kilichomkasirisha Paulo ni kwamba kama jumuiya ya waamini walilifumbia macho jambo hili, wakaridhika na maisha yaliendelea kama kawaida. Paulo anawaambia wasikubali kuwa karibu na dhambi wakaridhika kwani dhambi ni kama chachu ambayo inasambaa taratibu mpaka ngano yote inachachuka. Watu taratibu wataanza kuiga mfano baya wa mtu huyu wakiona kuwa ni kawaida. Tunapaswa tushtuke, tusikitike tuone uchungu kila tunapoona matendo maovu yakifanywa na watu wengine au na sisi na tuchukue hatua. Tuna uhakika kwamba mapamabano yetu dhidi ya dambi yatafanikiwa kwasababu tunaye Kristu aliyeshinda dhambi kwa ufufuko wake.

Katika somo la injili, mwinjili Marko anatueleza habari ya ufufuko wa Kristu. Marko pekee kati ya wainjili wote anasimulia kuwa yule mjumbe wa Mungu aliyewaambia wale wanawake habari ya ufufuko alitamka kwao kuwa waende  wekawaambia wafuasi na Petro kwamba Kirstu mfufuka amewatangulia Galilaya.   Marko anaweka msisitizo si tu kwamba wakawaambie wafuasi lakini na Petro. Kwa maneno haya Marko anataka kuonesha kuwa ufufuko wa Yesu umeshinda dhambi ya Petro ya kumkana Bwana wake mara tatu. Petro kwa sababu alimwamini na kumpenda Yesu hata alipokufa katika dhambi ya kumkana Yesu anaendelea kuishi. Petro anaishi kwa sababu hakuridhika na kumkana Yesu, tendo lile lilimpa uchungu, masikitiko na mahangaiko ya moyo na hivyo akatafuta nafasi ya kuamka na kuanza tena na kwa sababu hiyo Kristo alimfufua.

Ufufuko wa Kristu unapaswa kutupatia mtazamo mpya wa maisha yetu ya hapa duniani. Tunapaswa sasa kuyaona maisha ya hapa duniani kama maandalizi ya maisha ya milele. Tukiyatazama mambo yote ya ulimwengu huu kama msaada wa kutufikisha kwa Mungu hatutakuwa na hofu tena, hofu ya mambo ambayo dunia inayaona kuwa ndio kila kitu. Hatutakuwa na hofu ya kifo tena kwasababu ni mlango wa maisha ya umilele. Tutakuwa watu wa kutoa zaidi kuliko kupokea, watu wa kutumikia zaidi kuliko kutumikie. Hatuna hofu ya kupoteza wala kuwa masikini kwa kutoa, hofu ya kudhalilishwa kwa kutumikia, hofu ya kuchekwa kwa kutunza ubikira mpka siku ya ndoa takatifu.


Thursday, 2 April 2015

IJUMAA KUU YA MATESO YA BWANA. APRIL 3, 2015

Somo I. Isa 52:13-53:12, Somo II. Ebr 4:14-16; 5:7-9, Injili. Yn 18:1-19:42
Kanisa zima linaadhimisha leo mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristu msalabani. Ni siku ya kwanza katika siku kuu tatu za pasaka ambayo tumeianza jana kwa adhimisho la karamu ya mwisho. Leo historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu inasomwa kadiri ya mwinjili Yohane. Tafakari yetu leo itatazama ushiriki wa wahusika  mbalimbali katika historia hiyo ili wahusika hawa wawe kama kioo cha kujitazamia uhusiano wetu na Kristu pamoja na wenzetu pia.

Mtume Petro ni mhusika anayemuendea Yesu katika ukweli na wala hakuwa na unafiki. Petro alimpenda sana Yesu na daima aliishi kama alivyo, alinena na kutenda kile alichoamini kuwa kinafaa machoni  kwa Yesu, pale alipotenda mazuri Yesu alimpongeza na pale alipotenda mabaya Yesu alimkemea ili ajirudi. Maisha ya Petro yamekuwa ni ya kuanguka na kuinuka.  Maaskari wanapokuja kumkamata Yesu, Petro anamkata sikio mmojawapo wa wale waliokuja kumkamata kwa upanga. Yesu anamsihi Petro arudishe upanga wake ili mpango wa Mungu utimie. Baada ya Yesu kukamatwa wanafunzi wengine wanakimbia lakini Petro anamfuata Yesu mpaka ndani mbele ya Kuhani mkuu. Baadae Petro aliyeonesha ushujaa mkubwa katika kumpigania Bwana wake aliyempenda anaanguka kwa kumkana mara tatu. Ni kweli Petro ameanguka lakini ameanguka katika mazingira ya kumfuata Yesu Kristu na ndio maana alipogundua amekosa aliamka tena kwa kutubu. Yesu anamsamehe Petro na kumuweka kuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa lake kwa sababu moyo wa Petro daima ulimtafuta Yesu, umeanguka katika safari ya kumtafuta Yesu, Petro ameamka ili aendelee mbele.

Annas ni mhusika fisadi aliyedhamiria kumuangamiza Yesu hata ikibidi kwa kukiuka misingi ya haki kwasababu alimpinga katika ufisadi wake. Annas alikuwa ni mmiliki vibanda au maduka yaliyokuwa yanauza wanyama na vitu mbalimbali kwa ajili ya kutolea sadaka hekaluni  na biashara hiii ilifanyika ndani ya hekalu. Wauzaji wa vitu hivi kwa ajili ya kutolea sadaka waliwauzia watu kwa bei kubwa sana kuliko kama wangenunua nje ya hekalu kiasi kwamba maskini walishindwa kumtolea Mungu wao sadaka. Watu walilazimika kununua vitu hivi ndani ya hekalu kwa sababu vitu vilivyonunuliwa nje daima vilichunguzwa ubora wake kama vinafaa na mara nyingi kama si mara zote vilikataliwa. Hivyo Annas aliye wahi kuwa kuhani mkuu huko nyuma, kati ya mwaka 6 B.K n 15 B.K , alijipatia faida hekaluni kwa kuwanyonya maskini. Kadiri ya mwinjili Yohane,( Yn 2:15-25), Yesu alikasirishwa sana na vitendo hivi vilivyonajisi hekalu na kuamua kuwatimua wafanya biashara hekaluni. Annas,  akiwa bado ana ushawishi katika ofisi ya kuhani mkuu ambayo kwa wakati huu ilikuwa inakaliwa na shemeji yake Kayafa na pia kwa watawala, anaamuru Yesu aletwe kwake kwanza kabla ya kwenda kwa Pilato. Wayahudi walikuwa na sheria kuwa mtu hawezi kuhukumiwa kwa ushahidi wake mwenyewe hivyo hapaswi kuulizwa maswali ili atoe ushuhuda wake mwenyewe, lakini Annas anakiuka misingi hiyo kwa kumuuliza Yesu swali na Yesu anamkumbusha juu ya utaratibu kwamba awaulize watu , wao ndio watatoa ushuhuda juu yake. Yesu akahukumiwa kabla ya kesi kusikilizwa maana watu hawakuulizwa watoe ushuhuda.

Wayahudi ni wahusika wenye chuki kubwa sana dhidi ya Yesu kiasi kwamba inawaziba, macho, akili na mioyo yao wasione, wasiwaze wala kuamua sawaswa. Wayahudi tangu mwanzo walipinga vikali kulipa kodi kwa Kaisari na sababu yao kubwa ilikuwa kaisari ni mpagani, Mungu pekee aliye mfalme wao ndiye anastahili kupokea kodi yao. Mafasarisayo wanapomwendea Yesu na kumuuliza juuu ya uhalali wa kulipa kodi kwa kaisari(Lk 20:22), wanataka kumtega kuona kama na yeye anawaunga mkono ama la ili kupima Umasiya wake. Pia wayahudi tangu mwanzo walijitambua kama taifa linalooongozwa na mfalme mmoja tu naye ni Mungu (1Sam 12:12), lakini leo Pilato anapowauliza nimsulibishe mfalme wenu wanajbu kwa nguvu kabisa kuwa wao hawana mflame isipokuwa kaisari yule ambaye wanakataa kumpa kodi kwa sababu ni mpagani,  yule ambaye hawamtambui. Hii yote ni kwa sababu ya chuki.

Pilato ni mhusika asiyekuwa jasiri katika kusimamia mambo ya msingi na hasa haki. Pilato tayari alishaingia katika mgogoro na wayahudi, na wayahudi walimshitaki kwa Kaisari. Linapotokea hili Pilato anaogopa asipofuata matakwa yao watampeleka tena kwa kaisari na kibarua chake kitakua matatani kwasababu tayaria ana onyo. Pilato anafanya kituko kingine anapoweka chapa juu ya msalaba wa Yesu iliyokuwa inasema Yesu Mnazareti Mflame wa Wayahudi, Wayahudi walipombishia asiandike hivyo alishupalia msimamo wake, akasema niliyoandika nimeyaandika. Pale ambapo alitakiwa awe na msimamao katika kuhakikisha jambo la msingi kama haki ya kuishi inalindwa ameshindwa kushupalia msimamo wake hali aikijua fika kuwa Yesu hana kosa, lakini kwenye hili la chapa ambalo halina madahara yeyote haogopi macho ya Wayahudi anasimamia msimamo wake. Hata kwenye maisha yetu tunaweka msimamo kwenye mambo yasiyo na msingi lakini kwenye mambo muhimu hatuwi na msimamo thabiti.

Maaaskari waliokuwa chini ya msalaba ni wahusika wasiojali mahangaiko ya watu bali maslahi yao kwanza. Walikuwa wanahangaika kugawana vazi la Yesu kwa kulipigia kura liwe la nani. Yesu anateseka sana msalabani lakini wao si kitu kwao, lililo  muhimu ni mali zake wazigawane vipi . Ni mara ngapi tumewashuhudia watu wakikimbilia mifukoni mwa majeruhi wa ajali kutafuta pesa, simu na vitu vingine vya thamani na kuwaacha wakihangaika hadi kufa. Lori la mafuta limepata ajali watu wanakimbilia kuchota mafuta badala ya kuokoa majeruhi. Ndugu katika familia wanaanza kugombania mali za baba wa famiila anayekaribia kukata roho kitandani. Tumepoteza roho ya huruma na kuwajali watu katika mahangaiko yao. Wakati mwingine si lazima tuchukue mali zao, lakini tuko tunahangaika ili tupige picha tuzitume kwenye mitandao ya kijamii. Hatuna moyo wa huruma na kuwasaidia watu katika mahangaiko yao.

Kila mmoja akiingia ndani ya moyo wake leo anapomuona Yesu anateseka anajivika uhusika upi kati ya hao wanaojitokeza katika simulizi la mateso?. Tukumbuke basi siku ya leo ni ya kujiweka chini ya Yesu wa msalaba na kumuomba msamaha pale tuliposhiriki katika kumsulibisha na pia kuzidi kumuomba neema yake atuimarishe pale tuliposhiriki katika kumpigania na kumtetea ili tuzidi kumpenda daima.


Wednesday, 1 April 2015

ALHAMISI KUU. April 2, 2015

MISA YA KARAMU YA BWANA
Somo I. Kut 12:1-8, 11-14,  Somo la II. I Kor 11:23-26, Injili. Yn 13:1-15

Adhimisho la Karamu ya Bwana ndio mwanzo wa siku tatu kuu za pasaka yaani Ijumaa kuu, Jumamosi Kuu na Dominika ya Pasaka siku ambazo kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana. Hivyo siku tatu kuu za pasaka zinaanza kwa adhimisho hili na kuishia na masifu ya jioni ya pili ya Dominika ya pasaka. Leo kanisa kwa adhimisho hili la karamu ya Bwana linakumbuka mambo matatu; Kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu, Kuwekwa kwa Sakramenti ya Daraja na Amri kuu ya Upendo kwa Jirani.

Yesu alikuja duniani ili tuwe na uzima na ameanza tayari kazi yake hiyo katika maisha yake ya hapa duniani na kwa namna ya pekee kwa kifo chake pale msalabani. Baada ya ufufuko Yesu anapaa mbinguni lakini anataka aendelee kutupatia uzima kama alivyokuwa anafanya hapa duniani hadi ukamilifu wa dahari. Ili kufanikisha hilo anaweka ekaristi yaani mwili na damu yake. Katika ekaristi takatifu Yesu anaendelea kubaki nasi ili  kutupa uzima pamoja na kwamba alisharudi kwa Baba. Kwa maneno haya “twaeni mle wote huu ndio mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu” na “twaeni mnywe wote hiki ni kikombe cha damu yangu, damu ya agano jipya la milele, itakayomwagika kwa ajili yenu na kwa ajili ya wengi kwa maondoleo ya dhambi, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, Yesu anaweka sakramenti ya ekaristi. Tuipokee sakramenti ya ekaristi kwa uchaji ili tupate uzima wa milele

Yesu alikuja Duniani ili kuanzisha safari ya ukombozi. Alifanya kazi hii kwa kufundisha, kuponya magonjwa, kulisha watu chakula cha mwili na roho, kuwapa faraja watu na kilele chake ni kifo cha msalaba. Baada ya ufufuko Yesu anarudi kwa Baba yake lakini anataka habari hii njema ya ukombozi wake iwafikie vizazi vyote hadi ukamilifu wa dahari. Anaweka sakramenti ya daraja ili kuwepo watu watakaomwakilisha na kufanya kwa niaba yake hapa duniani. Mitume wanawekwa rasmi kwa kazi hiyo kwa maneno haya “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, nao wanawarithisha vizazi vya mbele yao kazi hiyo kwa kuwawekea mikono.

Yesu katika karamu ya mwisho anaweka amri mpya ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Mapendo yanayodai kujinyenyekesha kwa hali ya juu kwa ajili ya kuwahudumia wengine. Tunajifunza yafuatayo kuhusu kuwekwa kwa amri ya mapendo kadiri ya injili ya leo;

Yesu hali akijua kuwa amepewa mamlaka yote na Baba yake na kwamba saa yake ya kutukuzwa imefika,  hadhi ii kubwa haikumpa kiburi na badala yake alijinyenyekesha kiasi cha kuwaosha miguu mitume wake kazi iliyofanywa na watumwa. Unapogundua kuwa una karama fulani au cheo fulani unapata kiburi na kujiona mtu wa kutumikiwa zaidi au unajinyenyekesha na kutumikia?

Yesu alijua kuwa ametoka kwa Mungu na ya kwamba anarudi kwake lakini hali hii haikumfanya awadharau wanadamu na kuwa mbali nao kana kwamba sio wa aina yake badala yake ndio wakati hasa  alikuwa karibu nao  kiasi cha kufanya kazi ya watumwa ya kuwaosha wengine miguu. Kadiri unapokuwa karibu zaidi na Mungu kwa matendo yako mema unajiona kuwa hupaswi kuongea na kuwakaribia wadhambi au unatafuta nafasi ya kuwaonesha upendo wa Mungu ili wamuongokee?

Yesu  pia alijua kuwa saa yake ya kusalitiwa na kukanwa na Yuda na Petro, kwa namna ya pekee, imefika. Hili halikumfanya Yesu awake hasira na chuki dhidi ya mitume wake na hasa Yuda na Petro. Badala yake Yesu anawaka moto wa mapendo kwao kiasi cha kuwaosha miguu kama mtumwa afanyavyo kwa bwana wake.


Adhimisho la Karamu ya Bwana litusidie ili tumpokee Yesu wa ekaristi kwa imani na uchaji, tuwapokee mapadre kama Kristu mwingine, na tujibidiishe katika kuishi upendo katika kweli.

Thursday, 26 March 2015

DOMINIKA YA MATAWI, MWAKA B. MARCH 29, 2015

Masomo ya Kumbukumbu ya Kuingia Bwana Yerusalemu kwa Shangwe
Mk 11:1-10 au Yn 12:12-16
Somo I. Isa. 50:4-7, Somo la II. Flp 2:6-11, Inj. Mk 14:1-15,47

Kanisa leo linaadhimisha dominika ya matawi ya mateso. Ni dominika ya matawi kwasababu tunakumbuka  kuingia Bwana Yerusalemu kwa shangwe ambako alishangiliwa na watu kwa kutikisa matawi ya mitende akiwa amepanda punda. Tunafanya kumbukumbu hiyo kwa kubariki matawi na kuingia kanisani kwa maandamano tukiongozwa na padre anayemwakilisha Kristu na kutikisa matawi yetu tukiimba hosanna mwana wa daudi. Dominika hii huitwa ya mateso pia kwa sababu inatuingiza kwenye wiki kuu ambamo tunaadhimisha mateso kifo na kuzikwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu. Kumbukumbu ya kuingia kwa Bwana Yerusalemu kwa shangwe ikiishia tu kuwa ishara ya nje haitakuwa na umuhimu kwetu kwa hiyo ni vema basi tukatakafakari juu ya maana ya ishara hiyo ili dhimisho la leo lizae matunda ndani yetu.

Tukio la Bwana kuingia Yerusalem kwa shangwe laonesha ujasiri wa Yesu wa kuyakabili mateso yake mwenyewe kwa ajili ya ukombozi wetu. Yesu anaingia Yerusalem wakati saa yake ikiwa imefika yaani muda muafaka wa kukamatwa, kuteswa na  kuuawa kwa ajili ya ukombozi wetu. Yesu akijua haya yote na ya kwamba yatatokea Yerusalem, walipo wakuu wa mahukani na mafarisayo waliowaka hasira na chuki dhidi yake; wakitafuta nafasi ya kumkamata kwa udi na uvumba, anaingia Yerusalemu kwa uwazi akiwa amepanda punda akijionesha mbele ya umma wa watu bila kuogopa watesi wake. nay a kwambahaya yote yatatokea Yerusalem. Katika hali ya kawaida ya mwanadamu Yesu angeingia Yesrusalem kwa siri na kujificha ili watesi wake wasimuone au pengine wapate shida kidogo katikaa kumtafuta. Lakini yesu anawarahisishia kazi kwa kuingia kwa uwazi. Anatufundisha ujasiri katika kupokea mateso ambayo hayaepukiki katika maisha yetu kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu

Kumbukumbu ya kuingia Yerusalemu kwa shangwe inatufundisha kuwa daima tumtafute Yesu kwa ajili ya wongofu ili tuwe tayari kumfuata katika hali zote za raha na taabu. Tusimfuate na kumkimbilia Yesu   kwa sababu ya kuvutwa na   uwezo wake wa kufanya miujiza au mambo yasiyokuwa ya kawaida, umahiri wake wa kuhubiri  au kwa ajili ya kutimiza malengo ya ubinafsi wetu. Kati ya watu waliokuwa wanamshangilia Yesu walikuwepo wengi waliomfuata kwa sababu walimuona akitenda miujiza mingi na hasa walivutwa na muujiza kwa kumfufua Lazaro kule Betania. Kwa ujumla wake pia wayahudi wengi walimshangilia Yesu wakidhani kuwa yeye ni masia wa kisiasa anakuja kuuupindua utawala wa Kirumi kwa mtutu ili awarudishie utawala wao. Hawakumshangilia Yesu kwa sababu ni Masiya anayekuja kuwatoa kwenye utawala wa dhambi. Kwa sababu ya malengo hayo potofu ndio maana watu wote waliomshangilia ndio waligeuka kuwa maadui wake pale msalabani

Tunaalikwa leo tuwe tayari kufungua mioyo yetu ili tusikie sauti ya Mungu na tujifunze mapenzi yake kwetu. Yesu daima amekuwa akiwafundisha watu ili waelewe kuwa yeye ni nani hasa na amekuja duniani kwa ajili ya kazi gani . Lakini kutokana na ugumu wa mioyo ya watu na hasa kwa sababu ya  ubinafsi hawakuwa tayari kusikia. Daima walibaki na mtazamo wao wa masia wa kisiasa. Kabla ya kuingia kwenye saa yake Yesu anafanya jitihada ya mwisho ya kuwafungua macho Wayahudi ili waelewe aina ya masiya anayewajia  kwa kufanya ishara ya nje,  mbinu ilizotumiwa na  manabii waliomtangulia  ili kuwafanya Wayahudi  walelewe ujumbe wa Mungu baada ya kushindwa kwa maneno, unaweza  kurejea (1Fal 11:30-2). Kwa kawaida Huko Palestina punda ni mnyama mwenye hadhi kubwa sana. Ni mnyama anayetumiwa na mfalme wakati wa amani. Kukiwa na vita mfalme hutumia farasi. Yesu anaamua kuingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa amepanda punda ili awafundishe kuwa yeye ni mfalme na masia lakini ni mfalme wa amani na upendo na wala si mfalme wa vita. Pamoja na kufanya hayo yote Wayahudi walishindwa kumuelewa kwa sababu mioyo yao ilifungwa na ubinafsi wao. Nasi tukiruhusu ubinafsi wetu ututawale hatutatoa nafasi ya kusikiliza sauti ya Mungu inayoutuelekeza kutimiza mapenzi yake.

Kristu anapoamua kupanda punda kama ishara ya mfalme wa amani  anatufundisha kuwa silaha bora ya kupambana na adui ni upendo, huruma na amani. Wayahudi walikuwa na adui ambaye ni utawala wa Kirumi uliwofanya kuwa koloni lao. Walimsubiria mkombozi atakayekuja kumshinda adui huyu na kumtoa  kwa upanga ili awarudishie utawala wao, lakini kwa kupanda punda Yesu anawaambia kuwa yeye ni Mkombozi anayekuja kupambana na adui kwa kumpa upendo na uhuruma ili  adui huyu aguswe  dhamiri yake na abadilike kuwa mtu mwema.

Wayahudi waliimba hosanna mwana wa Daudi wakimaanisha utuokoe kutoka lugha ya kiebrania. Kama ambavyo tumeona hapo awali, wokovu walioutarajia wayahudi kutoka kwa Yesu ni wokovu wa kisiasa yaani Yesu awaongoze katika vita ya kuwaondosha Warumi katika nchi yao na kuwapatia uhuru. Sisi tunapoimba  leo hosanna mwana wa Daudi  tunamuita  Yesu atuokoe kwanza kiroho yaani atuongoze katika vita ya kumng’oa Shetani katika roho zetu na kutupatia uhuru wetu wa roho ili tuwe na amani na furaha.  Lakini zaidi ya hapo tukisha okoka ndani yetu , Yesu atuokoe katika mifumo dhalimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayowafanya watu wateseke kwa kukosa chakula, malazi, afya bora, elimu na haki nyingine nyingi za binadamu


Tumuombe Mungu ili dominika ya leo ituingize vyema katika tafakari ya mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristu tusije tukafanana  na wale wa wayahudi ambao walimshangilia lakini muda mfupi baadae walimgeuka. Tufanane na mama bikira Maria na yule mwanafunzi, waliolewa maana ya Kristu kuteseka na wakakubali kuteseka pamoja naye ili wapate wokovu. 

Thursday, 19 March 2015

DOMINIKA YA TANO YA KWARESIMA, MWAKA B. March 22, 2015

Somo I:  Yer. 31:31-34, Somo II: Ebr. 5:7-9, Injili : Yn. 12:20-33

Tumebakiza wiki moja kabla ya kuadhimisha mateso na kifo cha Kristu. Katika dominika ya leo kanisa linaanza kutuingiza katika tafakari ya mateso ya Kristu. Neno la Mungu leo linatufunulia ukweli kuhusu thamani ya mateso ya Kristu ambaye aliteseka kama wanadamu wengine. Ili kuweza kuona thamani ya mateso katika maisha inategemea namna tunavyoyapokea. Kristu aliyapokea mateso kwa imani na hivyo Baba yake wa Mbinguni akamuonesha thamani hiyo na kumpa uhakika wa utukufu baada ya mateso. Baada ya kuelewa thamani hiyo Kristo alitii sauti ya Mungu katika kuyakabili mateso

Katika somo la kwanza nabii Jeremia anawapa Waisraeli habari njema ya Mungu kufanya agano jipya nao. Katika agano hili jipya Mungu anasisitiza juu ya uhusiano wake na mwanadamu unaodai kujitoa bila kujibakiza ndani ya moyo wa mtu. Anaposema kuwa ataiandika sheria yake ndani ya moyo wa mtu anamanisha kuwa anataka watu wampende Mungu si kwa matendo ya nje tu bali kwa moyo na akili zao zote. Watu wote watamjua Mungu ndani ya mioyo yao kwa sababu watakuwa wameondolewa giza la dhambi ya asili kwa agano hili jipya. Waisraeli walivunja agano la wanza kwasababu walisisitiza zaidi juu ya uhusiano wao na Mungu kwa matendo ya nje kuliko kujitoa nafsi. Kujitoa nafsi kwa ajili ya Mungu kunahitaji kutoa sadaka kubwa. Hakuna sadaka kubwa isiyokuwa na maumivu au mateso. Tunapokosa ujasiri wa kuyakabili mateso na  maumivu hayo hautewezi kuwa waaminifu kwa agano.

Katika somo la pili mwandishi kwa Waebrania anamuonesha Kristu Kuhani mkuu aliyetesekea pamoja nasi ili atufundishe namna ya kuyakabili mateso. Kwa sababu ya uchungu mkubwa anaoupata Kristu kutokana na mateso sala yake kwa Mungu ni ya kilio cha sauti na kumwaga machozi kama ilivyo kwa mwanadamu mwingine yeyote anapokuwa katika mateso makali. Kristu anatufundisha kupokea mateso kwa imani ili tuweze kujifunza mapenzi ya Mungu kwetu katika mateso yake. Kristu alijifunza kuwa mateso yake ni kwa ajli ya ukombozi wetu na baada ya kutambua hilo anakubali kutii mapezni ya Mungu.  Kwa sababu ya kupokea mateso kwa imani mateso yanamfanya Kristu awe mkamilifu katika kazi yake , hivyo nafsi tukiyapokea mateso kwa imani  tunakuwa wakamilifu katika kumtumikia Mungu.

Katika somo la injili Kristu anatufundisha kuwa kukubali na kupokea mateso yanayotokana na kujikana nafsi zetu, kutolea sadaka yale tunayoyapenda sana, kujikatalia haki zetu ikibidi haki ya kuishi kwa ajili ya kumtumikia Mungu na watu tutatoa mazao mengi na tutazisalimisha nafsi zetu katika uzima wa milele. Tutatoa mazao kama vile upendo, unyenyekevu , uvumilivu, msamaha na utu wema. Kuamua kutii mapenzi ya Mungu katika mateso makali kuna ugumu mkubwa, kuna hofu nyingi  na kunahitaji sadaka kubwa. Hivyo kutii kwa kweli ni kuamuna kusonga mbele katika hofu nyingi na kushinda na hapa ndipo penye fadhila. Kristu alikabiliana na ugumu na hofu nyingi katika kuamua kutiii mapenzi ya Mungu katika mateso yake. Alifika mahali alimuomba Baba amuepushe na saa ya mateso lakini alikabiliana na hofu na ugumu wote na akaweza kutii. Tukiwa watu wa  sala daima Mungu hatuachi peke yetu katika kuyakabili mateso. Atakuwepo kwa ajili ya kututia moyo, atatuonesha mapenzi yake na namna ya kutii sauti yake. Katika injili Yesu anapokuwa na mahangaiko na hofu nyingi kuhusu mateso atakayoyapata sauti inatoka mbinguni na kumhakikishia kuwa mwisho wa mateso hayo ni utukufu.

Mwanadamu anapitia mateso mbalimbali katika maisha yake. Yapo mateso yanayotokana na dhambi zake mwenyewe, mateso haya si ya kuyakimbilia tunapaswa kufanya juhudi ya kuyaepuka. Kristu amekuja kutuondolea mateso haya kwa kifo chake msalabani na tukitaka kuendelea kuyaepuka ametuachia sakramenti zake na hasa ya ekaristi na kitubio. Yapo mateso ambayo hatuwezi kuyaepuka kwa sababu ya udhaifu wa miili yetu, kwa mfano, mateso yatokanayo na magonjwa. Haya ni mateso ambayo hata Kristu mwenyewe hakuyaondoa katika ulimwengu huu. Badala yake ametufundisha namna ya kuyakabili kwa imani ili tuweze kutambua mapenzi yake kwetu. Mateso haya tukiyapokea kwa imani na matumaini yanatusaidia katika malipizi ya dhambi zetu na za ulimwengu. Yapo mateso mengine ambayo hayaepukiki ikiwa tunataka kuwa wakimilifu kiroho na hata kimwili, mateso haya yanatokana na uamuzi wetu wa kujikatalia nafsi zetu, mambo tunayoyapenda kwa ajili ya Mungu na jirani. Unapojikatalia chakula katika kipindi hiki cha kwaresima unapata maumivu ya njaa lakini lengo lako ni kujitawala katika chakula ili upate nafasi ya kujibandua katika vitu vinavyopita na kukuza uhusiano wako na Kristu


Tunapoadhimisa dominika hii ya tano tumuombe Mungu atujalie kupokea mateso kwa moyo wa imani na matumaini ili tustahilishwe wokovu kwa mateso hayo.